Bakwata yataka haki uchaguzi mkuu, Serikali yajibu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijumuika na waislamu katika sala na Baraza la Eid El Adhaa iliyofanyika Kitaifa kwenye Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni jijini Dar es Salaam Juni 7, 2025. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Muktasari:
- Bakwata imetaka haki kutendeka kwa kila hatua katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2025.
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limeiomba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutenda haki kwa kila hatua ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru na wa haki kwa vyama vyote.
Bakwata likisema hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia kuwa Serikali itasimamia sheria na kanuni zilizowekwa ili Tanzania iendelee kuwa na utulivu na uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
"Serikali kama wadau tutaichukua kauli ya INEC na jukumu letu ni kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na utafanyika katika amani ya hali ya juu kabisa," amesema Majaliwa.
Wito wa Bakwata umetolewa leo Jumamosi Juni 7, 2025 na Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Sheikh Nuhu Mruma wakati akihutubia Baraza la Eid El- Adh' haa lililofanyika msikiti wa Mohammed VI uliopo makao ya makuu ya Bakwata, Kinondoni jijini Dar es Salaam. Majaliwa alihudhuria swala na kuhutubia baraza la Eid El- Adh' haa.
"Msingi mkubwa wa amani upo katika utoaji wa haki, tunaendelea kuviasa vyama vya siasa na wagombea kufanya siasa za kistaharabu na kuepuka lugha zisizo za ustaharabu," amesema Sheikh Mruma.
Bakwata pia limetoa wito kwa Watanzania kuilinda na kuitunza amani ya nchi, kwa sababu bila amani hakutakuwa na maendeleo wala fursa ya kufanya ibada haitakuwepo.
"Sote tunafahamu mwishoni mwa mwaka huu Taifa letu linaingia katika mchakato wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, sisi viongozi wa dini tunaendelea kuombea dua ili mchakato huo uende kwa amani.
"Tunawaomba Waislamu na wananchi wote kutumia fursa hii ya kikatiba ya kuchagua viongozi au kuwa wagombea katika nafasi mbalimbali ili kupata haki ya kuchaguliwa," amesema.
Sheikh Mruma amesema Bakwata lina matumaini kuwa mamlaka husika imeshafanya maandalizi husika ili haki hiyo ipatikane kwa kila mtu.
"Tunafahamu hatua inayofuata ni watiania kuchuku fomu ndani ya vyama vyao kuomba kuteuliwa kisha kuchukua fomu za INEC. Tunaviasa vyama vya siasa, kuteua wagombea bora na wenye sifa na kuepukana wagombea wenye uchu wa madaraka wanaotaka uongozi kwa hila na kutumia rushwa," amesema.
Kuhusu maadili
Sheikh Mruma amesema Bakwata linaendelea kusisitiza maadili ambayo ndiyo msingi muhimu ili kuwa na jamii yenye kuheshimu na kuthamini watu.
Amesema hivi karibuni imeshuhudiwa baadhi ya vitendo vinakwenda kinyume cha maadili ya Kitanzania.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitoa kauli mbaya na kuwakashifu wananchi wengine katika mitandao ya kijamii wakiwamo viongozi jambo alilosema si jema na haliwezi kuvumilika kwa sababu lina madhara makubwa, ikiwamo uvunjifu wa amani.
"Viongozi wa dini tunalaani vitendo hivyo na kuvikemea vikali kwa sababu si maadili yetu. Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaofanya vitendo hivi visivyo vya kiungwana na vile vya kuwavamia na kuwaumiza watu pasipo sababu ya msingi," amesema.
Afya ya akili
Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko amesema dunia na Tanzania, jamii inakabiliwa na tishio la hali mbaya ya afya ya akili.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Tanzania, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 wananchi waliohudhuriwa vituo vya kutolea huduma za afya kwa shida ya magonjwa ya afya ya akili walikuwa 293,952 ikilinganishwa na 246,544 kwa kipindi cha mwaka 2022/23.
Sheikh Ngeruko amesema: "… Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) jambo hili tunaweza kuliona dogo lakini kila mmoja kuanzia sasa anatakiwa kulitafakari. Akili za binadamu kwa sasa zimefunikwa na tunapoelekea kwenye uchaguzi, tuwachagua ambao afya za akili zipo kiwango cha chini.
"La sivyo tutawakabidhi uongozi watu ambao afya zao akili zipo chini, itakuwa hatari zaidi wakati huo. Chujio la kupima afya duni ya akili ya mtu ni namna anavyowasilisha sera pale anapowaomba wananchi kumpa kura," amesema.
Amesema wagombea wanaowasilisha sera zao kwa kutumia matusi, kejeli, dharau na ubaguzi, hawafai kuchaguliwa kupewa uongozi.
"Hili ni angalizo nalitoa kwenu tuna tatizo kubwa la afya ya akili, nenda kwenye mitandao ndio mtanielewa. Mtandao ndiyo unatuonyesha hali ni mbaya kiasi gani duniani," amesema.