Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Mwinyi ahimiza utulivu, amani kuelekea uchaguzi mkuu

Muktasari:

  • Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kuwachagua marais, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amewataka viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa kuwe na amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Dk Mwinyi ameyasema hayo katika Baraza la Eid lililofanyika leo Juni 7, 2025 katika ukumbi wa Dk Ali Mohammed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kuwachagua marais, wabunge, wawakilishi na madiwani.

“Tuendelee kuiombea nchi yetu kuwa na amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu kwani mazingira ya utulivu ni nguzo muhimu ya kuimarisha maendeleo ya jamii,” amesema.

Katika hotuba yake, amewataka waislamu kuzingatia mafunzo yanayotokana na ibada ya Hijja, hususan utii, mshikamano na maadili bora ya kijamii katika kuilinda amani.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutekeleza ibada hiyo muhimu, ikiwemo kuharakisha uanzishwaji wa Mfuko wa Hijja, pamoja na kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Zanzibar hadi Saudi Arabia.

Amewaombea mahujaji wote walioko Makka warejee nyumbani salama, sambamba na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wagonjwa na wale waliotangulia mbele ya haki.

Dk Mwinyi ametumia fursa hiyo kutoa salamu za sikukuu kwa wananchi wote wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, huku akitoa pongezi kwa kamati ya maandalizi ya baraza hilo, Jeshi la Polisi kwa gwaride la heshima, pamoja na vyombo vya habari kwa kufanikisha utoaji wa taarifa kwa umma.

Baraza hilo limehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla; Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini, na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.