Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Upendeleo vyombo vya umma usijirudie uchaguzi mkuu ujao

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza kati ya Agosti 28 na Oktoba 28,2025 kitakuwa ni kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge, ambacho vyombo vya habari vinapaswa kutenda haki kwa wagombea wote.

Ukiacha maadili ya jumla ya uandishi wa habari yanayotaka habari ziwe za ukweli, sahihi na zisizotoa upendeleo kwa mgombea au chama cha siasa, zipo sheria mbili mahsusi ambazo zinasimamia wajibu wa wanahabari katika uchaguzi nchini.

Ni muhimu sana wadau wa uchaguzi wakazifahamu vyema sheria hizi kwani katika uchaguzi mkuu wa 2020, vyombo vya umma vilitajwa kutotenda haki kwa wagombea urais wa upinzani, na kupendelea mgombea anayetokana na CCM.

Nitatangulia kuainisha sheria hizi mbili ambazo zimetungwa mahsusi kwa ajili ua kuzuia upendeleo, halafu nitakuwekea utafiti wa maudhui ya uchaguzi mkuu wa 2020, ili mjue tulipotoka, tulipo na tunapotaka kwenda katika uchaguzi ujao.

Japokuwa sheria zipo hivyo, lakini ukisoma ripoti ya Utafiti wa ‘Ubora wa maudhui ya vyombo vya habari Tanzania 2020’ uliofanywa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), hali ni tofauti kabisa.

Utafiti huo ulichunguza uripoti wa vyombo vya habari uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ukihusisha sampuli 2,400 za kazi za kihabari zilizopatikana kwenye magazeti 14, vituo vya redio 14 na vituo vitano vya televisheni Tanzania Bara na visiwani.

Kulingana na ripoti hiyo, utafiti huo ulifanywa na Abdallah Katunzi wa SJMC na Christoph Spurk wa  Zurich University of Applied Sciences katika Institute of Applied Media Studies.

Matokeo yanaonyesha kutokuwepo kwa uwiano wa uripoti wa wagombea kati ya yule wa chama tawala (CCM) ikilinganishwa na wagombea kutoka vyama vya upinzani ambapo mgombea wa CCM, Joh Magufuli alipewa nafasi kubwa zaidi.

Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali ambavyo ni Daily News, Habari Leo, Zanzibar Leo, TBC Taifa, TBC1, ZBC Radio, na ZBC TV viliripoti kwa asilimia 81 taarifa za Magufuli ikilinganishwa na asilimia 26 ya Tundu Lissu wa Chadema.

Vyombo vya habari vya serikali viliripoti zaidi matukio ya CCM kuliko yale ya vyama vya upinzani ingawa japo kwa uchache, hali ilikuwa tofauti kidogo kwa Mwananchi, The Citizen, Mwanahalisi Online, Nipashe, Arusha 1 FM na ITV.

Kulingana na ripoti, vyombo hivyo viliripoti zaidi matukio ya vyama vya upinzani ikilinganishwa na ya CCM na kwa maneno mengine, vilitekeleza misingi ya dhima ya vyombo vya habari ya kutoa taarifa anuai kwa hadhira, yaani wapigakura.

Ripoti hiyo inasema maudhui ya sera za wagombea kama zinavyotolewa kwenye ilani zao za uchaguzi hayakuripotiwa kwa kiasi cha kutosha, bila kujali kwamba wapigakura walihitaji taarifa za kutosha ili kufanya maamuzi sahihi.

Sitashangaa kuona licha ya uwepo wa sheria mahususi, wapo baadhi ya wanasiasa na wananchi hawafahamu uwepo wa sheria hizi, lakini pia kuna mwandishi ukimuuliza juu ya sheria hizi hazifahamu na umma unamtarajia kutenda haki.

Ni muhimu sana kwa mwanasiasa yeyote anayegombea katika uchaguzi huu, iwe ni kiti cha Rais, ubunge au udiwani, kuzifahamu haki zao katika habari na matangazo yanayorushwa na vyombo vya umma na binafsi katika uchaguzi mkuu.

Sheria ya kwanza ni sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na marekebisho yake na Kanuni za Sheria ya Gharama za Uchaguzi za 2010 zilizochapwa katika GN namba Julai 9,2010 na marekebisho yake ya mwaka 2025.

Ukisoma sehemu ya VII ya kanuni hizi inahusu matumizi ya vyombo vya habari vya umma ambapo kifungu cha 21 kinasema wakati wa kampeni, vitatenga muda kwa ajili ya wagombea urais kutoka kila chama cha siasa, ili watumie kunadi ilani zao.

Kwa utekelezaji mzuri wa kanuni hii, kifungu kidogo cha (2) kinataka kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi mkuu, kiwasilishe nakala ya ilani ya uchaguzi ya chama chake kwa menejimenti ya vyombo vya utangazaji habari vya Serikali.

Lakini kifungu cha 22(1) kinasema kila gazeti la Serikali litaweka safu maalum kwa kila mgombea anayegombea kiti cha rais ili kutangaza na kuhabarisha umma juu ya ilani ya uchaguzi ya chama cha siasa kinachomdhamini mgombea huyo.

Nimeamua kuandika haya ili umma ufahamu kuwa vyombo vya habari vya umma ambavyo ni TBC1 na TBC Taifa, Daily News na Habari Leo vinaendeshwa kwa kodi yangu mimi na wewe hivyo wanawajibika kutopendelea mgombea yoyote yule.

Kuhusu vyombo binafsi, kifungu cha 23 kinasema kwa kutumia gharama zake mwenyewe, kila mgombea atakuwa na haki kutumia vyombo binafsi vya habari kwa ajili ya kufanya kampeni na atafanya hivyo ili kutangaza ilani ya uchaguzi.

Lakini ili kuweka usawa, kanuni hiyo inasema mgombea hatatumia vyombo hivyo vya habari kwa namna ambayo vinampa upendeleo na manufaa zaidi ukilinganisha na mgombea mwingine katika uchaguzi mkuu uliopo mbele yao.

Endapo hilo litakiukwa kifungu cha 24(3) kinasema chama cha siasa au mgombea anaweza kuwasilisha malalamiko kwa Msajili wa vyama vya siasa dhidi ya chama hicho, mgombea au mhariri wa chombo cha habari kilichotoa upendeleo huo.

Chama cha siasa au mgombea aliyeathiriwa na upendeleo huo anaweza kufungua maombi Mahakama Kuu na kuomba amri ikiwamo amri ya kumzuia mgombea, chama cha siasa, chombo cha habari au mhariri kuacha kukiuka kifungu hicho.

Sheria nyingine ni ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani namba 1 ya mwaka 2024 nayo imeweka vifungu mahsusi kwa vyombo vya habari vya umma vinavyotaka vitoe nafasi sawa kwa wagombea urais na makamu wao.

Kifungu cha 74, kinasema wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo watakuwa na haki ya kutumia huduma ya vituo vya umma wakati wa kampeni.

Kifungu kidogo cha Pili kinasema baada ya kushauriana na wagombea, vyama vya siasa vinavyohusika na maafisa wanaohusika na vyombo vya habari vya umma, INEC itaratibu matumizi ya haki za matangazo chini ya kifungu hicho.

Kila chombo cha habari kinachomilikiwa na Serikali kinachochapisha taarifa kitaongozwa na misingi ya kutopendelea wala ubaguzi kwa wagombea kwa kiwango cha nafasi kitakachotengwa kwa ajili ya wagombea wa nafasi hizo.

Kwa madhumuni ya utekelezaji wa kifungu hicho, sheria inasema Tume inaweza kutoa maelekezo kwa maandishi ambayo yatapaswa kuzingatiwa na chombo chochote cha habari kinachomilikiwa na Serikali.

Sasa tunakwenda katika uchaguzi mkuu 2025, ripoti ya utafiti wa uchaguzi mkuu 2025 kuhusiana na vyombo vya habari tumeiona je, vyombo vyetu vya umma vitarudia kosa lilelile la kimaadili na kisheria la kukipendelea chama tawala?

Pengine ujio wa Bodi ya Ithibati Tanzania (JAB) utatumia kifungu kile cha 12 cha sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kuhakikisha waandishi waliopewa Ithibati wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia maadili.

Kulingana na kifungu hicho, majukumu ya JAB ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa kanuni za maadili kwa wanahabari na kusimamia viwango vya maadili ya kitaaluma, weledi na nidhamu miongoni mwa wanahabari nchini Tanzania.

Kutoa upendeleo kwa kuruhusu matangazo ya chama kimoja zaidi na kuminya nafasi sawa kunafanya mizani iegemee upande mmoja hivyo wapiga kura watajikuta wanashawishiwa zaidi na sera za chama kinachopewa upendeleo.

Pamoja na sheria, uwepo wa JAB, upendeleo ule wa 2020 utajirudia?

0656600900