Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifo watu 28 Rais Samia atuma salamu za rambirambi aziagiza Tanroads, Tarura

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka madereva kuongeza umakini barabarani na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameungana na Watanzania wengine kutuma salamu za rambirambi kutokana na ajali ya gari iliyosababisha vifo vya watu 28 na kuwajeruhi wengine wanane.

Sambamba na salamu zake za rambirambi, mkuu huyo wa nchi pia ameziagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), kuboresha hali ya barabara hasa maeneo yenye changamoto kubwa zaidi, kwa usalama wa watumiaji wote.

Ajali hiyo, ilitokea usiku wa jana Jumamosi Juni 7, 2025 katika Mlima Iwambi, kwenye barabara kuu ya Tanzania - Zambia, mkoani Mbeya.

Katika taarifa yake hiyo aliyoichapisha kupitia kurasa za mitandao yake ya kijamii, Rais Samia amewaombea marehemu wote wapumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka.

“Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, familia zote za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyenzi Mungu awajalie subra na uvumilivu,” ameandika.

Ametumia salamu zake hizo za rambirambi, kuwasisitiza madereva kuendelea kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lililokuwa limebeba shehena ya unga kutoka Dar es Salaam kuelekea Zambia, lililogonga kwa nyuma magari mawili aina ya Mitsubishi Rosa na Toyota Lite Ace na hatimaye kuanguka katika bonde la Mto Mbalizi.

Chanzo cha ajali kinasadikiwa kuwa uzembe wa dereva wa lori kushindwa kulimudu kwenye mteremko.

Katika ajali hiyo, watu 28 wamepoteza maisha, kati yao 12 ni wanawake na wanaume 16. Hadi sasa, miili 19 imetambuliwa na tisa haijatambuliwa. Aidha watu wanane, wakiwamo wanaume sita na wanawake wawili wamejeruhiwa.