Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia amtaka IGP Wambura asisubiri amani ivurugike

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi, lisisubiri amani ivurugike ndiyo lipambane, badala yake lianze kwa kudhibiti viashiria vya uvunjifu.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha linadhibiti viashiria vya uvunjifu wa amani, vinavyotokea kabla, wakati na hata baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Amelitaka jeshi hilo lisisubiri amani ivurugike ndiyo lipambane, badala yake lianze kwa kudhibiti viashiria vya uvunjifu.

Agizo linalofanana na hilo, alilitoa pia Januari 22, 2024 kwa Jeshi la Wananchi (JWTZ), alipolitaka lihakikishe linajipanga kikamilifu kwa kuwa uchaguzi unahusisha watu wengi na vyama vyenye nia tofauti, hivyo hana hakika kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa.

Akizungumza katika hafla hiyo,  Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura amesema hatavumiliwa yeyote atakayevuruga amani na utulivu katika kipindi cha kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi huo.

Rais Samia ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Juni 9, 2025 alipohutubia hafla ya kuhitimisha mafunzo kwa maofisa na wakaguzi wasaidizi wa polisi kwa mwaka 2024/25.

Hata hivyo, ameeleza kuridhishwa na namna jeshi hilo lilivyoeleza mpango wake wa kutovumilia vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

“Niwatake mjipange vilivyo, ili kuhakikisha mnaendelea kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, tusisubiri amani ivunjwe, viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani tuvidhibiti mapema,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan akijadiliana jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura katika sherehe za kuhitimisha mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa jeshi hilo, Kurasini, Dar es Salaam.

Kuhusu hoja hiyo, Wambura amesema jeshi hilo limejipanga vema kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu kabla, wakati na baada.

“Tunakuahidi, nchi hii ni salama, nchi hii ina amani, jeshi la polisi haliko tayari kumvumilia yeyote atakayeleta uvunjifu wa amani kwa namna yoyote ile.

“Sisi kama jeshi la polisi, tuna wivu mkubwa na amani ya nchi yetu na tutalinda amani, utulivu wa nchi hii kwa wivu mkubwa kipindi chote, kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu,” amesema.

Sambamba na kilichoelezwa na Wambura, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa naye amesema wahitimu wa kozi ya maofisa na wakaguzi wa jeshi hilo, wamejengewa uwezo kuhakikisha wanaimarisha amani wakati wa mchakato huo.

Amesema mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Bara na Zanzibar, hivyo vyuo vyote vilitoa muda kwa wahitimu kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura.

“Tumewajengea uwezo kuhakikisha uchaguzi husika utasimamiwa kwa kufuata sheria za nchi, ili amani na utulivu viendelee kutamalaki, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi,” amesema.


…ataka mkakati kukomesha ajali

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuja na mkakati wa kuhakikisha kile alichokiita mzimu wa ajali unaoiandama nchi unakoma.

Kauli ya Rais inatokana na kile alichofafanua kwamba, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kuimarisha usalama barabarani, bado mzimu wa ajali umeliandama Taifa.

Wakati Rais akiyasema hayo leo, ni siku tatu tangu itokee ajali iliyoondoa uhai wa wananchi 28 na kuwajeruhi wengine 12, baada ya lori kugonga gari lingine kwa nyuma, mkoani Mbeya.

Amejenga hoja yake hiyo, kwa kurejea takwimu za matukio ya ajali, akisema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu pekee, zimetokea 1,322 na kupoteza uhai wa watu 1,275.

Amesema idadi hiyo ya vifo kwa ajali za miezi minne ya mwaka huu pekee, ni ongezeko la asilimia tisa ukilinganisha na ajali za kipindi kama hicho, mwaka jana.

“Kila tunavyochukua hatua ndivyo ajali nazo zinaongezeka, sasa hebu tulitazameni vizuri eneo hili kuna nini hasa. Kama ni barabara zetu kama Taifa, tufunge mikaja, eneo lingine tutengeneze barabara zetu ili ajali zisitokee.

“Kama ni kufunga vifaa vya usalama barabarani tufanye hivyo, kama ni uzembe wa madereva wawekwe wafundishwe, muweke masharti magumu ya kumfanya mtu kuwa dereva,” amesema Rais Samia.

Amesema kunapaswa kuwepo vikwazo zaidi kwa kuwa eneo la ajali limeliandama Taifa na vifo vimeongezeka, hivyo watakaopangwa kwenye usalama barabarani wawe na mikakati mizuri.


Uadilifu

Akizungumzia suala la uadilifu, Rais Samia ametaka kila askari awe mfano kwa mwenzake, huku vitendo vya rushwa, uhalifu na utovu wa nidhamu viepukwe.

Amesema ni matumaini ya Watanzania askari hao wanakwenda kusimamia haki za raia, wanakomesha vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.

“Haya ndiyo maradhi makubwa na sitaki kusema yameisha, bado yapo yanaendelea, muda baada ya muda tunarushiwa viklipu na mimi nikirushiwa namrushia IGP watu wako hao barabara fulani angalia. Na namshukuru nikimrushia hachelewi anachukua hatua hapohapo,” amesema.

Hivyo, amewataka maofisa hao wakakomeshe rushwa, akikazia kwamba katika mafunzo yao  hawakufunzwa ili kupewa silaha zaidi za kuwakomesha watu kwenye maeneo hayo, badala yake wanapaswa kuwa jawabu la malalamiko.

Ameusifu wimbo wa maadili wa jeshi hilo, akisema iwapo askari wataendana nao, jeshi hilo litakuwa bora kuliko lolote la ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tukisema ukweli, tunaanza kuona mabadiliko makubwa ndani ya Jeshi la Polisi. Hata ukiangalia nidhamu ya polisi wetu, utendaji na manung’uniko yamepungua sana,” amesema.

Amesisitiza mafunzo kazini yatolewe kuendana na mazingira ya sasa kwa kuwa hata wahalifu wanatumia mbinu za kisasa, huku akiitaka menejimenti itekeleze mapendekezo ya tume ya haki jinai.

Ameahidi kushughulikia changamoto za jeshi hilo kwa kuongeza vitendea kazi na masilahi kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu.


IGP Wambura

Katika hotuba yake, IGP Wambura amerejea matukio mbalimbali ya ujambazi, wizi na unyang’anyi yaliyokuwepo zamani, akisema tangu Rais Samia aingie madarakani, yamepungua.

Amesema kuongezewa masilahi na kupandishwa vyeo kwa askari, kumewaongezea ari na molari ya utendaji wa jeshi hilo, huku ajira mpya zikiziba ombwe la askari katika kamandi mbalimbali.

Amehusisha kupungua kwa matukio na kuimarishwa kwa jeshi hilo kwa maana ya vitendea kazi na mafunzo ndani na nje ya nchi.

“Nchi kama Misri, Urusi, China, Marekani, Uturuki, India tunapeleka askari kwa mara moja peke yake tunapeleka zaidi ya 30,” amesema.

Kuhusu mafunzo hayo, Mambosasa amesema wahitimu wamefundishwa masomo 13 na wamefanyiwa tathmini kuona iwapo wamekidhi vigezo vya ufaulu kwa mitihani ya darasani na mafunzo ya nje kwa vitendo na ufuatiliaji wa tabia.

Amesema askari saba walishindwa kufikia viwango vya chuo kwa kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu na waliondoshwa chuoni.

Amesema wanafunzi wawili kati yao mwanaume mmoja na mwanamke mmoja waliondoshwa kwa utovu wa nidhamu huku wakaguzi wasaidizi waliokidhi vigezo na kustahili kupandishwa vyeo wakiwa 174 na  maofisa wakiwa 780.