Hamahama yaendelee, wengine Chadema watimkia ACT-Wazalendo

Muktasari:
- Wanasiasa wawili waliokuwa sehemu ya wanamuungano wa G55 wamehamia chama cha ACT Wazalendo, badala ya Chaumma kama ilivyofanywa na wenzao.
Dar es Salaam. Baada ya kundi la waliokuwa makada wa Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) lililounda G55, kutimkia katika Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wawili kati yao wamebadili njia na kujiunga na ACT Wazalendo.
Waliojiunga na ACT Wazalendo ni mwanzilishi wa programu ya Chadema Digital, Glory Tausi na Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi ambao awali, walitarajiwa wangejiunga na Chaumma kama wenzao.
Wawili hao, wanathibitisha vurugu za kisiasa zinazoendelea ndani ya vyama, kwa makada kuvihama vyama vyao na kutimkia katika majukwaa mapya, kueleza Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.
Ukiacha yale makundi yaliyoshuhudiwa yakihama kutoka vyama vya Chadema, ACT Wazalendo na kuhamia CCM kwenye ziara za viongozi wa chama hicho tawala, pia kumeshuhudiwa vyama vya upinzani vyenyewe vikibadilishana wanachama.
Hivi karibuni, Wakili wa Kujitegemea, Peter Madeleka alijiunga na ACT Wazalendo akitokea Chadema, huku wengine zaidi ya 1,000 wakijiunga na Chaumma.
Mwenendo wa ACT Wazalendo wa kuthamini na kujali usawa wa kijinsia, kadhalika hatua yake ya kuonyesha nia ya kupambana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kushiriki uchaguzi, ni miongoni mwa sababu zilizotajwa na wawili hao kukichagua chama hicho.
Wawili hao ni sehemu ya wanachama wapya ambao ACT Wazalendo inawapokea, baada ya hivi karibuni kumpokea Wakili wa Kujitegemea, Peter Madeleka.
Ntobi na Glory wametangaza kuhamia ACT Wazalendo leo, Jumanne Juni 3, 2025 na kupokewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam.
Katika maelezo yake kuhusu uamuzi huo, Glory amesema amevutiwa namna chama hicho kinavyoiishi falsafa ya usawa wa kijinsia kwa vitendo na kimeonyesha thamani, kumjali na kumpenda mwanamke.
Hilo, amesema linathibitishwa na namna chama hicho kilivyosheheni wanawake katika uongozi wake wa juu, kadhalika kimekuwa kikiwapa nafasi wanawake kugombea nyadhifa za juu.
"ACT Wazalendo inaonyesha wazi kuwa ina mpango wa wazi wa kukabiliana na umasikini, uhaba wa ajira na mfumuko wa bei katika nchi yetu," amesema.
Kwa mujibu wa Glory, akiwa katika jukwaa hilo jipya la kisiasa, atakuwa tayari kuhakikisha inajengwa Tanzania yenye haki, uwazi na atakuwa tayari kuleta mabadiliko.
Amesema ni vema kukumbuka kuwa, adui wao Mkuu sio vyama vya upinzani, bali ni CCM na kwamba hawapaswi kusahau hilo.
Kwa upande wa Ntobi, amesema akiwa Chadema amewahi kuwa Diwani mwaka 2015/20 na baadaye akawa Mwenyekiti wa Madiwani katika Kanda ya Serengeti, kisha Mwenyekiti wa chama hicho Shinyanga.
Ameeleza atatumia uzoefu huo kuhakikisha anatekeleza wajibu wake wa kisiasa ndani ya ACT Wazalendo kwa kuwa anavutiwa kufanya kazi na mtu anayemwelewa zaidi katika siasa, Zitto Kabwe.
Ntobi amesema amejiunga na ACT Wazalendo kwa kuwa ni chama kinachoamini katika kupambania haki kwa kushiriki uchaguzi, badala ya kususia, akidokeza muhuni hasusiwi.
"Tulihangaika tukakuta kitu linachoitwa muhuni hasusiwi na kwamba nimeona nijiunge kuhakikisha tunaendeleza harakati hizi," amesema.
Amesema ACT Wazalendo ina sura ya kitaifa tofauti na vyama vingine na imekuwa vigumu kufyeka pori jipya bora waende kwenye lile ambacho tayari limeshafikia hatua kubwa.
Ado Shaibu amesema wiki kadhaa zilizopita alieleza kuwa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu kitabeba wajibu wa kuwa jukwaa kwa wapiganaji na wapambanaji wanaotaka kuiwajibisha CCM.
Katika mkutano wake huo, amesema aliwakaribisha wananchi wote wenye nia ya kufanya mageuzi kuhakikisha wanajiunga na chama hicho.
"Ninayo furaha kuwaleta mbele yenu wapiganaji wakubwa kabisa katika siasa za Tanzania ambao wamepata heshima ya kukaribishwa na Katibu Mkuu," amesema.
Ametangaza kwa Watanzania wengine wenye nia ya kupambana watambue kuwa hakuna jukwaa kwa yeyote anayetaka mapambano ya kweli zaidi ya ACT Wazalendo.