Prime
Usiyoyajua kuhusu safari ya G55 hadi Chaumma

Muktasari:
- Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo mamia ya waliokuwa wanachama wa Chadema kujiunga na chama hicho.
Dar es Salaam. Hatimaye siri ya mageuzi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kutoka hali ya ukame wa wanachama na ukata wa fedha hadi kuwa na uthabiti wa ghafla wa kisiasa na kifedha – imewekwa wazi.
Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe (maarufu kama Mzee wa Ubwabwa), amefichua hatua kwa hatua kilichojiri nyuma ya pazia kwenye mchakato huo, akieleza jinsi mpango wa kupokea mamia ya wanachama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ulivyosukwa na kutekelezwa.
Uamuzi wa makada hao kujiengua Chadema na kujiunga Chaumma ulianza kuwa wazi Mei 7, 2025 pazia likifunguliwa na waliokuwa wanaunda sekretarieti ya uongozi uliomaliza muda wake chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe kwa hoja walikuwa hawaridhishwi na utendaji wa uongozi mpya wa Chadema chini ya Tundu Lissu.

Kundi hilo liliwajumuisha manaibu katibu mkuu Bara na Zanzibar, Berson Kigaila na Salumu Mwalimu na aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano na mambo ya nje, John Mrema na baadaye kufuatiwa na wengine.
Mwishoni mwa wiki hii, Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Rungwe ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ambapo amesimulia mpango wa wanachama hao kujiunga na Chaumma ulivyosukwa, akisema yalikuwa mazungumzo ya takriban miezi miwili kuanzia Machi 2025.
“Mtu wa kwanza kunitafuta na kuniambia wanataka kujiunga na Chaumma alikuwa John Mrema, ilikuwa kwa njia ya simu ndipo nilipomweleza aje ofisini na kweli alikuja hapa ofisini tukaanza kuzungumza mambo ya chama chetu. Nikampatia katiba yetu aende akaisome aielewe kwanza kabla ya kuendelea na mazungumzo yetu,” amesema Rungwe.
Baada ya hatua hiyo, Rungwe anasema walikubaliana na Mrema wakutane wiki moja baadaye na walikutana na kuhitimisha kuwa inabidi mwenyekiti huyo azungumze kwanza na viongozi wenzake.
Anasema hatua ya Mrema na wenzake kukubali kukutana naye kwa mara mbili, ilitosha kuamini kuwa ilikuwepo nia ya dhati kwao kutaka kujiunga na Chaumma.

“Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa katiba yetu inaruhusu lakini mapendekezo waliyokuja nayo ni kutaka baadhi ya nafasi za juu za chama na kama unavyojua suala la madaraka ni jambo zito, lazima uzungumze na wenzako waliridhie,” anasema.
Kwa mujibu wa Rungwe, kina Mrema walikwenda na mapendekezo ya nafasi za katibu mkuu, naibu katibu mkuu na makamu mwenyekiti na kwa sababu hiyo, isingekuwa rahisi aamue mwenyewe bila kuushirikisha uongozi wote.
“Haikuwa kazi rahisi, tulianza kuelezana hapa ndani, hatukuwa na matatizo na kila mtu alikuwa anaeleza hisia zake lakini mwisho wa siku watu wangu walifurahi na kukubali kuachia nafasi kwa masilahi mapana ya chama,” anasema.
Baada ya mapendekezo hayo, Rungwe amesema alianza kuzungumza na aliyekuwa Katibu Mkuu, Mohammed Masoud na Naibu Katibu Mkuu Bara, Rahman Rungwe, wote walikubali kuachia nafasi hizo.
“Hawa walinielewa mapema na walisema wamekaa hapa kwenye chama kwa muda mrefu, hawajaona mabadiliko ya maana, sasa wenzetu wanakuja labda wanakuja na mabadiliko, ‘sasa mimi ning’ang’anie nini na si mila yetu’,” anasema Rungwe.
Anasema uzito wa kulimaliza hilo, ulibaki kwenda kuzungumza na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bara, Kayungo Mohammed anayeishi mkoani Morogoro, hivyo alilazimika kufunga safari kumfuata.
“Niliona nisimweleze kwa simu kwani haileti heshima au kumwita aje Dar es Salaam na niliamua kufunga safari kwenda kwake Morogoro na kufanya naye mazungumzo, alinielewa vizuri na alinijibu yuko tayari kupisha na hana wasiwasi hata kidogo,” anasema Rungwe.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Rungwe, ilifuatiwa na mchakato wa kuhakikisha wanasiasa hao wanajiunga rasmi na Chaumma, huku vyombo mbalimbali vya habari vikimfuata kutaka kujua ukweli wa mambo.
“Katikati ya hilo, waandishi wa habari wakawa wananifuata kuniuliza wanasikia hivi, mara hivi, niliwakatalia na sikutaka kusema chochote kwa sababu chungu kilikuwa bado hakijaiva, nikuambie nini sasa,” anasema.
Ukimya wake kwa wanahabari, anasema ulichochewa na usiri wa mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kwa pande hizo mbili, hata hivyo anashangaa ni nani aliyezivujisha.
“Wale walipokuja hawakutaka nafasi ya mwenyekiti kwa kuwa hii ni ya kwangu mimi, hakuna anayeweza kuichukua na walikuwa hawana haja na nafasi ya mwenyekiti,” anasema.
Baada ya kukamilika mazungumzo na viongozi wa chama chake, anasema walikutana tena na G55 la waliokuwa wagombea ubunge na udiwani Chadema 2020, kukubaliana eneo na siku ya kuwapokea.
“Ingawa kulikuwa na usiri mzito tulikubaliana tukio la kuwapokea lifanyike Golden Tulip Masaki na kama mlivyoona nadhani mlikuwepo, kulitanguliwa na vikao vya chama kisha waliitwa kutambulishwa, kisha kuthibitishwa na halmashauri kuu ya chama chetu,” anasema.

Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe
Akizungumzia jambo hilo, Dar es Salaam Mei 21, 2025, siku wanapokelewa wananchama wapya 3,000, Ubungo Plaza, Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu aliwataja Julius Mwita, John Mrema, Edward Kinabo, Benson Kigaila, Catherine Ruge, Suzan Kiwanga, Devotha Minja na yeye mwenyewe kuwa ndio waliofanikisha safari hiyo.
“Walipokea maneno mengi ya kejeli, vitisho vingi, kukatishwa tamaa kwingi lakini hawakurudi nyuma, Kinabo alikuwa anachukua mihutasari yote ya vikao kusimamia vyombo vya habari usiku na mchana kuwaratibu,” anasema.
Kipekee, Mwalimu pia alimtaja Mrema kama aliyefanya kazi kubwa ya kuwaongoza kwenye vikao vya mashauriano wakati unafanyika utafiti wa chama gani wanaweza kwenda kujiunga.
“Nakushuru Mrema umefanya kazi kubwa, hadi sasa upara naona umeongezeka umefanya kazi kubwa yakupigiwa mfano,” anasema Mwalimu.
Wafanya utafiti
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Kigaila amesema kabla ya kutangaza kuihama Chadema, walianza kufanya utafiti kwa kuangalia vyama 17 vyenye usajili wa kudumu isipokuwa CCM na Chadema.

“Chadema tunakotoka si mbadala wetu kurudi, na CCM haiwezi kuwa mbadala wetu ukitoka upinzani kwenda CCM maana yake unastaafu siasa, kwa hiyo unaenda kupumzika,” anasema Kigaila.
Maneno mengi
Baada ya kuwapokea wanachama wapya kutoka Chadema, Rungwe anasema maneno yamekuwa mengi kulingana na matukio yanayofanyika kuonekana ni ya gharama kubwa.
“Ni kweli mambo yanafanyika makubwa, tunaleta mabadiliko na hata ukiangalia mwonekano wa fulana zetu ni hatari, ingawa maneno ya watu yamekuwa mengi siyachukulii uzito, yamekuwa ya kawaida mno kama nasaidiwa na fedha kwani kuna tatizo gani,” anasema.

Hata hivyo, anasema hakuna sheria wala taratibu zilizovunjwa kuhusu hatua yao ya wanasiasa hao kujiunga na Chaumma.
Kuhusu madai ya chama chake kudhaminiwa na baadhi ya vyama ikiwemo CCM, Rungwe anasema CCM ni chama kama cha kwake, kikitoa fedha linakuwa jambo la kawaida.
“Ukweli wa mama yangu, yote yanayojitokeza kwenye chama changu sijapokea hela yeyote, sijajua zinatoka wapi, kama watanipa nitapokea si watakuwa wamenipa msaada, hakuna aliyekataza,” anasema.
Anasisitiza hawezi kukataa msaada kutoka chama chochote, akirejea tukio la Tundu Lissu kuwahi kusaidiwa fedha na watu kutoka makundi mbalimbali ikiwemo CCM ununuzi kuchangia gari lake na alizipokea.
“Alipewa fedha kwa ajili ya kwenda kununua gari tena walisema hadharani na Lissu alizipokea, sasa inakuwaje akipewa Rungwe watu wanachukia …unachukia nini? Au hamtaki na mimi nipate msaada,” anasema Rungwe kwa msisitizo.
Bado anautaka urais
Licha ya kupokea wanachama hao, Rungwe anasema katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu, chama hicho kinakwenda kushindana si kushiriki.

“Sasa tumepata nguvu na wenzetu wanaokuja wataleta ushindani mkubwa na tutapita mkoa kwa mkoa kuwaeleza watu tuna jambo gani na tunataka kuwafanyia nini? Kuwaeleza azma yetu kwao, hatuwezi kuwaeleza habari ya ubwabwa ukiwa umejifungia ndani,” anasema.
Katika uchaguzi huo, anasema dhamira yake ya kugombea urais iko palepale, ingawa bado hajui uamuzi wa wanachama utakuwaje muda utakapofika.
“Ila binafsi nitapeleka jina langu katika mchakato wa ndani wa chama wakiamua kama ni mimi basi, lakini ikiwa vinginevyo, haina shida. Nia ya kuwania urais ninayo hadi hivi sasa bado sijaitengua,” anasema.
Anasema mbali na yeye kuwania urais, pia wataweka wagombea wa udiwani na ubunge kila sehemu kwa kuzingatia sheria na hawatasusa.
Mbadiliko
Rungwe anasema kwa sasa yuko tayari kufanya mabadiliko yoyote ama ya kikatiba au muonekano wa chama hicho alichokianzisha mwaka 2012 na kupata usajili wa kudumu maka 2013.

“Tumewapa katiba wasome na lazima mjue waliojiunga tupo kitu kimoja, hakuna wageni tena ukishakuja hapa ugeni haupo tena, kwa hiyo wakitaka mabadiliko tutashauriana,” anasema.
Anasisitiza hakukiuza chama chake, kwa kuwa ni wajibu wa chama kupokea wanachama wapya, hivyo watu wasishangae kuona wengine wakijiunga na Chaumma.
Amtaja Mbowe
Katika mahojiano hayo, Rungwe anasema hakuwahi kuzungumza na Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe kuhusu mpango wa kujiunga na chama hicho, ingawa naye anasikia tetesi zikielezwa mitaani.
“Akija tutamkaribisha hakuna shida yoyote, hatuwezi kukataa mwanachama ilimradi afuate utaratibu tunamkaribisha bila ubishi wowote na hata wengine kama wapo waje milango iko wazi,” anasema Rungwe.
Si utayari wa kumpokea Mbowe kama mwanachama pekee, anasema yuko tayari hata ikitokea anataka kuwania urais na wajumbe wakampitisha, atamwachia.
“Hamna shida akihitaji nafasi yangu tutaenda kwenye uchaguzi wajumbe wakiamua nitakubali, si watakuwa wameamua, kwani kuna shida gani ni jukumu la kuongoza chama tu,” anasema.
“Lakini, siwezi kumpisha hivi hivi kwa kuwa tuna mchakato wa ndani, atatangaza nia na mimi nitatangaza kama wajumbe wataamua kumchagua yeye, basi haina shida nitakuwa tayari kuungana na wenzangu,” anasema.
Wakati Rungwe akijibu hivyo, Kigaila katika mahojiano yake na Mwananchi amesema amekuwa akikutana mara kwa mara na Mbowe lakini wanazungumza mambo ya kawaida, hajawahi kumgusia kuhusu kujiunga na Chaumma.
“Mbowe alikuwa kiongozi wangu na rafiki yangu, naweza kuonana naye mara kwa mara na kuzungumza mambo ya kawaida kwa sababu ni mtu anayeweza kukusaidia mawazo ya kiuongozi na kibiashara,” anasema.
Kigaila anasema Mbowe ana utajiri mwingi ukimtumia unanufaika, ni mtu mwenye akili mbovu tu ndiye anayesema mwanasiasa huyo hana maana.
Falsafa ya ubwabwa
Wakati mahojiano na Rungwe yakiendelea, aliwaagizia ubwabwa waandishi na ukaletwa. Alipoulizwa huwa anamaanisha nini anaposema sera ya ubwabwa amesema: “Huwa ninamaanisha chakula kinapaswa kutolewa shuleni na hospitalini bure.”

Anasema miaka ya nyuma Serikali ilikuwa ikitoa chakula shuleni: “Mtoto akiwa ameshiba, hata akifundishwa anaelewa, sasa utamfundishaje mwanafunzi mwenye njaa akaelewa, kwa hiyo Chaumma tunasema tutatoa chakula shuleni.”
Rungwe anatolea mfano, mtu ambaye ametoka mkoani kwenda Dar es Salaam: “Akiwa Dar es Salaam na hana ndugu, basi akaumwa na kupelekwa hospitalini, akiwa hospitali hana ndugu na pale baba na mama yake ni Serikali, ndiyo inapaswa kugharamia chakua.”
Amesema hata waliojiunga ndani ya chama hicho wataeleweshwa dhana ya kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni na hospitalini kwa wale watakaotakiwa kulazwa na kama watakuwa hawaelwi dhana hawatachoka kuwaeleza hilo na kulibeba.
“Unajua mtu aliyekula akashiba, huwezi kumdanganya. Mtu mwenye shibe anaweza kulizalisha na kuchangia kwenye taifa. Kwa hiyo Chaumma tunaposema ubwabwa tunamaanisha chakula kitolewe shuleni na hospitalini,” amesema.
C4C
Kuhusu ziara ya chama hicho ya Chaumma For Change (C4C) inayotarajiwa kuzinduliwa jijini Mwanza Juni 1, 2025 na kuzunguka mikoani kwa siku 16, Rungwe anasema atakuwa kwenye jopo hilo pamoja na vijana wake.
“Nitakuwa nao pamoja siwezi kuwaacha, ingawa siwezi kumaliza siku zote lakini tutakuwa pamoja, mimi ni nahodha lazima niwepo…utasema hutaki...hutaki nini? Awee, nitashiriki kama kawaida,” anasema.

Akizungumzia ziara hiyo, Mei 21, 2025 kwenye mkutano maalumu wa kuwapokea wanachama wapya, Mwalimu alisema Rungwe kama atakuwa amechoka wapo tayari kutumwa wakakijenge chama hicho.
“Tumesema hakuna kulala na bahati nzuri tuna mwenyekiti… tutamwambia atulie aziachie kazi hizi mashine, tupe kibali tukupigie huu mzigo, si ndio mzee Rungwe?
“Mzee amefanya kazi kubwa katika nchi hii, wengine hawajui Rungwe ni mmoja kati ya mamilionea wa nchi hii, mkimuona anakuja na sera ya ubwabwa ni kwa sababu anajua thamani ya kushiba,” anasema.
Rungwe ni nani
Rungwe anasema alizianza siasa akiwa kada wa Tanu baadaye CCM, kabla ya kuanza kwa siasa za vyama vingi, alipojiunga na NCCR-Mageuzi alikokaa kwa muda mrefu.
“Baada ya kukaa kwa muda mrefu niliingia kwenye mgogoro na viongozi, mambo yalikuwa magumu ndipo niliposhauriana na wenzangu nia yangu ya kuanzisha chama kipya,” anasema.
Rungwe anasema baada ya kuwaeleza wenzake walikubali wazo lake na kuahidi kumuunga mkono, ndipo mwaka 2012 alianza mchakato na hatimaye 2013 Chaumma ikazaliwa.