Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saumu Rashid ateuliwa kupeperusha bendera ya UDP urais 2025

Mgombea urais wa kupitia UDP, Saumu Rashid (katikati) akiwa na mgombea mwenza wake, Faki Juma, na mgombea urais wa Zanzibar, Naima Mohamad (kushoto), baada ya kutangazwa rasmi katika Mkutano Mkuu wa chama hicho leo jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga


Muktasari:

  • Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Hussein Lutambi amesema Saumu amepita baada ya kupigiwa kura za ‘ndiyo’ na wajumbe 376 kati ya jumla ya kura 390 zilizopigwa.

Dar es Salaam. Chama cha United Democratic Party (UDP) kimechagua Saumu Rashid kuwa mgombea wake wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Pamoja naye, Naima Salum Mohamad amepitishwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Wote hao kwa pamoja wamepitishwa katika mkutano mkuu maalumu uliofanyika leo Agosti 11, 2025, jijini Dar es Salaam.

Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Hussein Lutambi amesema Saumu amepita baada ya kupigiwa kura za ‘ndiyo’ na wajumbe 376 kati ya jumla ya kura 390 zilizopigwa.

Mgombea urais kupitia Chama cha UDP, Saumu Rashid (kulia) akiwa na mgombea mwenza wake, Faki Juma, mara baada ya kutangazwa rasmi katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika leo jijini. Picha na Michael Matemanga



Baada ya kutangaza matokeo hayo, amesema mgombea urais huyo amemchagua Juma Khamis Faki kuwa mgombea mwenza wake. Faki ni Naibu Katibu Mkuu wa UDP upande wa Zanzibar.

Kwa upande wa Zanzibar, Naima ndiye aliyechaguliwa na wajumbe hao kugombea nafasi ya urais. Naima, ambaye katika uchaguzi huo alipigiwa kura za wazi, wajumbe wote walimpitisha kwa kura za ‘ndiyo’.


Walichosema wagombea

Saumu amesema amefarijika wanachama kuwa na imani naye kwamba ataweza kupeperusha bendera ya chama hicho.

“Ninaahidi kwamba tunaenda kunadi sera yetu kwa pamoja kwa wananchi, lengo likiwa kuwaletea maendeleo,” amesema Saumu.

Kwa upande wake, Naima amesema hiuo sio mara ya kwanza kugombea, kwani aliwahi kugombea ubunge mara mbili lakini haikuwa bahati kwake, na safari hii akaona aingie katika nafasi ya urais.


Cheyo ampa salamu Msajili

Awali, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, amewashukuru wajumbe kwa namna walivyoshiriki uchaguzi huo kwa amani.

“Mie naishiwa maneno kwa kazi nzuri mliyoifanya, wajumbe. Niahidi tu kwa wagombea, sisi tutakuwa nyuma, mbele na pembeni yao, maana tukisema tu nyuma mtasema nyinyi mnafanya nini huko nyuma,” amesema.

Kuhusu Msajili wa Vyama vya Siasa, Cheyo amemtaka kuondoa mashaka kwamba UDP haitashiriki katika uchaguzi huo na kumtaka apeleke habari kwa Watanzania wote kwamba watashiriki.

“Tunachotaka ni kitu kimoja, nyie mliopewa majukumu ya kuangalia usalama na utii wa sheria za nchi kama zilivyosema, basi mfanye kazi yenu.

“Wote tushirikiane, kwani miaka yote Tanzania watu wamekuja kujifunza uchaguzi, kwa hiyo, kwa mwaka huu sioni sababu watu kutokuja kujifunza,” amesema Cheyo na kuongeza:

“Sisemi kwamba mtutishe, bali tufanye uchaguzi kwa amani bila kuoneana, bila kutishana wala kuiba kura.”

Kiongozi huyo amesema kwa miaka 30 ameona vyama vya upinzani vimeisaidia nchi kuwa na heshima na mtazamo tofauti.

“Tulipoanza siasa mwaka 1994, mkulima alikuwa akikopwa mazao yao kila msimu, lakini sasa naona hata chama tawala kinazungumza juu ya mkulima kuwa kilimo ni biashara.

“Mfumo huo umetokana na UDP, kwamba ‘no cash, no korosho.’ Kwa hiyo, mtu anayeenda kwa mkulima kujaribu kukopa mazao yao, nadhani atapata upinzani mkubwa sana.

Mgombea urais wa Jamhuri kupitia UDP, Saumu Rashid, akiomba kura kwa wajumbe wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

“Hivyo, UDP tunajivunia kuleta mabadiliko haya. Hata nikisikia kwenye redio kilimo ni biashara nasema ‘yes,’ elimu imefika, na nina hakika kama kila mtu akifanya hivi nchi yetu itastawi na kilimo kitakuwa biashara,” amesema Cheyo na kuongeza;

“Kwa hiyo, wanaofikiri chama kama chetu hakina kazi ya kufanya wajifunze kuwa wana kazi. Hata hiyo ya kutoa somo ni kazi pia pale wanaposhauri ni vema watu wakaenda hivi.”

Hata hivyo, Cheyo amesema UDP wanaunga mkono harakati zote za amani kusaidia wanyonge, na ndio maana moja ya kaulimbiu yao inasema “mnyonge anyanyuke.”

Kutokana na hilo, ameitaka Serikali kuisaidia nchi hii kutawala na kubainisha kuwa njia ya kuweza kutawala ni kuishi kwa amani.

“Hatutaki kusikia huyu kafa, huyu kachukuliwa, unamchukua mtoto wa watu unampeleka wapi? Mahali pazuri ni Tanzania. Sasa wewe unamchukua mtoto wa watu unaenda kumtupa. Atakayetusaidia haya yasitokee ni Serikali, kwani usalama wetu tunauweka kwao.

“Sana sana sisi tutapiga kelele, jamani, naonewa, jamani natekwa, lakini mtu atakayeweza kutusaidia ni Serikali, hivyo naomba vyombo vyake viwe imara kuhakikisha Watanzania tunaishi kwa usalama kwa kuwa hatuna mahala pa kukimbilia zaidi ya Tanzania,” amesisitiza Cheyo.


Msajili awapongeza

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, akimwakilisha Msajili, Jaji Mitungi, amewapongeza UDP kwa kufanya mkutano huo akisema umeenda vizuri.

“Maandalizi mazuri, hata mimi nayaona, na sio kwa muonekano tu, lakini hata kwa utaratibu na utulivu, wajumbe wanaingia vizuri ndani.

“Kwa upande wa Mwenyekiti wa UDP, sina mashaka, kwa sababu kama alivyosema angeweza kulala nyumbani kutokana na afya yake, lakini katika hili hakutaka kulala.

“Kwa kweli mheshimiwa mwenyekiti tunakupongeza, unakipenda chama chako, na hata wanachama wanakipenda chama chao, ndio maana leo wapo hapa,” amesema Nyahoza.

Ameongeza kuwa: “Demokrasia ikifuata sheria inapatikana amani, na kuna taratibu zipo ikiwemo haki ya kugombea, na ni jukumu letu kuja kuangalia ni namna gani mnatekeleza sheria katika kumteua mgombea kwa mujibu wa Katiba.”


Vyama waliokuwapo

Akiwakilisha vyama vya siasa vilivyoalikwa katika mkutano huo, Costantine Kibonde kutoka Chama cha Demokrasia Makini, amewaomba wagombea waliopitishwa na chama hicho kuwa wana sababu ya kushirikiana nao kwenda kuendeleza sera za upendo, ambazo zinakwenda kuenezwa kwenye majukwaa na zaidi ziwe ni amani ya Tanzania.

“Wote leo tumekutanishwa hapa vyama tofauti na UDP kwa sababu ya amani iliyopo, hivyo nisisitize upendo huu twende tukausambaze hata tunapokuwa katika majukwaa ya kampeni,” amesema Kibonde ambaye pia ndio mgombea urais wa chama hicho.

Katika mkutano huo, jumla ya wajumbe kutoka mikoa 30 kati ya 31 walihudhuria, ambapo waliopaswa kuwepo ni wajumbe 400, lakini waliofanikiwa kufika ni 390, na hivyo kuwapa haki ya kuchagua wagombea.