Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheikh Ponda atajwa kuwania ubunge Dar

Muktasari:

  • Sheikh Ponda ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa na msimamo wa kusimamia haki za binadamu, amepokewa ACT-Wazalendo na kukabidhiwa kadi

Dar es Salaam. Uamuzi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo, unatajwa kuwa huenda kiongozi huyo akawania ubunge katika jimbo mojawapo kati ya manne yanayotajwa jijini Dar es Salaam.

Taarifa za ndani ambazo Mwananchi imezipata hivi sasa, timu ya ushauri ya kada huyo mpya wa ACT- Wazalendo ipo katika mashauriano na utafiti wa kina ili kubaini wapi kiongozi wao atagombea ubunge kwa mara kwanza kati ya majimbo matatu.

Majimbo hayo ni Kinondoni, Temeke, Mbagala na jimbo jipya la Chamazi.

Kinondoni, Temeke na Mbagala majimbo yenye historia ya kunyakuliwa na upinzani kwa nyakati tofauti, kuanzia mwaka 2000 aliyekuwa kada ya Chama cha Wananchi (CUF), Frank Magoba alichaguliwa kuwa mbunge wa Kigamboni.

Vivyo hivyo katika uchaguzi mkuu wa 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wagombea Abdul Mtulia (Kinondoni) na Abdallah Mtolea (Temeke) walishinda ubunge wa majimbo hayo kwa mara ya kwanza baada ya kuwabwaga kina Idd Azzan na Abbas Mtemvu.

Ingawa hadi sasa Sheikh Ponda ambaye leo Alamisi, Juni 5, 2025 amekabidhiwa kadi na Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu bado hajatamka wazi kama atawania ubunge au la lakini kwa maelezo aliyotatoa katika hotuba ya shukrani baada ya kujiunga na chama hicho yanaashiria atakwenda kugombea.

Mmoja wa viongozi waandamizi wa ACT- Wazalendo aliyeomba hifadhi ya jina lake alipoulizwa hilo amesema: “Kaka, huyu ni mwamba, atagombea Kinondoni. Sasa tusubiri muda ufike utamwona anachukua fomu.”

Katika hotuba yake, mbele ya viongozi na wanachama wa wa ACT- Wazalendo, Sheikh Ponda amesema kujiunga na chama cha siasa atapata wigo mpana wa kuendeleza harakati na jitihada za kudai haki za binadamu ili kuhakikisha nchi inakuwa katika utawala bora.

"Kuchukua kadi leo ya chama cha siasa kunanipa fursa ya kuungana watu mbalimbali wakiwamo kina Madeleka (Peter) na wengine ili kuunganisha nguvu ya kuleta mabadiliko katika siasa katika nchi hii," amesema.

"Leo kujiunga na ACT-Wazalendo kunaniongezea uwezo na wigo, mimi ni kiongozi wa dini ni watu wengi, ingawa mwanzoni eneo hili ( siasa)  nilikwama kufanya kazi  kutokana na taratibu, lakini sasa nina uhakika wa kufanya kazi zaidi kupitia siasa," amesema Sheikh Ponda.

Mwananchi imemtafuta Sheikh Ponda ambaye amesema alichokifanya ni kujiunga kwenye chama ili kushiriki siasa rasmi kama hatua ya awali, lakini wananchi wakimuhitaji kuwania nafasi yoyote atafikiria.

"Mtazama wangu wananchi wenyewe wanihitaji kwanza, si kwenye ubunge pekee hata nafasi yoyote basi tutakaa na kujadiliana kisha kutoa uamuzi.

"Nimejitokeza hadharani ili wananchi wanione kwanza, najua wananchi wataniunga mkono si kwa sababu ya chama bali kazi zangu ninazozitekeleza kila siku za kupambania haki," amesema Sheikh Ponda.


Sababu ya kujiunga na siasa

Baada ya maisha ya harakati na uongozi wa kiroho na kuingia rasmi kwenye siasa kwa kukabidhiwa kadi, Sheikh Ponda amejiumga na siasa akisema analenga kulitumia jukwaa hilo kurejesha haki, uwazi na usawa katika michakato ya uchaguzi.

Sheikh Ponda ambaye awali, alionekana katika majukwaa ya kisiasa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kama sehemu ya viongozi wa dini waalikwa bila kuwahi kuweka wazi uanachama wake, kwa sasa amejirasimisha ndani ya ACT- Wazalendo.

Uamuzi wake wa kujiunga na chama hicho, umechochewa na kile alichoeleza, kuwepo kwa viongozi wa dini katika siasa kutachochea kulindwa kwa utu, Taifa na kuzuia ufisadi.

Sheikh Ponda ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akiingia kwenye mvutano na Serikali kutokana na msimamo wake wa kusimamia haki za binadamu, amepokewa na kukabidhiwa kadi na Semu.

Sheih Ponda amesema amejitosa kwenye chama hicho ili kuongeza nguvu ajenda ya 'linda demokrasia ' inayolenga kurejesha haki, uwazi na usawa katika michakato ya uchaguzi nchini.

Kiongozi huyo amesema anaamini amani ya kweli haiwezi kustawi pale ambako kura zinaibwa, sauti za wananchi zinakandamizwa na sheria zinatumika kuwanyamazisha wale wanaosema ukweli.

"Taifa letu linastahili kuongozwa kwa misingi ya sheria kila mtu bila kujali cheo chake, dini yake au kabila lake, yuko chini ya sheria," amesema.

"Sheria inapaswa kuwa kinga ya haki za binadamu, si chombo cha kuwatesa wananchi, tumeshuhudia jinsi sheria kama ile ya kupambana na ugaidi ikitumika vibaya kuwalenga wale wanaopinga dhuluma," amesema Sheikh Ponda.

Kutokana na hilo, Sheikh Ponda ametoa wito kwa vijana, wanawake, wazee na viongozi wa dini, kuungana katika uwanja wa mapambano ya kudai haki mbalimbali zikiwamo za kisiasa zitakazohakikisha kura zinahesabiwa kwa haki na viongozi wanaochaguliwa wanawakilisha matakwa ya wananchi.

"Tumeshuhudia wananchi wakipigwa na vyombo vya dola kwa sababu ya kulinda kura zao zisiibwe. Pia, tumeshuhudia wananchi wakipigwa na vyombo vya dola kwa madai ya kwenda mahakamani kusikiliza mashauri ya viongozi wao," amesema Ponda.

Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, moja ya malengo yake makubwa ya kuchukua kadi ya chama cha siasa ni kujiimarisha kisheria ili kupata jukwaa la kuwaelimisha wananchi wajue ajenda kuu ya Taifa lao (Katiba mpya) na kuwahamasisha wapiganie mambo ya msingi.

"Mapambano ya kudai haki si ya mtu mmoja wala chama kimoja bali yanahitaji umoja wa wapigania haki wote. Wale walioko katika vyama vya siasa, viongozi wa dini na kila Mtanzania anayejali mustakabali wa Taifa letu," amesema Sheikh Ponda.


Walichokisema ACT-Wazalendo

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema Sheikh Ponda ni mwamba wa harakati za kudai haki za binadamu na utawala bora wa sheria na wana furaha kumpokea ndani ya chama hicho.

"Nina furaha kumpokea ili aja kuendeleza harakati za kudai haki. Tunashukuru kuja kujiunga na chama chetu, tumesikia historia yako karibu sana," amesema.

"Kuja kwako ACT-Wazalendo kutasaidia kuongeza nguvu ya kupigania haki na demokrasia, nichukue fursa kuwakaribisha wale wote wanaopenda demokrasia. Wajibu wetu ACT ni kutoa jukwaa ili kuing' oa CCM tukiendelea hivi tutashinda Zanzibar na Tanzania bara," amesema Semu.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema kitendo cha Ponda kujiunga na ACT-Wazalendo, ni historia na tukio kubwa litakaloacha alama kubwa kwa chama hicho kumpokea kiongozi huyo ambaye ni mzalendo na mwadilifu.

"Leo ni siku ya Ponda ambaye si mgeni kwenye harakati hizi, amepitia ziko zama alikuwa CUF, zipo nyakati alipanda majukwaa ya Chadema, lakini leo ACT imepata heshima kubwa kwa uamuzi wa Sheikh Ponda kujiunga na chama hiki," amesema Ado.

Kada mpya wa ACT-Wazalendo, Wakili Peter Madeleka amesema Ponda ni mtu muhimu kwenye harakati za upambanaji wa kudai haki na utawala wa sheria.

"Kudai haki ni gharama, lakini Sheikh Ponda ameshailipa, gerezani ni kama sebuleni kwake… ametimiza wajibu wa kutetea haki za binadamu pasipp kubagua," amesema Madeleka.