Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Doyo wa NLD akishinda kuuza ‘mashangingi’ ya viongozi

Muktasari:

  • Hiyo ni moja ya ahadi iliyotolewa leo Jumapili Agosti 10,2025 na mgombea urais wa Chama Cha NLD Doyo Hassan Doyo aliyoitoa muda mfupi baada ya kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo kwenye Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Dodoma. "Siku ya kwanza nitakapoapishwa pale uwanja wa Taifa mara moja nakwenda kutangaza mnada wa kuuza magari yote ya Serikali yenye gharama kubwa ili fedha zikahudumie wananchi."

Hiyo ni moja ya ahadi iliyotolewa leo Jumapili Agosti 10, 2025 na mgombea urais wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo aliyoitoa muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuomba kugombea nafasi hiyo kwenye Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Mgombea huyo amesema chama chake kikishika dola, magari yote yatakayotumiwa na watumishi wa Serikali gharama yake haitazidi Sh30,000 milioni.

Doyo ambaye ameingia katika viunga vya ofisi za INEC akiwa amepanda bajaji, ameeleza namna chama hicho kilivyojipanga kuondoa matumizi yasiyo ya lazima katika Serikali, ili wanyonge wapate ahueni ya maisha.

Msafara wa Doyo umeshirikisha gari nne zilizowabeba wapambe na mgombea mwenza, Chausiku Khatibu Mohamed zikiongozwa na  pikipiki chache zilizokuwa zikipiga hodi na kuwasha taa.

"Mfano hili la ajira siendi kupunguza, bali nakwenda kumaliza kabisa suala la ukosefu wa ajira, haiwezekani tukawa na vijana wamemaliza vyuo vikuu zaidi ya miaka mitatu halafu hawana ajira," amesema Doyo.

Mgombea huyo amesisitiza kufuta tozo kwa wajawazito na kuondoa madai ya gharama wanazodaiwa ndugu wakati wakiwa na mgonjwa wao.

"Hili la kudai fedha ndipo mruhusu maiti iondoke hospitali ni aibu kubwa, nasema hivyo kwa sababu kaka yangu alipoteza maisha tukakuta tunadaiwa karibu Sh7 milioni ndipo tupewe mwili, tulichanga hadi Sh2 milioni lakini wakagoma, lazima nikomeshe hayo mambo," amesema.

Amesema Serikali atakayoongoza itakuwa na vipaumbele vinne ambavyo ni elimu, afya, ajira na miundombinu akisisitiza watajenga barabara ya njia nane Dar es Salaam hadi Chalinze ambako watajenga bandari kuenzi uongozi wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.