Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

IGP Wambura atoa msimamo wa Polisi kuelekea chaguzi mkuu

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limesema litahakikisha kabla, wakati na baada ya uchaguzi kunakuwa na amani na usalama wa kutosha

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura amesema jeshi hilo halitamvumilia yeyote atakayevuruga amani na utulivu katika kipindi cha kabla, wakati na hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Wakati Wambura akisema hivyo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema maofisa na wakaguzi wote wa jeshi hilo wamejengewa uwezo kuimarisha amani na usalama katika mchakato wote wa uchaguzi.

Kauli hizo za viongozi hao wa Jeshi la Polisi, zinakuja ikiwa imebaki miezi michache kabla ya Tanzania kuingia katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Wambura ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Juni 9, 2025 alipohutubia katika sherehe za kuhitimisha mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa jeshi hilo, Kurasini, Dar es Salaam.

Katika maandalizi ya uchaguzi huo, amesema jeshi hilo limejipanga vema kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu kabla, wakati na baada.

“Tunakuahidi, nchi hii ni salama, nchi hii ina amani, jeshi la polisi haliko tayari kumvumilia yeyote atakayeleta uvunjifu wa amani kwa namna yoyote ile.

“Sisi kama Jeshi la Polisi tuna wivu mkubwa na amani ya nchi yetu na tutalinda amani, utulivu wa nchi hii kwa wivu mkubwa kipindi chote, kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu,” amesema.

Sambamba na kilichoelezwa na Wambura, Mambosasa naye amesema wahitimu wa kozi ya maofisa na wakaguzi wa jeshi hilo  wamejengewa uwezo kuhakikisha wanaimarisha amani na usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Amesema mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Bara na Zanzibar, hivyo vyuo vyote vilitoa muda kwa wahitimu kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura.

“Tumewajengea uwezo kuhakikisha uchaguzi husika utasimamiwa kwa kufuata sheria za nchi, ili amani na utulivu viendelee kutamalaki, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi,” amesema.

Sambamba na kujengewa uwezo kuhusu uchaguzi, amesema wahitimu wamefundishwa masomo 13 na wamefanyiwa tathmini kuona iwapo wamekidhi vigezo vya ufaulu kwa mitihani ya darasani, na mafunzo ya nje kwa vitendo na ufuatiliaji wa tabia.

Amesema askari saba walishindwa kufikia viwango vya chuo kwa kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu na waliondoshwa vyuoni.

Kwa upande wa wakaguzi wasaidizi, amesema wanafunzi wawili kati yao mwanaume mmoja na mwanamke mmoja waliondoshwa kwa utovu wa nidhamu.

Amesema wakaguzi wasaidizi  174 wamekidhi vigezo na wanastahili kupandishwa vyeo huku maofisa 780 wote wamekidhi viwango na wanastahili kupandishwa vyeo.