Prime
Mambo mawili yanayomsubiri Sheikh Ponda ACT- Wazalendo

Muktasari:
- Uamuzi wa Sheikh Ponda kujiunga na chama cha ACT -Wazalendo pamoja na mambo mengine umechochewa na kile alichoeleza, kuwa kuwepo viongozi wa dini katika siasa kutachochea kulindwa kwa utu, Taifa na kuzuia ufisadi.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema uamuzi wa Sheikh Issa Ponda kujiunga na chama hicho unakwenda kuongeza chachu ya kisiasa na utasaidia kupigania haki na demokrasia nchini.
Amesema Sheikh Issa Ponda ni mwamba wa harakati za kudai haki za binadamu na utawala bora wa sheria, na hivyo wanafuraha kumpokea ndani ya chama hicho.
“Ninayo furaha kumpokea ili aje kuendeleza harakati za kudai haki. Tunashukuru kuja kujiunga na chama chetu, tumesikia historia yako, karibu sana. Nichukue fursa kuwakaribisha wale wote wapenda demokrasia waje kujiunga na chama chetu, milango iko wazi. Wajibu wetu ACT ni kutoa jukwaa ili kuing’oa CCM. Tukiendelea hivi, tutashinda Zanzibar na Tanzania Bara,” amesema Semu.
Semu ameyasema hayo leo Alhamisi, Juni 5, 2025, alipokuwa akimkabidhi Sheikh Ponda kadi ya uanachama wa ACT-Wazalendo baada ya kujiunga na chama hicho.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaib amesema Sheikh Ponda ameshasajiliwa kidijitali na amechagua kadi yenye hati ya Maalim Seif Shariff Hamad (Mwenyekiti wa zamani wa ACT-Wazalendo – marehemu).
Baada ya maisha ya harakati na uongozi wa kiroho, Sheikh Ponda, ambaye ni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, ameingia rasmi katika siasa za vyama.
Akizungumza baada ya kupokewa, Sheikh Ponda amesema lengo lake ni kuona haki, uwazi na usawa vinarejea katika michakato ya uchaguzi Tanzania.
Sheikh huyo, ambaye awali alionekana katika majukwaa ya kisiasa ya Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwa sehemu ya viongozi wa dini waalikwa, hakuwahi kuweka wazi uanachama wake, lakini sasa amejirasimisha ndani ya ACT-Wazalendo.
Amesema kama viongozi wa dini watasimamia vyema siasa za nchi hii kama alivyofanya, watachochea kulindwa kwa utu, Taifa na kuzuia ufisadi.
Sheikh Ponda, ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akiingia kwenye mvutano na Serikali kutokana na msimamo wake, amepokewa leo katika ofisi za Makao Makuu ya ACT-Wazalendo na viongozi waandamizi wa chama hicho.
Akizungumza baada ya kupokelewa na kukabidhiwa kadi, Sheikh Ponda amesema amejiunga na ACT-Wazalendo kwa lengo la kuongeza nguvu katika ajenda ya chama hicho ya Linda Demokrasia inayolenga kurejesha haki, uwazi na usawa katika michakato ya uchaguzi nchini.
Kiongozi huyo amesema anaamini amani ya kweli haiwezi kustawi kama kura zinaibiwa, sauti za wananchi zinakandamizwa, na sheria zinatumika kuwanyamazisha wale wanaosema ukweli.
“Taifa letu linastahili kuongozwa kwa misingi ya sheria, ambapo kila mtu bila kujali cheo chake, dini yake, au kabila lake yuko chini ya sheria. Sheria inapaswa kuwa kinga ya haki za binadamu, si chombo cha kuwatesa wananchi. Tumeshuhudia jinsi sheria kama ile ya kupambana na ugaidi ikitumika vibaya kuwalenga wale wanaopinga dhuluma,” amesema Sheikh Ponda.
Kutokana na hilo, Sheikh Ponda ametoa wito kwa vijana, wanawake, wazee, na viongozi wa dini kuungana katika uwanja wa mapambano ya kudai haki mbalimbali zikiwemo za kisiasa zitakazohakikisha kura zinahesabiwa kwa haki na viongozi wanaochaguliwa wanawakilisha matakwa ya wananchi.
“Tumeshuhudia wananchi wakipigwa na vyombo vya dola kwa sababu ya kulinda kura zao zisiibwe. Pia tumeshuhudia wananchi wakipigwa na vyombo vya dola kwa madai ya kwenda mahakamani kusikiliza mashauri ya viongozi wao,” amesema Ponda.
Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, moja ya malengo yake makubwa ya kuchukua kadi ya chama cha siasa ni kujiimarisha kisheria ili kupata jukwaa la kuwaelimisha wananchi wajue ajenda kuu ya Taifa lao (katiba mpya) na kuwahamasisha wapiganie mambo ya msingi.
“Mapambano ya kudai haki si ya mtu mmoja wala chama kimoja, bali yanahitaji umoja wa wapigania haki wote. Wale walioko katika vyama vya siasa, viongozi wa dini, na kila Mtanzania anayejali mustakabali wa taifa letu,” amesema Sheikh Ponda.