Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma yalia na INEC kutenda haki uchaguzi wa Oktoba

Katibu Mkuu wa Chama cha Chaumma, Salum Mwalimu akiendesha harambee ya kuchangia Msikiti wa Bakwata Masjid Noor Simiyu kwenye Sikukuu ya Eid-El-Adha leo Jumamosi Juni 7, 2025.

Muktasari:

  • Salum Mwalimu, katibu mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) atoa wito kwa watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutenda haki katika kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba ili Watanzania wote wavuke salama na wakiwa wamoja.

Bariadi. Katibu Mkuu wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum  Mwalimu ametoa wito kwa watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutenda haki katika kusimamia uchaguzi Mkuu wa Oktoba baadaye mwaka huu.

Ametoa wito huo leo Juni 7, 2025, baada ya kuungana na waumini wengine wa dini ya Kiislamu kwenye swala ya Eid al-Adha katika msikiti wa Bakwata Mkoa wa Simiyu – Masjid Noor, uliopo Bariadi.

Akizungumza baada ya kumaliza kuongoza harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa msikiti huo, Mwalimu amesema wanaposherekea sikukuu hiyo viongozi wasihubiri amani bila haki, hasa kwa kuwataka wasimamizi wa uchaguzi wakatende haki.

"Tunapohimiza amani tuhubiri na haki, vyote viende sambamba na hata watendaji watakaoenda kusimamia uchaguzi mkuu wakatende haki ili tukimaliza wote tuwe wamoja," amesema. Mwalimu

Pia amewataka waumini hao na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki haki hiyo ya msingi ya kuchagua, kuchaguliwa na kupiga kura kama Katiba ya Tanzania inavyoeleza.

"Mkashiriki uchaguzi. Msirudi nyuma, nendeni mkagombee udiwani, ubunge na urais, tukapeane mawazo kuhakikisha tunashinda na kupata viongozi watakaokuja kuondoa matatizo yanayowakabili Watanzania," amesema Mwalimu

Kwa upande wake Imamu wa Masjid Noor, Yakubu Saburi katika hotuba yake, amewasihi Watanzania na waumini wa dini hiyo waache kuchezea amani iliyopo ili wavuke salama kwenye uchaguzi huo.

"Nawaomba ilindeni amani iliyopo tuvuke salama kwenye mchakato wa uchaguzi na kupata viongozi bila vurugu. Naomba vijana wa kitanzania, hasa waislamu, wasitumike kuvuruga amani iliyopo," amesema Yakubu.

Amesema wapo watu wenye imani kama waliopo Tanzania kama Yemen na Syria lakini walipoichezea walipoteza ndugu zao, mali zao na kujikuta wakirudi nyuma.

"Neno amani ni kila kitu cha thamani kubwa, inapaswa kulindwa. Kuna baadhi ya nchi hata ibada kama hii hawawezi kufanya ni kwa sababu wamechafua na kuharibu amani ambayo ni nguzo muhimu kwa kila jambo," amesema.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Ukombozi wa Umma Chaumma, Salum Mwalim akishiriki ibada ya Eid-El-Adha Mkoani Simiyu kwenye ya Msikiti wa Bakwata leo Juni 7,2025.

Amesema vita ni haramu, yakitokea makombora inakuwa hali tofauti walio wengi wanachanganyikiwa mtu badala ya kumwokoa mwanawe au mkeo anajikuta anabeba begi.

"Viungo tulivyopewa na Mungu tuvitumie kwa uangalifu, macho tuone magumu wanayopitia wenzetu, masikio tusikilize na kuelewa wanayopitia wenzetu, tutumie kugusa maisha ya wengine.

"Tusikubali kutumika kuharibu amani yetu, mara nyingi tunaongea amani wengi wanahisi tuko upande fulani, jamani hali ikivurugika hakuna atakayeona hilo," amesema.

Katika hatua nyingine, Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Issa Kwezi alitumia fursa hiyo, kusisitiza umuhimu wa kulinda maadili akijenga hoja kuwa ilivyo sasa nchini, hata watu wazima hawana maadili, yote hayo yatokea kwa kisingizo cha ukuaji wa demokrasia.

"Ndugu zangu maadili ni kwa wote kuanzia watoto hadi watu wazima, kuheshimiana hata kiongozi lazima uchunge cheo chako kwa kuwajali wenzako na kulinda heshima zao. Tutumie lugha zuri katika kuwahusia watu na ukikosoa tumia njia ya kistaarabu," amesema

Amesema kutokutumia mfumo mzuri katika kufikisha ujumbe unasababisha mgongano kwa yule unayemfanyia kuhisi unamkosea heshima.

Mwalimu na viongozi wenzake wa chama hicho, wamesitisha mikutano ya Operesheni yake ya Chaumma For Change (C4C) kwa siku mbili Ijumaa na Jumamosi kutoa nafasi kwa wananchi kusherehekea sikukuu hiyo.

Ratiba ya mikutano ya hadhara ya kuongea na umma sasa itaendelea kesho Juni 8, 2025, katika mikoa ya Kanda nne ya Victoria, Kaskazini, Magharibi na Serengeti.