Prime
Masheikh, wanasiasa wataka uchaguzi huru, haki

Muktasari:
- Wananchi wahimizwa kushiriki uchaguzi na kujiepusha na uvunjivu wa amani.
Dar/mikoani. Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini wamehimiza umuhimu wa kudumisha amani kama msingi wa haki, maendeleo na utekelezaji wa ibada, wakitoa wito kwa Watanzania kuepuka kauli za chuki au uchochezi kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Aidha, wamewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kugombea nafasi za urais, ubunge na udiwani, pamoja na kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura.
Wito huo umetolewa katika maadhimisho ya sikukuu ya Eid El- Adh' haa, yaliyofanyika leo Jumamosi, Juni 7, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutenda haki kwa kila hatua ya uchaguzi huo, ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru na wa haki kwa vyama vyote.

Bakwata ikisema hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amejibu wito huo akisema Serikali itasimamia sheria na kanuni zilizowekwa ili Tanzania iendelee kuwa na utulivu na uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
"Serikali kama wadau, tutaichukua kauli ya INEC na jukumu letu ni kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na utafanyika katika amani ya hali ya juu kabisa," amesema Majaliwa akihutubia Baraza la Eid El- Adh' haa.
Wito wa Bakwata umetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Sheikh Nuhu Mruma wakati akihutubia Baraza la Eid El- Adh' haa lililofanyika katika msikiti wa Mohammed VI uliopo makao ya makuu ya baraza hilo, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
"Msingi mkubwa wa amani upo katika utoaji wa haki, tunaendelea kuviasa vyama vya siasa na wagombea kufanya siasa za kistaharabu na kuepuka lugha zisizo za ustaharabu," amesema Sheikh Mruma.
Bakwata pia imetoa wito kwa Watanzania kuilinda na kuitunza amani ya nchi, likisema bila amani hakutakuwa na maendeleo wala haitakuwepo fursa ya kufanya ibada.
"Sote tunafahamu mwishoni mwa mwaka huu Taifa letu linaingia katika mchakato wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, sisi viongozi wa dini tunaendelea kuomba dua ili mchakato huo uende kwa amani.
"Tunawaomba Waislamu na wananchi wote kutumia fursa hii ya kikatiba ya kuchagua viongozi au kuwa wagombea katika nafasi mbalimbali ili kupata haki ya kuchaguliwa," amesema.
Sheikh Mruma amesema Bakwata ina matumaini kuwa mamlaka husika imeshafanya maandalizi ili haki hiyo ipatikane kwa kila mtu.
"Tunafahamu hatua inayofuata ni watia nia kuchuku fomu ndani ya vyama vyao kuomba kuteuliwa, kisha kuchukua fomu za INEC. Tunaviasa vyama vya siasa, kuteua wagombea bora na wenye sifa na kuepukana wagombea wenye uchu wa madaraka wanaotaka uongozi kwa hila na kutumia rushwa," amesema.
Msingi ni maadili
Sheikh Mruma amesema Bakwata inaendelea kusisitiza maadili ambayo ndiyo msingi muhimu ili kuwa na jamii yenye kuheshimu na kuthamini watu.

Amesema hivi karibuni imeshuhudiwa vitendo vinavyokwenda kinyume cha maadili ya Kitanzania.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitoa kauli mbaya na kuwakashifu wananchi wengine katika mitandao ya kijamii, wakiwamo viongozi, jambo alilosema si jema na haliwezi kuvumilika kwa sababu lina madhara makubwa na uvunjifu wa amani.
"Viongozi wa dini tunalaani vitendo hivyo na kuvikemea vikali kwa sababu si maadili yetu. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaofanya vitendo hivi visivyo vya kiungwana na vile vya kuwavamia na kuwaumiza watu pasipo sababu za msingi," amesema.
Afya ya akili
Kwa upande wake, Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko amesema dunia na Tanzania, jamii inakabiliwa na tishio la hali mbaya ya afya ya akili.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Tanzania, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 wananchi waliohudhuriwa vituo vya kutolea huduma za afya kwa shida ya magonjwa ya afya ya akili walikuwa 293,952 ikilinganishwa na 246,544 kwa kipindi cha mwaka 2022/23.
“ Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), jambo hili tunaweza kuliona dogo lakini kila mmoja kuanzia sasa anatakiwa kulitafakari. Akili za binadamu kwa sasa zimefunikwa na tunapoelekea kwenye uchaguzi, tuwachagua ambao afya za akili zipo kiwango cha chini.
"La sivyo tutawakabidhi uongozi watu ambao afya zao akili zipo chini, itakuwa hatari zaidi wakati huo. Chujio la kupima afya duni ya akili ya mtu ni namna anavyowasilisha sera pale anapowaomba wananchi kumpa kura," amesema.
Amesema wagombea wanaowasilisha sera zao kwa kutumia matusi, kejeli, dharau na ubaguzi, hawafai kuchaguliwa kupewa uongozi.
"Hili ni angalizo nalitoa kwenu, tuna tatizo kubwa la afya ya akili, nenda kwenye mitandao ndio mtanielewa. Mtandao ndiyo unatuonyesha hali ni mbaya kiasi gani duniani," amesema.
Akizungumza baada ya swala, katika Msikiti wa Muuminina, Mailimoja, mkoani Pwani Kadhi wa mkoa huo, Sheikh Zuberi Rashidi amewasihi waumini waendelee kuwa mabalozi wa amani katika jamii hasa wakati huu Taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu.
“Uislamu ni dini ya amani tunapaswa kuonyesha mfano katika kuheshimiana, kushiriki uchaguzi kwa amani na kuwachagua viongozi tunaowaona wanafaa kwa masilahi ya Taifa,” amesema.
Amesema kipindi cha uchaguzi huwa nyeti, hivyo ni wajibu wa kila raia kuhakikisha hatumii jukwaa hilo kuchochea vurugu au chuki, bali kulinda umoja wa kitaifa.
Sheikh Yahya Kivuma akizungumza baada ya swala ya Eid El -Adh'haa katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma amesema katika kipindi hiki kutakuwa na maneno mengi ambayo yanaendelea kwa kisingizio ni mwaka wa uchaguzi ili kuvuruga amani ya nchi.
“Nawaomba Watanzania tuiombee nchi yetu amani katika kipindi hiki maana amani ikipotea hatuna nchi nyingine ya kukimbilia, tuna nchi moja tu ya Tanzania. Kwa hiyo, tuilinde amani tuliyonayo maana ikipotea ni gharama kuirudisha,” amesema.
Sheikh Kivuma amewataka Watanzania kuwaombea viongozi walioko madarakani ili wawe na busara ya kuiongoza nchi.
Sheikh Swedi Twaibu aliyemwakilisha Mufti katika swala hiyo, amewataka Watanzania kuwa na subira na kuvumiliana kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi, hivyo watu wengi watatumia nafasi hiyo kuvuruga amani.
Amesema mwaka huu kuna watu watavuana nguo kwa kutoleana siri zilizofanyika miaka ya nyuma kwa sababu tu ya uchaguzi, hivyo amewaomba Watanzania kuwa wavumilivu.
Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Ayas Njalambaha amesema katika kipindi cha uchaguzi mkuu, wananchi wajitokeze kwa wingi kumchagua kiongozi bora atakayewaletea maendeleo.
Ameitaka jamii kuweka misingi imara katika kulea na kutunza watoto, akibainisha kuwa bila kufanya hivyo, litaibuka Taifa lisilo na maadili na kuharibu taswira ya nchi.
Akizungumza baada ya swala katika viwanja vya Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, Sheikh wa mkoa huo, Alhaji Ibrahim Mavumbi pia amesisitiza kutuzwa amani nchini.
Amewahimiza kuhakikisha wanashiriki uchaguzi mkuu akisema uchaguzi ni lazima na vitabu vya dini vinaelekeza kuchagua viongozi.
"Usiposhiriki uchaguzi utakuwa umetenda dhambi kwa kuwa ni sheria kwa mujibu wa dini yetu, hivyo twendeni tukashiriki uchaguzi kwa amani," amesema.
Umuhimu wa kudumisha amani pia umesisitizwa na Imamu wa Masjid Noor, Yakubu Saburi, aliyesema:
"Nawaomba ilindeni amani iliyopo tuvuke salama kwenye mchakato wa uchaguzi na kupata viongozi bila vurugu. Naomba vijana wa Kitanzania wasitumike kuvuruga amani iliyopo.
Tusikubali kutumika kuharibu amani yetu, mara nyingi tunaongea amani wengi wanahisi tuko upande fulani, jamani hali ikivurugika hakuna atakayeona hilo."
Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaabani Mlewa, katika swala iliyofanyika kimkoa katika Msikiti wa Shafii, Bomang'ombe wilayani Hai, amesisitiza kudumishwa kwa amani, upendo na utulivu kwani ndiyo msingi muhimu wa maendeleo.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Issa Kwezi, amezungumzia umuhimu wa kulinda maadili akijenga hoja kuwa, ilivyo sasa nchini, hata watu wazima hawana maadili, yote hayo yakitokea kwa kisingizio cha ukuaji wa demokrasia.
"Ndugu zangu, maadili ni kwa wote kuanzia watoto hadi watu wazima, kuheshimiana. Hata kiongozi lazima achunge cheo chake kwa kuwajali wenzake na kulinda heshima zao. Tutumie lugha nzuri katika kuwahusia watu na kukosoa; tumia njia ya kistaarabu," amesema.

Amesema kutokutumia mfumo mzuri katika kufikisha ujumbe kunasababisha mgongano kwa yule unayemfanyia kuhisi unamkosea heshima.
Waumini pia wametakiwa kuelekeza nguvu zao katika kuwasaidia yatima, maskini na watu wasiojiweza ili na wao waweze kuwa na furaha kama watu wengine.
Wito huo umetolewa na Sheikh Said Ali Bakari katika Msikiti wa Ijumaa, Machomane, mjini Chake Chake.
Imeandikwa na Peter Elias na Bakari Kiango (Dar), Sanjito Msafiri (Kibaha), Rachel Chibwete (Dodoma), Saddam Sadick (Mbeya), Hawa Kimwaga (Tabora), Tuzo Mapunda (Bariadi), Bahati Chume (Hai) na Salim Hamad (Pemba)