Ilani ya ADC kuongeza umri wa kustaafu, matibabu bure
Muktasari:
- Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kinatarajia kuzindua Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ambayo wataitumia kuinadi kwa Watanzania ili kuwashawishi kuwapa dhamana ya kuwaongoza ikiwa imesheheni mambo lukuki ikiwamo ya huduma za afya bure.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shabaan Itutu ameeleza mambo lukuki yaliyosheheni kwenye ilani ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ikiwemo kuongeza umri wa kustaafu kwa wataalamu wabobevu kama madaktari kutoka miaka 60 ya sasa hadi 70.
Pia, matibabu bure, maiti hakuna kutozwa gharama hospitali, elimu bure, mikopo kwa wote, kuondoa utitiri wa kodi zenye kero kwa wananchi kama maegesho ya magari, kujenga viwanja vya kisasa vya mpira kila mkoa na pembejeo za kilimo, mazao kutozwa kodi hadi yanapokwenda sokoni na vifaa vya uvuvi kutozwa kodi.
Kiongozi huyo anaeleza hayo ikiwemo ukiwa umepita mwezi mmoja baada ya mkutano mkuu wa chama hicho, ulioketiwa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam na kuwateua wagombea urais watakaopeperusha bendera ya chama hicho, akiwemo Wilson Elias kwa Tanzania bara, Hamad Hamad Rashid kwa upande wa Zanzibar. Ambao watakuwa mstari wa mbele kunadi sera na kufafanua ahadi hizo kwa umma.
Akizungumza leo Jumatatu, Agosti 11, 2025 baada ya kumaliza mkutano wa kamati tendaji ya chama hicho, uliokuwa unapitia ilani hiyo kabla ya kufanya uzinduzi, Itutu amesema wao wameshamaliza kazi wameshaandaa wagombea makini na wanataka kura ya Mtanzania iwe sauti yake katika kufanya mageuzi.
"Wenzetu Chama cha Mapinduzi (CCM), miaka 60 ya uhuru wameshindwa kuwasaidia Watanzania, huu ni wakati wetu, ADC tumekuja na ilani iliyosheheni sera zinazokuja kujibu changamoto za wananchi.”
"Tumefanya tafiti zetu na tumeona hakuna chama chenye ilani iliyosheheni sera bora kama zetu ni jukumu la Watanzania kutupigia kura kwa wingi ili Oktoba 29, 2025 tuingie madarakani tuunde Serikali rafiki hatutaweka mawaziri mizigo tutaweka watu tunaojua wanaumia na changamoto zinazowatesa Watanzania," amedai Itutu.
Kuongeza umri wa kustaafu
Wataalamu wanasoma na kupata uzoefu kuanzia miaka saba tena kwa kutumia kodi za Watanzania, Itutu amesema lazima walindwe ili ujuzi walioupata utumike vile inavyotakiwa.
"Mathalan Tanzania madaktari na maprofesa wanatumia miaka mingi kusoma huwezi kusema wakifikisha miaka 60 wastaafu, jambo hili halijakaa sawa ADC kupitia ilani yetu tumesogeza hadi miaka 70 ili ujuzi waliousomea ulete tija kwa Watanzania," amesema.
Utafiti na uchaguzi walioufanya, Itutu amesema wamebaini wabobevu wanastaafu wengi ikiwa wametumika miaka michache na wanaenda kuomba ajira mataifa mengine.
"Tumefikiri kwa kina hatutaki hivyo, kupoteza watu hao muhimu na hata wakifikisha miaka 70 tutaangalia kama hali yao inaruhusu na wana nguvu tunawalinda kwa kuwapa ajira za mikataba," amesema Itutu.
Kuhusu suala la matibabu bure limefafanuliwa kwa ufasaha na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Hassan Mvungi aliyesema chama hicho kimejipanga kutoa matibabu bure na ikiwa ugonjwa utakuwa unahitaji ubobevu wa nje Serikali itagharamia.
"Nchi ina raslimali nyingi kila kona, wenzetu Zanzibar wameweza iweje huku tushindwe kwani wao wana jambo gani la ziada kutushinda, tumejipanga kujenga afya bora za Watanzania," amedai.
Wakati chama hicho kikijipanga kwa uzinduzi wa ilani hiyo kimeweka bayana Agosti 14,2025 wagombea wake wa urais wataenda kuchukua fomu za mbio za urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na kuanza mchakato wa kupita kutafuta wadhamini 200 kila mkoa.