Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheikh Twaha ahimiza wanasiasa kuhubiri amani, mshikamano

Muktasari:

  • Awataka watoe kauli zenye kujenga, kuheshimu na kutunza amani ya Tanzania.

Waumini wa dini ya Kiislamu (Sunni) mkoani Morogoro wamekusanyika kwenye swala ya Eid-ul -Adh – haa iliyofanyika katika viwanja vya shule Sekondari Forest Hill Manispaa ya Morogoro katika ibada ambayo imeongozwa na Imam Abdalaah Ahmad leo Ijumaa Juni 6, 2025.

Eid-ul -Adh – haa ni sikukuu inayoadhimishwa na Waislamu ulimwenguni kote kufuatia kukamilika kwa ibada ya Hijja kwa waumini wa dini hiyo, (Makkah), ikiwa ni nguzo moja wapo kati ya nguzo tano za Uislamu.

Katika ibada ya Hijja (Hajj), Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani hukusanyika bila kujali tofauti zao za mazingira, lugha, jinsia au rangi, kwa lengo la kuonesha usawa na umoja mbele ya Mwenyezi Mungu na hukutana katika eneo la Arafat kwa ajili ya ibada hiyo muhimu.

Tofauti na ibada nyingine kama swala, sadaka na saumu ambazo hufanyika mara kwa mara, Hijja inafanyika mara moja tu kwa maisha, ila kwa wenye uwezo wanaweza kwenda zaidi ya mara moja.

Katika hotuba yake mbele ya waumini wa dini hiyo baada ya kumaliza swala ya Eid-ul -Adh – haa, Sheikh Ibrahim Twaha, amevitaka vyama vya siasa nchini Tanzania kuhakikisha kuwa mawasiliano na kauli zao zinazingatia masilahi ya taifa kwa kulinda na kudumisha amani iliyopo.

“Nawahusia vyama vyote vya siasa vya Tanzania, tunaomba ndani ya kauli zenu mnazozungumza ziwe zenye kujenga na kuheshimu na kuhifadhi amani hii ambayo tumeihangaikia.

“Amani tuliyonayo ni wazi inawavutia hata watu kutoka mataifa mbalimbali kuja kwetu kufanya vikao vyao. Hata nchi ambazo zina migogoro pia zinakuja kufanya vikao vya usuluhishi nchini kwetu,” amesema Sheikh Twaha.

Sheikh Twaha ambaye pia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation,  amesisitiza kuwa kuwa Tanzania imejijengea heshima kimataifa kama nchi ya utulivu na kwamba ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha tanalinda taswira hiyo njema, hasa katika kipindi hiki ambacho harakati za kisiasa zinaendelea kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu 2025.

“Waislamu mnafanya ibada zenu vizuri, nawahusia msikubali kabisa kutoa maneno  ya uchonganishi yatakayoharibu amani hii. Acheni wanasiasa waongee, vyama vyao viongee, lakini tunawaombeni kada zote za vyama vya siasa hebu kuweni mstari wa mbele kudumisha amani tuliyokuwa nayo Tanzania,” ameongeza Sheikh Twaha.

Pia, Sheikh Twaha amesisitiza waumini wa dini hiyo kuzingatia maadili, hasa kwa wanawake wa Kiislamu kuendelea kuishi namna maadili ya dini yao inavyowaongoza, pamoja na kutilia mkazo suala zima la malezi imara kwa watoto kujenga kizazi ambacho kitakuwa na hofu ya mungu.

Kauli hiyo ya Sheikh Twaha, imeungwa mkono na Sheikh Salimu Dulla, Mlezi wa Taasisi ya The Islamic Foundation, pamoja naye Adam Kitika, Mratibu wa JAI Mkoa wa Morogoro wakisisitiza kuwa viongozi wa kidini wana jukumu kubwa katika kuunganisha jamii na kuhakikisha kuwa tofauti za kisiasa hazigeuki kuwa chanzo cha migogoro.