Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Amani idumishwe kuelekea uchaguzi mkuu-Kadhi Pwani

Waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa nje ya msikiti wa Masjid Muuminina Kibaha Mkoa wa Pwani. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Kadhi wa Mkoa wa Pwani, Sheikh Zuberi Rashidi amesema kipindi cha uchaguzi huwa nyeti, hivyo ni wajibu wa kila raia kuhakikisha hatumii jukwaa hilo kuchochea vurugu au chuki.

Kibaha. Amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu ni ujumbe waliopewa waumini wa Kiislamu leo Juni 7, 2025 baada ya swala katika Msikiti wa Muuminina uliopo Mailimoja, mkoani Pwani kuadhimisha sikukuu ya Eid El -Adh'haa.

Waumini hao pia wamechinja mifugo mbalimbali kwa ajili ya sadaka katika maadhimisho hayo.

Akizungumza baada ya swala hiyo, Kadhi wa Mkoa wa Pwani, Sheikh Zuberi Rashidi amewasihi waumini waendelee kuwa mabalozi wa amani katika jamii hasa wakati huu Taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu.

“Uislamu ni dini ya amani tunapaswa kuonyesha mfano katika kuheshimiana, kushiriki uchaguzi kwa amani na kuwachagua viongozi tunaowaona wanafaa kwa masilahi ya Taifa,” amesema.

Amesema kipindi cha uchaguzi huwa nyeti, hivyo ni wajibu wa kila raia kuhakikisha hatumii jukwaa hilo kuchochea vurugu au chuki, bali kulinda umoja wa kitaifa.

Adam Mwasha, kiongozi wa msikiti huo amesema jumuiya ya waumini wa Muuminina imechinja ng’ombe 20 kwa ajili ya kugawa nyama kwa waumini na jamii inayowazunguka, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha ibada hiyo ya kipekee inayohimiza moyo wa kujitolea na kushirikiana.

“Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) imekuwa ikisisitiza mshikamano na upendo miongoni mwa waumini na sisi tumejitahidi kuonyesha hayo kwa vitendo kupitia sadaka ya Eid. Tunashirikiana na kuwasaidia wasiokuwa na uwezo,” amesema.

Aisha Salumu, muumini aliyeshiriki swala katika msikiti huo ameishukuru jumuiya hiyo kwa kuweka mazingira rafiki kwa kila mtu kushiriki.

“Tulishirikiana kuchangishana fedha mapema, tukafanikiwa kununua ng’ombe kwa ajili ya kuchinja. Hakika maandalizi yamekuwa mazuri na yamewawezesha wanawake kushiriki kikamilifu,” amesema.