VIDEO: Mpina, Othman waiteka Unguja, wapokewa na umati
Muktasari:
- Kutokana na umati uliokuwapo uliofuatana na msafara, barabara za kuelekea bandarini, Darajani hadi viwanja vya Mnazi Mmoja na Maisara zimefungwa kwa muda.
Unguja. Umati wa wananchi na wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, mjini Unguja wamefurika kuwapokea watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Luhaga Mpina na Othman Masoud (Zanzibar) waliokwenda kujitambulisha.
Wananchi na wanachama hao walianza kujitokeza eneo la Bandari ya Malindi, ambako Mpina, Othman na Fatma Abdulhabib Ferej (mgombea mwenza) walitua mjini hapa leo Jumamosi Agosti 9, 2025 wakitokea Dar es Salaam.
Umati wa wananchi na wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, mjini Unguja wamefurika kuwapokea watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Luhaga Mpina na Othman Masoud (Zanzibar) waliokwenda kujitambulisha.
Watiania hao wamesindikizwa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Isihaka Mchinjita na Ismail Jussa (Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Katibu Mkuu, Ado Shaibu na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho.
Matembezi
Saa 4:10 asubuhi safari ya matembezi ya kuwatambulisha watiania hao ilianza eneo la bandarini ambako Othman, Mpina na Ferej walipanda gari moja la wazi na mbele yao walisindikizwa na viongozi waandamizi wa chama hicho.
Njiani walipungia mikono wananchi na wachama wa ACT-Wazalendo waliojitokeza kuwalaki wakati msafara wao ukipita.
Umati wa wananchi na wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, mjini Unguja umefurika kuwapokea watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Luhaga Mpina na Othman Masoud (Zanzibar) waliokwenda kujitambulisha.
Msafara huo uliosindikizwa na matarumbeta na muziki uliopigwa kutokea gari la matangazo ulilazimika kusima katika baadhi ya maeneo kusalimia wananchi.
Maeneo ambayo msafara huo umesimama ni Malindi, Soko la Darajani, makutano ya mataa ya Mkunazini, Kisiwandui hadi Kisonge, ambako walishuka na kutembea kwa miguu hadi 'Mnarani square' ambako matembezi yalihitimishwa yakichukua takribani dakika 50.
Barabara zafungwa
Kutokana na umati uliokuwapo uliofuatana na msafara huo, barabara za kuelekea bandarini, Darajani hadi viwanja vya Mnazi Mmoja na Maisara zimefungwa kwa muda.
Msafara ukiwa eneo la Darajani ambako ni eneo maarufu la biashara, baadhi ya wafanyabiashara waliacha shughuli zao na kufuatilia tukio wakiwa wamejipanga pembezoni kwa mistari miwili.
Watiania hao wapo uwanja wa Mnarani ambako watazungumza na wananchi na wanachama wa ACT-Wazalendo.