Rais Samia ataka mkakati kukomesha ajali

Rais Samia Suluhu Hassan akijadiliana jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura katika sherehe za kuhitimisha mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa jeshi hilo, Kurasini, Dar es Salaam.
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ametaka utafutwe mkakati wa kukomesha matukio ya ajali, yanayoendelea kutokea nchini.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi kuja na mkakati wa kuhakikisha kile alichokiita mzimu wa ajali unaoiandama nchi unakoma.
Kauli yake hiyo, inatokana na kile alichofafanua, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kuimarisha usalama barabarani, bado mzimu wa ajali umeliandama Taifa.
Mkuu huyo wa nchi anaeleza hilo, siku mbili tangu itokee ajali iliyoondoa uhai wa wananchi 28 na kuwajeruhi wengine 12, baada ya lori kugonga gari lingine kwa nyuma, mkoani Mbeya.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumatatu Juni 9, 2025 alipohutubia hafla ya kufunga mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa Jeshi la Polisi, jijini Dar es Salaam.
Amejenga hoja yake hiyo, kwa kurejea takwimu za matukio ya ajali, akisema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Aprili 2025 pekee, yametokea 1,322 na kupoteza uhai wa watu 1,275.
Amesema idadi hiyo ya vifo kwa ajali za miezi minne ya mwaka huu pekee, ni ongezeko la asilimia tisa ukilinganisha na ajali za kipindi kama hicho, mwaka jana.
“Kila tunavyochukua hatua ndivyo ajali nazo zinaongezeka, sasa hebu tulitazameni vizuri eneo hili kuna nini hasa. Kama ni barabara zetu kama Taifa, tufunge mikaja eneo lingine tutengeneze barabara zetu ili ajali zisitokee.
“Kama ni kufunga vifaa vya usalama barabarani tufanye hivyo, kama ni uzembe wa madereva wawekwe wafundishwe, muweke masharti magumu ya kumfanya mtu kuwa dereva,” amesema.
Amesema kunapaswa kuwepo vikwazo zaidi kwa kuwa eneo la ajali limeliandama Taifa na vifo vimeongezeka, hivyo watakaopangwa kwenye usalama barabarani wawe na mikakati mizuri.