Makini wataja vipaumbele vitatu wakichukua fomu za urais
Dodoma. Mgombea urais wa Chama cha Makini, Coaster Kibonde amechukua fomu ya kuomba kuwania nafasi hiyo huku akiainisha mambo matatu.
Leo Jumapili Agosti 10, 2025, Kibonde akiongozana na mgombea mwenza wake, Azza Haji Suleiman wameingia katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) saa 3:10 asubuhi na kupokewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima.
Wagombea hao wameingia katika viunga vya INEC wakiwa na msafara wa magari matatu na wapambe wachache waliovalia sare za chama hicho na kukaribishwa ndani ya ukumbi wanakotolea fomu.
Baada ya kukabidhiwa fomu, Kibonde amesema Chama cha Makini kimejipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuongozwa na vipaumbele vitatu ambavyo ni elimu, kilimo na afya.
"Naamini Oktoba tunakwenda kushinda kiti cha Rais na kutinga Ikulu, Serikali yetu ni ya matumaini, kila Mtanzania atafurahi," amesema Kibonde.
Katika ufafanuzi wake, amesema kumnyima elimu mtoto wa Kitanzania ni sawa na kumpa kifungo cha maisha, lakini mtu akinyimwa afya ni sawa na hukumu ya kifo
"Kwenye afya tunakuja na kitu kinaitwa Care Makini ambayo ni bima kwa wote na tutajenga vituo vya afya vya kisasa kila kata, lakini kwa upande wa kilimo, tutahakikisha kila kijana anapatiwa ekari tano ili alime kisasa," amesema Kibonde.
Hata hivyo, amesema katika safari ya kuisaka Ikulu, wamejenga matumaini makubwa kutoka kwa INEC kwa namna ilivyowashirikisha wakiamini kuwa watatangazwa baada ya kushinda uchaguzi wa Oktoba 2025.