Prime
Uchaguzi 2025: Kete ya ushindi kwa vyama

Muktasari:
- Oktoba 2025, Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Urais huku wadau mbalimbali wakionesha maeneo yanayopaswa kuzingatiwa ili vyama viweze kuibuka washindi.
Dar es Salaam. Licha ya malalamiko ya kasoro za kisheria katika mchakato wa uchaguzi, wadau wa siasa wanasema ipo kete ya ushindi kwa vyama vya upinzani katikati ya mazingira yanayolalamikiwa.
Miongoni mwa kete hizo kwa mujibu wa wadau hao ni kusimamisha wagombea wachache kwenye maeneo wanayokubalika na kuwekeza kwa wananchi.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa upinzani, wadau wameeleza kuwa, hata chama tawala cha CCM kina nafasi ya kudumisha ushindi wake, bila malalamiko iwapo kitaamua kufanyia kazi mabadiliko yanayohitajika na kikatumia uzoefu wake kushindana.
Hoja na mitazamo hiyo inaibuka katika mazingira ambayo, vyama vya upinzani na baadhi ya wadau wa siasa wamekuwa wakilalamikia changamoto za kisheria katika mfumo wa uchaguzi na hivyo kunyima mazingira ya haki na usawa wa mchakato wenyewe.
Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na muundo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (Inec), wanasema inatoa nafasi zaidi kwa chama tawala huku ikivididimiza vingine, kwa kuwa bado wasimamizi wa mchakato huo wanateuliwa na Rais ambaye naye ni miongoni mwa wagombea.
Wakati wadau wakiibuka na malalamiko hayo, Serikali imesema tayari ilikwishafanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi mwaka 2024 na inavishangaa vyama vinavyolalamika.
“Mwaka 2024 Bunge lilitunga, sheria mbili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na ile ya INEC. Tulifanya mabadiliko yale kwa sababu kulikuwa na wito uliotoka kwa vyama vya siasa na wadau mbalimbali,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari wakati wa kongamano la kwanza la kitaifa la kisheria.
Uwekezaji kwa wananchi
Akizungumzia hilo hivi karibuni, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amesema siri ya ushindi kwa vyama hasa vya upinzani ni kuwekeza kwa wananchi ili kupata kura nyingi.

Kura hizo, amesema hazitatosha kuvipa vyama hivyo ushindi wa kiti cha urais, lakini angalau zitavipa idadi ya kura zitakazoviwezesha kupata ruzuku na nafasi nyingi za wabunge wa viti maalumu.
"Hii inaweza kuwaokoa wakabaki na wabunge wa viti maalumu na watapata ruzuku kwa idadi ya kura watakazopata,” amesema.
Dk Masabo amesema uwekezaji kwa wananchi aghalabu unafanywa kwa kutafiti na kujua mwelekeo wao, kisha unaandaa sera zitakazowashawishi.
"Shida ya vyama vya upinzani miaka yote huwa havina sera mbadala ukisoma Ilani zao ni lugha tu inabadilika lakini mambo ni yale yale vinayoeleza," amesema.
Baada ya kujua mwelekeo wa wananchi, amesema vyama hivyo pia vinapaswa kuondoa hofu iliyopo kwa baadhi ya watu kuwa wasipokichagua chama fulani mambo yao hayatakuwa sawa.
“Lazima vyama hivyo vitengeneze na kujenga hoja zitakazoeleza ni kwanini wananchi wavipigie kura hata kama wanajua havitashinda nafasi ya urais,” ameeleza.
Kuungana
Kwa mujibu wa Dk Masabo, mbinu nyingi ilikuwa ni muungano wa vyama vya upinzani kukusanya nguvu za kuhakikisha vinapata kura nyingi katika maeneo mahususi.
"Lakini hii siioni ikifua dafu kwa sababu tayari vilishashindwa kushirikiana na vimeweka wazi misimamo yao. Hata hivyo. isingekuwa rahisi kushirikiana huku kila kimoja kina maslahi yake binafsi," amesema.
Zaidi ya mbinu hiyo, Dk Masabo amesema hakuna ushindi vinavyoweza kuupata zaidi ya kuingia makubaliano na mshindani mkuu kuomba viachiwe baadhi ya nafasi.
Ajenda
Mtazamo huo unashabihiana na ule uliotolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Dk Lazaro Swai akisema vijiandae kwa ajenda zitakazowashawishi wananchi kuvichagua.
Ajenda hizo, amesema ni zile ambazo zimekuwa zikitamaniwa na wananchi, hivyo wasiache kuugusa umma kwa kuongelea mambo yao.
“Wanachokitaka wananchi kwa sasa ni kusikia hoja ambazo zitawagusa moja kwa moja. Hawataki mambo ya jumla, kwa hiyo siri ya ushindi ni kuandaa ajenda za namna hiyo,” amesema.
Sambamba na hilo, amesema kukosekana mshikamano kwa vyama hivyo vya upinzani, kumevifanya vikose ajenda ya pamoja kuhusu uchaguzi.

Hatimaye, amesema kila chama kimebaki kushinikiza jambo lake kwa hoja zake, hivyo vimekosa nguvu ya pamoja.
Awali, ameeleza vilishikamana kusukuma ajenda ya mabadiliko ya Katiba hadi kukatokea kuundwa kwa kikosi kazi.
“Kwa sasa wamepoteza mwelekeo kuhusu hiyo ajenda kwa sababu kila mmoja ameshika lake. Yupo anayesema hakuna uchaguzi bila mabadiliko, wengine wanasema waende kushiriki,” amesema.
Amesema kuna umuhimu kwa vyama hivyo kujenga ushawishi ili vipate uwakilishi wa nafasi mbalimbali utakaoviwezesha kusukuma ajenda vikiwa na wazungumzaji kwenye vikao muhimu vya uamuzi.
“Wakisusia uchaguzi kwa mawazo yangu, moja kwa moja hata nafasi ya kupata wawakilishi kwenye nafasi mbalimbali wataikosa kwa hiyo nafasi yao ya kuzungumza inaendelea kuwa finyu,” amesema.
Siri nyingine ya ushindi, amesema ni kuhakikisha vinasimamisha watu wenye mvuto, hoja, ushawishi na hata watakapochaguliwa wawe na uwezo wa kufanya uamuzi.
Dk Swai amesema mbinu nyingine ni kuhakikisha vinasimamisha wagombea katika maeneo ambayo vina uhakika vinaungwa mkono zaidi.
Amesema hilo litawezesha rasilimali chache vya vyama zilizonazo zitumike katika uwekezaji zaidi kwenye maeneo ambayo vina nguvu na hatimaye kupata ushindi.
“Vikisema vinataka kuweka wagombea nchi nzima ilhali havina rasilimali inayotosha kupambania maeneo yote, vitakosa nguvu na hatimaye kushindwa kote. Ni kama kutaka yote kwa pupa na kukosa yote,” amesema Dk Swai.
Kwa upande wa CCM, amesema siri ya ushindi wake bila malalamiko ipo kwenye uamuzi wa kufanya mabadiliko yanayodaiwa, kisha kitumie uzoefu wake kushindana.
“CCM ina uzoefu wa kushindana kwenye uchaguzi, imekuwa ikishindana kwa zaidi ya karne sasa tangu kikiitwa Tanu. Kinaweza kufanya mabadiliko yanayohitajika na bado kikawa na nguvu ya kushindana,” amesema.
Hakuna ushindi labda wa kupewa
Kwa upande wa Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema hakuna siri ya ushindi wa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo, labda ule wa kupewa.
Ameisisitiza hoja yake hiyo akisema haoni dalili iwapo upinzani utashinda nafasi yoyote kutokana na changamoto ya mazingira ya kisheria yanayoikabili nchi.
“Wapinzani wanaoweza kushinda ni wale watakaoamua kushirikiana na Serikali iliyopo madarakani au kuomba wapewe nafasi kadhaa kwa makubaliano ili kuonyesha kuna mazingira huru ya kisiasa nchini,” amesema.
Hata hivyo, amesema ingawa vyama hivyo vitapewa viti mathalan vya ubunge, bado hautakuwa ushindi na uchaguzi hautakuwa huru na haki.
Amesisitiza ni hatari kwa chama cha siasa kuingia kwenye uchaguzi kikilenga kushinda ubunge au kupata ruzuku pekee.
“Kama watu wanafikiria kufanya uchaguzi ili vyama vyao vipate ruzuku hiyo ni kuwaibia wananchi kodi zao kwa sababu ruzuku zinatokana na kodi ya wananchi,” amesema.