Majaliwa: Tuzingatie sheria kwa shughuli tunazofanya, kuabudu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia kwenye sala na Baraza la Eid El Adhaa lililofanyika Kitaifa kwenye Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni jijini Dar es Salaam leo Juni 7. 2025. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Muktasari:
- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema shughuli mbalimbali ziwe za kikundi, binafsi au za umma lazima zizingatie sheria.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wanaofanya shughuli mbalimbali ziwe za kikundi, binafsi au za umma kuzingatia sheria, ikiwemo katika kutekeleza uhuru wa kuabudu.
"Tunavyokuja kuabudu, lazima tuzingatie sheria ya uhuru wa kuabudu. Katiba ya Tanzania ibara 19(3) imeweka bayana ufafanuzi wa kuabudu ilimradi hakuna uvunjifu wa amani na sheria za nchi.
"Kuabudu si watu tu kukutana na kufanya wanavyotaka, bali iko sheria iliyoruhusu hata msikiti kuwa hapa au kanisa kuwa pale, ndiyo iliyoruhusu kiongozi wa dini awepo ili kuzungumzia masuala ya dini," amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijumuika na waislamu katika sala na Baraza la Eid El Adhaa iliyofanyika Kitaifa kwenye Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni jijini Dar es Salaam Juni 7, 2025. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Majaliwa ameeleza hayo leo Jumamosi Juni 7, 2025 alipohutubia Baraza la Eid El- Adh' haa lililofanyika katika Msikiti wa Mohammed VI uliopo makao ya makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Kinondoni, Dar es Salaam.
Baraza la Eid El- Adh' haa, lilitanguliwa na swala iliyofanyika katika msikiti huo na kuhudhuriwa na waumini wa dini ya Kiislamu.
Eid El- Adh' haa ni sikukuu inayoadhimishwa baada ya Waislamu kukamilisha ibada ya Hijja ambayo ni nguzo ya mwisho katika tano za Uislamu na hufanyika katika miji ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia.
Majaliwa amesema masuala yote ya dini yanalindwa na sheria, hata uwepo wa masheikh na maimamu, kwa sababu sheria imewaruhusu kufanya hivyo.
"Tunapopata nafasi ya kuja hapa kama leo hii, tunatarajia viongozi mtatumia muda mwingi uliotengwa kwa ajili ya ibada kuzungumzia dini na si vinginevyo, kwa sababu uwepo wa jengo hilo na ujio waumini ni kuja kusikia neno la Mungu na kuendelezwa kiimani, hali itakayoleta amani na utulivu.
"Tunafanya haya kwa sababu tunazo sheria, unapoivunja sheria na kufanya vinginevyo sheria inachukua mkondo wake. Lazima tukumbushane na kufanya mambo kwa sababu kuna uhuru, hata hivyo uhuru una mipaka. Haki lazima iende na kutimiza wajibu," amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia kwenye sala na Baraza la Eid El Adhaa lililofanyika Kitaifa kwenye Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni jijini Dar es Salaam leo Juni 7. 2025. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati ambao Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa Juni 2, 2025 alitangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima, lenye makao yake makuu Ubungo, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa barua, iliyotolewa Jumatatu Juni 2, 2025 Kihampa alieleza kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337: “Kwa kutoa mahubiri yenye muelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.”
Viongozi wa dini
Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema Serikali inawaamini viongozi wa dini wa madhehebu yote kwa sababu wamekuwa chachu ya kuimarisha amani na mshikamano katika Taifa, kupitia mahubiri wanayoyatoa.
Amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano mzuri kati yake na viongozi wa dini zote, wa madhehebu mbalimbali nchini, ili kila mmoja ashiriki kuhakikisha Taifa linakuwa na amani ya kutosha.

"Ninaamini viongozi wa dini mtaendeleza jukumu hilo la kuwasihi Watanzania kuwaona kila mmoja ana mchango wa kulifanya Taifa la Tanzania kuwa tulivu na kuimarisha mshikamano miongoni mwetu," amesema.
Amesema dini ina misingi yake na imejengwa kwa namna ya kuwafanya waumini wake kuwa na staha, ustaharabu, uvumilivu, hivyo viongozi wa dini pia wana nafasi kubwa ya kuhamasisha waumini kushiriki shughuli za maendeleo.
"Dini imeifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani wakati wote na viongozi wa dini mnayo nafasi ya kukemea mambo yote yanayosababisha mmomonyoko wa maadili ndani ya Taifa hili. Imani hii imejengwa kwa miaka mingi na Taifa tuna masilahi nayo," amesema.
Majaliwa amesema waumini wanapojengwa kiimani, basi iwe ya kujenga Taifa si kuwajengea watu imani inayokwenda kulibomoa Taifa, ambayo itasababisha jamii kuharibika.
Amesisitiza kuwa dini haina nafasi ya kubomoa jamii, bali ipo kwa ajili ya kujenga jamii inayoizunguka.