Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCK kupunguza hofu ya kustaafu kwa watumishi wa umma

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, akimkabidhi fomu ya uteuzi wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mgombea wa Chama cha Kijamii (CCK), David Daud Mwaijojele, leo Agosti 12, 2025, ofisi za Tume, Njedengwa, Dodoma.

Muktasari:

  • Mgombea urais CCK amesema sababu kuu inayowafanya watumishi wengi kuogopa kustaafu hata wanapofikia umri wa kustaafu ni kutokujua watakwenda wapi au watafanya nini baada ya kumaliza utumishi wao.

Dodoma. Mgombea wa nafasi ya Rais kupitia Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele, ametaja moja ya changamoto kubwa kwa watumishi wa umma kuwa ni hofu ya kustaafu, akisema wengi wao hukosa ujasiri wa kuacha kazi hata wanapofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza leo Jumanne, Agosti 12, 2025, baada ya kukabidhiwa rasmi fomu za kugombea urais, Mwaijojele amesema sababu kuu inayowafanya baadhi ya watumishi wa umma kusita kustaafu ni kutokujua watakwenda wapi au kufanya nini baada ya maisha ya ajira.

“Watu wengi wanaogopa kustaafu kwa sababu hawajajiandaa kisaikolojia wala kiuchumi. Hawajui wataishije au watakaa wapi baada ya kazi. Lakini suluhisho lipo,” amesema Mwaijojele, bila kufafanua kwa undani mapendekezo ya chama chake katika kushughulikia changamoto hiyo.

Mwaijojele ameahidi kuweka wazi mikakati ya CCK kuhusu masuala ya wastaafu katika kampeni zake za urais.

Hata hivyo, Mwaijojele amesema moja ya mikakati ya kuwawezesha watumishi wa umma kunufaika baada ya kustaafu ni kuanzishwa kwa mpango maalumu wa makato ya kodi, ambapo sehemu ya mapato yao itahifadhiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanapofikia umri wa kustaafu, wanakuwa tayari na makazi yao, hivyo kupunguza hofu ya maisha baada ya utumishi.

Mbali na watumishi wa Serikali, Mwaijojele ameahidi kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa migodini pamoja na waandishi wa habari, akibainisha kuwa makundi hayo hufanya kazi katika mazingira magumu yanayohitaji msaada na uangalizi wa karibu kutoka kwa Serikali.

Ameongeza kuwa masuala ya afya, elimu, mazingira na uchumi ni miongoni mwa maeneo atakayoyapa kipaumbele iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi.

Hata hivyo, alikataa kuingia kwa kina kuhusu mipango hiyo, akieleza kuwa ataweka wazi sera na ahadi zake baada ya kuteuliwa rasmi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).