Prime
Wiki ya mchakamchaka uteuzi wa wagombea vyama vya siasa

Muktasari:
- Chama tawala cha CCM, tayari kimemteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Dk Hussein Mwinyi akiteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Dar es Salaam. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikikamilisha hatua ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea ubunge na udiwani, vyama vingine vya siasa vinaendelea na mchakato huo huku baadhi yao vikitarajia kuhitimisha kazi hiyo wiki ijayo.
Baadhi ya vyama tayari vimepata wagombea urais huku vingine vikijiandaa kwa mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo, vitafanya uteuzi wa wagombea wake wa nafasi za urais kwa upande wa Bara na Zanzibar.
Awali, vyama hivyo vilieleza dhamira yao ya kuwa na mgombea mmoja kwa nafasi ya urais, hata hivyo hilo linaonekana gumu kwa sababu kila chama kinaendelea na michakato yake ya ndani ya kuwapata wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani.
Viongozi wa vyama hivyo wameeleza namna walivyojipanga kusimamisha wagombea kwenye nafasi hizo huku wanawake wakipewa kipaumbele ikiwamo kuwapunguzia gharama za uchukuaji fomu kwenye baadhi ya vyama.
Chama tawala cha CCM, tayari kimemteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Dk Hussein Mwinyi akiteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Juni 28, 2025, chama hicho kilianza mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa nafasi za ubunge na udiwani. Mchakato huo ulikamilika Julai 2, 2025 ambapo makada 5,475 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge.
Wakati huohuo, vyama vingine vya ACT Wazalendo, CUF na NCCR Mageuzi vinaendelea kukamilisha mchakato wa kuwapata wagombea kwenye nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani.
Uchukuaji fomu unaendelea
Mwenyekiti wa Ada-Tadea, Juma Ali Khatib amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya chama hicho kwa nafasi za ubunge na udiwani bado unaendelea na wanatarajia utakamilika wiki mbili zijazo.
Amesema katika mchakato huo, chama hicho kimewaruhusu wanawake kuchukua fomu bila malipo yoyote ili kuwachochea wengi wao kujitokeza huku kikiamini kukiwa na wanawake wengi viongozi, maisha ya wananchi yatabadilika.
“Tunahamasisha wanawake wengi kuchukua nafasi za kugombea, tunafanya hivyo kuendana na falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan na 4R zake. Wanawake ni watu ambao wakipata nafasi ya kuongoza sehemu wanakuwa waaminifu na waadilifu, tofauti na wanaume,” amesema.
Amesema mwitikio ni mzuri na wanachama wengi wanachukua fomu huku wengine wakitoka vyama vingine kama ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF).
Kuhusu nafasi za urais, Khatib amesema tayari wamepata wagombea, akiwamo yeye aliyeteuliwa kugombea urais wa Zanzibar wakati Georges Busungu akiteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sasa hivi tunasubiri mchakato wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) ili wapate barua ya kwenda kuchukua fomu na mchakato wa kampeni uanze,” amesema mwanasiasa huyo.
Katibu Mkuu wa chama cha Sauti ya Umma (Sau), Majalio Kyara amesema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu katika chama hicho kwa nafasi za ubunge na udiwani utaanza Julai 15, 2025 na utakamilika Agosti 14. Mchakato huo utahusisha nafasi za uwakilishi, ubunge na udiwani upande wa Zanzibar.
Kwa upande wa nafasi ya urais, Kyara amesema tayari chama hicho kimepata wagombea ambao ni yeye kwa upande wa Tanzania Bara na Ali Mwalimu Abdallah kwa upande wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa DP, Philipo Fumbo amesema chama hicho kitashiriki uchaguzi na mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali unaendelea na wiki ijayo watakuwa na mkutano mkuu kwa ajili ya kuwateua.
“Mkutano huo una ajenda moja ya kuchagua wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urais wa Zanzibar pamoja na mgombea mwenza. Watu wengine wamejitokeza kutaka nafasi za uongozi,” amesema.
Amesema chama hicho kimeweka utaratibu kwa wanawake kuchukua fomu bila kulipia na hadi sasa wamejitokeza wanawake wawili kati ya watatu waliotia nia ya kugombea nafasi ya mgombea mwenza wa urais.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AAFP, Said Soud Said amesema fomu zimeanza kutolewa katika maeneo tofauti, lakini watafanya kikao cha pamoja kujadili waliochukua fomu kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Richard Lyimo amesema makada Bado wanaendelea kuchukua fomu na kurejesha maeneo mbalimbali nchini.
"Pazia litafungwa Julai 17, 2025 hapo ndipo tutakuwa na idadi kamili ya waliochukua Kisha tutaingia kwenye hatua za mchujo, ingawa kwa sasa bado sijapata takwimu ya waliochukua," amesema Lyimo
Kwa mujibu wa Lyimo, wamejipanga kuweka wagombea nchi nzima ili kuikabili CCM inayoweka wagombea majimbo yote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa United, Democratic Party (UDP), Saum Rashid amesema pazia lao wamefungua kuanzia Julai Mosi, 2025 na halitakuwa na ukomo hadi wanaingia kwenye Uchaguzi Mkuu.
“Tumeona tusiweke ukomo kwa sababu tunahitaji kupata wagombea wengi na hadi mwishoni mwa mwezi huu tutakuwa na mkutano mkuu tutatoa mwongozo sahihi wapi tumefikia tangu kufungua pazia,” amesema Saum.
Katibu Mkuu wa NLD, ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Doyo Hassan Doyo amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa nafasi za ubunge na udiwani unaendelea tangu kufunguliwa kwa pazia hilo Juni 30, 2025.
“Zaidi ya watu 80 wamechukua fomu za kutia nia kugombea ubunge, naamini idadi itaongezeka kwani pazia tutafunga Julai 30, mwaka huu. Mikoa kama Dar es Salaam, makada wamejitokeza katika majimbo yote,” amesema Doyo.
Kwa mujibu wa Doyo, si Dar es Salaam pekee, hata majimbo ya Jiji la Mwanza asilimia kubwa wamechukua fomu za kuwania ubunge na udiwani ingawa changamoto iliyopo ni kwamba vyama vyao ni vidogo wagombea wao hawatangazwi na vyombo vya habari.
“Tumejipanga kushindana na CCM, Mkoa wa Tanga katika majimbo 11 ya uchaguzi; Kilindi, Handeni Mjini, Handeni Vijijini na Tanga Mjini makada wamesha chukua fomu,” amesema Doyo.
Amesema hata katika Mkoa wa Simiyu, kati ya majimbo tisa ya uchaguzi wamechukua fomu kwenye majimbo matano, huku upande wa Mkoa wa Mbeya, amesema wamechukua fomu kuomba kugombea Jimbo la Rungwe, Kyela na Mbarali.
Hata hivyo, amesema bado anaendelea kukusanya taarifa kutoka mikoa mbalimbali ya wanaochukua fomu ya kutia nia kuomba nafasi mbalimbali
Katibu Mkuu wa chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Mwalimu Aziz amesema licha ya kumpata mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar, pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa nafasi ya ubunge na udiwani litafunguliwa rasmi kuanzia kesho Julai 4, 2025 na litaenda hadi INEC, watakapotoa ratiba yao,” amesema Aziz.
Kwa mujibu wa Aziz, matarajio yao ni kwamba hamasa itakuwa kubwa kwani wanaoonyesha nia ni wengi ikiwemo wanawake.
Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Dk Evaline Munisi amesema pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa ubunge na udiwani lilianza Julai Mosi na wanatarajia kufunga rasmi Julai 22, 2025.
“Tangu tumefungua hadi sasa, hakuna taarifa iliyonifikia kwa kuwa shughuli inafanyika ngazi ya mikoa lakini kuanzia wiki ijayo, zitakuwa zimenifikia. Mipango yetu ni kusimamisha wagombea nchi nzima kwa udiwani na ubunge,” amesema.
Alisema wamejipanga kuweka mgombea na hawana lengo la kuungana na chama chochote kama walivyowahi kuweka wazi msimamo wao.
Katibu Mkuu wa CUF, Husna Abdallah amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji unaendelea na pazia litafungwa rasmi Julai 15, 2025.
“Hadi sasa waliochukua fomu ya urais wa Tanzania wako wawili na urais kwa upande wa Zanzibar amechukua mmoja na udiwani na ubunge watu wanaendelea kuchukua fomu,” amesema Husna.
Husna amesema idadi kamili itatolewa baada ya kufungwa pazia hilo na kuanza vikao vya mchujo kupata wagombea wenye sifa na malengo ni kupata wagombea wanaokubalika kila jimbo.
Vyama kushirikiana
Akizungumza kuhusu vyama vya upinzani kushirikiana na kusimamisha mgombea mmoja kuikabili CCM kwenye uchaguzi kwa kiti cha urais, Doyo amesema vingi bado havijamaliza kufanya uteuzi.
“Tunashindwa kuendelea na hatua hiyo kwa sababu wengine bado hawajakamilisha michakato yao ya ndani, tumekwamia hapo watu wanatafuta fedha za mikutano mikuu,” amesema Doyo.