Kamati Kuu Chaumma yateua wakurugenzi wa chama, wamo G55

Muktasari:
- Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa chama, Hashim Rungwe, kimejadili ajenda kuu mbili, ikiwemo kuchagua wakurugenzi wa idara za makao makuu ya chama kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, Ibara ya 55.
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimefanya uteuzi wa wakurugenzi katika idara mbalimbali za chama hicho, ikiwajumuisha viongozi waliotoka Chadema na wale waliojiuzulu nafasi zao kuwapisha wanachama wapya.
Leo Jumamosi, Mei 24, 2025, kikao cha Kamati Kuu kilichohusisha wajumbe 15, kimefanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe.
Kikao hicho kimejadili ajenda kuu mbili--- moja, kuchagua wakurugenzi wa idara za makao makuu kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, Ibara ya 55; na mbili, kujadili na kupitisha ratiba ya ziara ya kitaifa ya C4C (Chaumma For Change) inayotarajiwa kuzinduliwa Juni Mosi, 2025, kwa lengo la kutambulisha viongozi wapya wa ngazi ya taifa.
Walioteuliwa na Kamati Kuu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho, ni Kayumbo Kabutali, Mkurugenzi wa Idara ya Bunge, Halmashauri na Serikali za Mitaa; John Mrema, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi; naibu wake ni Ipyana Samson.
Wengine ni Catherine Ruge, Mkurugenzi wa Uchumi, Fedha na Mipango; naibu wake ni Stewart Kaking’i; Ismail Kangeta, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kampeni na Organization; manaibu wake ni David Chiduo na Mohamed Chiduo.
Pia wamo Rahman Rungwe, Mkurugenzi wa Uhusiano, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; msaidizi wake ni Aisha Madoga; Edward Kinabo, Mkurugenzi wa Itikadi na Mafunzo kwa Umma; naibu wake ni Dorothy Mpatiri.
Kwa upande wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu, mkurugenzi bado hajateuliwa. Hata hivyo, Estae Fulano ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa idara hiyo.
Vilevile, Elia Marwa ameteuliwa kuongoza Idara ya Utafiti, Tathmini na Ufuatiliaji, huku Naibu Mkurugenzi akiwa Bibiana Benedicto. Idara ya Ulinzi bado haijapata mkurugenzi wake; badala yake, inakaimiwa na Prosper Makonya.
Wengine walioteuliwa ni Julius Mwita, Katibu wa Sekretarieti; Reginald Munisi, Mtaalamu wa Mikakati; Khadija Mwago na Salma Sharifu, Wakuu wa Utawala; Magret Mlekwa, Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia.
“Katika uteuzi huo, waliokuwa viongozi kabla ya ujio wa G55 ni Kayumbo Kabutali, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara; Rahman Rungwe, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara; Ipyana Samson, aliyekuwa Katibu wa Habari na Uenezi; na Bibiana Benedicto, aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi,” inasomeka taarifa hiyo.