Shura ya Maimamu yaja na mapendekezo kuboresha maisha ya Watanzania

Muktasari:
- Imependekeza Serikali ianzishe sera na mfumo ambao raia atalipa asilimia asilimia 20 ya gharama ya matibabu na Serikali italipa asilimia 80 zilizobaki ili kuwapunguzia mzigo wananchi, hasa wenye vipato vidogo.
Dar es Salaam. Shura ya Maimamu Tanzania imeishauri Serikali kuwekeza vya kutosha katika kuzalisha walimu wengi na bora, iwaajiri wahitimu wote wa kozi hiyo na iwalipe mishahara bora.
Pia, imependekeza Serikali ianzishe sera na mfumo ambao raia atalipa asilimia asilimia 20 ya gharama ya matibabu na Serikali italipa asilimia 80 zilizobaki ili kuwapunguzia mzigo wananchi hasa wenye vipato vidogo.
Hayo yamebainishwa leo Juni 7, 2025 na Katibu wa Shura ya maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda wakati akiwasilisha waraka wa shura kwenye Baraza la Iddi Adh-ha, kuhusu hali ya maisha ya Watanzania katika nyanja mbalimbali.
Sheikh Ponda amesema Shura inapendekeza kwamba Taifa lazima liwekeze nguvu kubwa katika elimu. Amesema Tanzania inaandaa walimu wachache ukilinganisha na mahitaji, kwani mwaka 2024/25, Serikali ilipanga kuajiri walimu 12,000 wakati mahitaji ni makubwa.
Amesema walimu kwa madarasa ya awali na msingi peke yake ni 116,885. Amesisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa walimu na kuwaajiri wote.
“Mtaala uzingatie ujuzi, maarifa, uzalendo na kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujitegemea,” amesema.
Pia, amesema ufanyike utafiti na tathmini za mara kwa mara kupima ubora wa wanafunzi na elimu. Amesema wanapendekeza Serikali ihakikishe shule ina vifaa muhimu na vya kutosha kama vile vitabu, maabara, maji safi, chakula, vyoo na umeme.
Kuhusu sekta ya afya, Sheikh Ponda amesema raia wengi wanatamani Serikali ingerejesha mfumo wa awali wa kutouziwa huduma na dawa katika hospitali za Serikali.

“Katika fikra za kutafuta njia ya kati na kati tunapendekeza Serikali ianzishe sera na mfumo ambao raia atalipa asilimia 20 ya gharama ya matibabu na Serikali italipa asilimia 80 iliyobaki,” amesema.
Pia, amesema wanapendekeza Serikali iondoshe uwakala au zabuni katika ununuzi wa vifaa na dawa, badala yake inunue moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji. Amesema hatua hiyo itaondosha ufisadi katika ununuzi.
Kuhusu uchaguzi ujao, Sheikh Ponda amesema sheria za uchaguzi muhimu katika kujenga mfumo wa demokrasia na utoaji haki. Hata hivyo, amesema sheria hizo zinalalamikiwa na jamii na taasisi mbalimbali.
“Wito wetu, tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na wadau wanaowakilisha wananchi kujadili malalamiko yaliyopo kabla ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu,” amesema Sheikh Ponda ambaye hivi karibuni alijiunga na Chama cha ACT- Wazalendo.
Shura ya Maimamu Tanzania imeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) isimamie mchakato kwa haki, watu wasinyimwe haki ya kuchagua na kuchaguliwa kwa makosa madogo madogo.