Prime
Kitanzi cha mwisho cha watiania CCM
Dar es Salaam. Hatima ya nani atakayepeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi za ubunge, uwakilishi wa majimbo na viti maalumu Tanzania Bara na Zanzibar, inatarajiwa kujulikana ndani ya saa 72 zijazo.
Muda huo wa siku tatu unatajwa kuwa “tanuri la mwisho” kwa wote waliowania nafasi hizo, wakisubiri kupitishwa rasmi ili kuingia Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Uamuzi huo utatokana na matokeo ya vikao vya Kamati Kuu (CC) na baadaye Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), vinavyotarajiwa kufanyika kuanzia kesho, Alhamisi Agosti 21 na Ijumaa Agosti 22, 2025.
Vikao hivyo ndivyo vya mwisho kuamua majina ya wagombea wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Safari hiyo ya mchakato ilianza Juni 28, 2025, pale wanachama walipochukua fomu kuomba ridhaa ya chama. Baada ya hapo, walihojiwa na kupitishwa kwenye vikao vya awali vya mchujo, kabla ya kupigiwa kura za maoni na wajumbe Agosti 4, 2025.
Katika hatua hizo, baadhi ya watiania walikatwa mapema na vikao vya chama, huku wengine wakiangushwa na wajumbe kupitia kura za maoni.
Hata hivyo uteuzi huo unatajwa kwamba utahusisha zaidi walioongoza kwa kura, kama ulivyo mtazamo wa Dk Benson Bana, balozi na mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),.
Amesema iwapo CCM itaamua kuwapitisha wale walioongoza katika kura za maoni, basi wabunge wengi wa zamani hawatakuwa bungeni katika Bunge la 13.
Mwanazuoni huyo ameeleza hilo linadhihirisha kuwa, wanasiasa hao hawachaguliki tena na wananchi, ndiyo maana wajumbe wameanza kuwatenga.
“Kwenye siasa watu wanaahidi uongo au wanaahidi mambo mengi wakati hawawezi kuyatimiza na bahati mbaya wananchi hawapendi uongo, ndiyo maana unakuta mbunge anaishia kipindi kimoja,” amesema.
Licha ya mtazamo huo, vikao hivyo vitakavyoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan ndivyo vyenye uamuzi wa mwisho wa kumteua yeyote kati ya aliyeingia katika kura za maoni.
Kutokana na uhalisia huo, ndio maana kuna hofu na wasiwasi miongoni mwa watiania wa nafasi hizo.
Hofu zaidi inatokana na malalamiko dhidi ya vitendo vya rushwa na vingine vinavyomwondolea uhalali mtiania, hivyo wengi wao hawajui nani kati yao anatuhumiwa au taarifa zake zimewafikia wakubwa.
Hayo yanakuja wakati ambao, uteuzi wa watiania wa udiwani umeshakamilika ukihusisha zaidi walioshinda kura za maoni na sasa wanachukua fomu kwa wasimamizi wasaidizi, kusubiri uteuzi wa mwisho Agosti 27, 2025.
Wasiwasi watawala
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa watiania aliyeongoza katika kura za maoni (jina linahifadhiwa), amesema pamoja na dalili kuonyesha walioongoza wana nafasi kubwa, lakini wasiwasi miongoni mwao bado ni mkubwa.
“Wasiwasi haupo kwangu pekee, hadi kwa familia yangu. Tumekuwa tukisali muda wote kumwomba Mungu awezeshe hili lipite. Nikisema wanasiasa karibu wengi huwa tunakumbwa na magonjwa ya shinikizo la damu, hii ndiyo sababu,” amesema.
Ameeleza pamoja na utayari wake wa kupokea matokeo yoyote kutoka katika vikao hivyo, kutoteuliwa kutamuumiza ingawa hakutamkatisha tamaa.
Mtiania mwingine jimbo moja mkoani Kagera, amesema hofu ni kwa wale wanaojijua kuwa na makandokando, hivyo wanajiona katika nafasi ndogo ya kuteuliwa kwa sababu chama kina mifumo inayowezesha kujua hali itakuwaje.
“Kwa mimi kwanza mzoefu bungeni, lakini sina makandokando, siwezi kuwa na wasiwasi. Kama sitateuliwa nitajua chama kimeona apatikane mtu mwingine, lakini siwezi kuwa na wasiwasi,” amesema.
Kwa wasiojipanga kwa matokeo tangu wanaomba ridhaa, ndiyo watakaopata hofu, laini wanaoelewa ukweli wa mambo haitawasumbua, kama inavyoelezwa na mtiania mwingine.
Ameeleza: “unapoomba ridhaa ya kugombea kwa chama chako, usiwe na majibu yako kwamba wewe ni bora na unastahili unachoomba.
“Wewe unaomba ridhaa ukikataliwa utasema umeonewa, si mmeomba na wenzio, sasa inabidi apatikane mmoja atakayepeperusha bendera, ukipewa, wewe ujue kuna mwenzio amenyimwa na ukinyimwa wewe ujue kuna mwenzio amepewa,” amesema.
Walioongoza kwa kura
Katika mchakato wa kura za maoni, wajumbe wa CCM, wamewapa uongozi wa kura makada 272 wanaowania ubunge wa majimbo Tanzania Bara na Zanzibar huku washindani wao wakisubiri vikao vinavyoanza leo.
Miongoni mwa walioshindwa, wamo naibu mawaziri wanne, akiwemo wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo aliyekuwa anawania Jimbo la Maswa Mashariki.
Wengine ni Jumanne Sagini wa Katiba na Sheria (Butiama), Cosato Chumi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mufindi Mjini) na Khamis Hamza Chilo wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira (Uzini).
Katika orodha, wamo pia waliokuwa wabunge wa Bunge la 12 zaidi ya 40, wakiwemo waliouweka kando ukuu wa mikoa – Daniel Chongolo (Makambako), Juma Homera (Namtumbo) na Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini).
Kwa waliopita wamo wawili kati ya waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu kupitia Chadema – Jesca Kishoa aliyeongoza katika Jimbo la Iramba Mashariki na Kunti Majala Jimbo la Chemba, huku wenzao tisa wakiwa katika kundi la wanaosubiri ngekewa kutoka kwenye vikao.
Wabunge hao ni Ester Bulaya, Esther Matiko, Hawa Mwaifunga, Cecilia Paresso na Nusrat Hanje.
Kwa mujibu wa matokeo ya kura za maoni katika Jimbo la Bunda Mjini, Bulaya ameshika nafasi ya tatu kwa kura 625, nyuma ya Mbunge wa Bunda Mjini aliyemaliza muda wake, Robert Maboto 2,545 na Kambarage Wasira aliyepata kura 2,032.
Kwa upande wa Hawa Mwaifunga aliyetiania katika Jimbo la Tabora Mjini naye ameshika nafasi ya tatu akipata kura 326, nyuma ya Shaaban Mrutu aliyeongoza kwa kura 6,612 na Kisamba Tambwe kura 395.
Nafasi ya tatu, imeshikwa pia na Matiko aliyekuwa katika Jimbo la Tarime Mjini, akipata kura 196, nyuma ya Michael Kembaki aliyeongoza kwa kura 1,568.
Felister Nyau alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 527, nyuma ya Moris Makori aliyeongoza kwa kupata kura 2,148 kisha Mbunge aliyemaliza muda wake, Profesa Patrick Ndakidemi akipata kura 627 na Salim Kikeke 491.
Katika Jimbo la Karatu, Cecilia Paresso ameshika nafasi ya pili akipata kura 1,341, nyuma ya Mbunge aliyemaliza muda wake, Daniel Awack aliyeongoza kwa kupata kura 7,884, huku Patrice Mattey 658, Pantaleo Paresso 142 na Shedrack Qamna 55.
Nusrat Hanje naye katika Jimbo la Ikungi Mashariki ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,918, nyuma ya Thomas Kitima aliyeongoza kwa kupata kura 2,100, huku aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Miraji Mtaturu akipata kura 1,111.
Wengine katika Jimbo hilo ni Emmanuel Ihonde kura 772 na Jonathan Njau 355.