Bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa zapungua Zanzibar

Muktasari:
Bei za mafuta hupangwa kulingana na mwenendo wa soko duniani
Unguja. Gharama za mafuta ya taa, dizeli na petroli zimepungua Zanzibar ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Maji (Zura) imetangaza bei mpya za mafuta yakiwamo ya taa ambayo hayajawahi kupungua kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Akitangaza bei hizo leo Jumapili Juni 8, 2025, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Hassan Haji amesema bei mpya zitaanza kutumika kesho Juni 9, 2025.
Kwa mujibu Zura, lita moja ya petroli itauzwa Sh2,968 kutoka Sh2,969 ya Mei sawa na punguzo la Sh1 ( asilimia 0.03).
"Bei ya dizeli itauzwa Sh3,162 kutoka Sh3,191 ya Mei ikiwa ni tofauti ya Sh29 huku bei ya lita moja ya mafuta ya ndege itauzwa kwa Sh2,521 kutoka Sh2,537 ikiwa ni tofauti ya Sh16 sawa na asilimia 0.63," amesema Mbaraka.
Kwa upande wa mafuta ya taa, bei imeshuka kwa Sh50 kutoka Sh3,200 hadi Sh3,150 sawa na asilimia 1.56.
Hata hivyo, kwa zaidi ya mwaka mmoja bei ya mafuta ya taa ilikuwa haipandi wala kushuka ikiwa katika ya Sh3,200.
Akitaja sababu nyingine ya mafuta hayo (ya taa) kushuka kwa sasa amesema ni bohari ya mafuta hayo kuwa na kiwango cha kutosha badala ya utaratibu uliokuwa ukitumika wa kuagiza nishati hiyo kila wakati.
Amesema matumizi ya mafuta yanazidi kupungua mahitaji kutokana na hamasa ya kutumia nishati safi (gesi).
Mbaraka amesema baadhi ya vituo vya kuuzia nishati hiyo vinafikiria kubadilisha matumizi yake kuanza kuuza gesi na mafuta mengine.
"Na sisi mamlaka tutawakubalia kwasababu unakuta mtu anakaa na mafuta kwa muda mrefu yanashikilia fedha ambazo zingekuwa kwenye mzunguko," amesema Mbaraka.
Mamlaka huoangeza bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani na gharama za uingizaji katika Bandari ya Tanga.
"Kodi na zoto za Serikali, kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja na gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni zinazotumika kununulia mafuta," amesema Mbaraka.
Wakizungumza kuhusu kushuka kwa bei hizo, baadhi ya watumiaji wa mafuta wameshauri kuwa na bohari kubwa zaidi za kuhifadhia mafuta ili kuepusha mabadiliko ya kila mara.
Said Hussein Ali, mwendesha bodaboda ameishauri Serikali kurejea utaratibu wake wa kutoa ruzuku ili kupunguza gharama hizo kwa kiwango kikubwa zaidi.
"Ukiangalia kiwango kilichopungua kwa petroli ni kidogo sana, shilingi moja kwa mtu anayenunua mafuta ya kawaida hata haoni kama imepungua labda kwa watumiaji wakubwa wa nishati hiyo," amesema.
Kuhusu kupungua kwa bei ya mafuta ya taa, Ashura Hamza Makame amesema nishati hiyo inapaswa ipungue zaidi kwa sababu bado yanatumiwa na watu wengi wa hali ya chini.