Dk Nchimbi aeleza watakavyoibadili Bukoba, Byabato asema...
Muktasari:
- Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amekamilisha ziara Mkoa wa Kagera na kuahidi miradi mbalimbali ya maendeleo
Bukoba. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewaeleza wananchi wa Bukoba, Mkoa wa Kagera watakachokifanya miaka mitano ijayo ikiwamo kujenga vituo vya afya vitatu na zahanati nne.
Pia, amesema kupitia ilani ya CCM ya 2025/30 itakayotekelezwa chini ya mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan imejipanga kujenga shule mbili za msingi na madarasa 131 pamoja na kujenga madarasa 26 ya shule za sekondari.
Amewahakikisha Manispaa ya Bukoba kwamba, watajenga mradi wa umeme wa kibeta na kuimarisha ujenzi wa jengo la abiria la kisasa na ujenzi wa soko la machinjioni.
Dk Nchimbi ametoa ahadi hizo leo Jumapili, Septemba 7, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu akimwombea kura mgombea urais Samia, wabunge na madiwani uliofanyika Bukoba Mjini.
Mkutano huo ni wa nne kwa siku ya leo katika mkoa huo, akianza na Ngara, Kyerwa na Bukoba Vijijini huku akitumia usafiri wa helikopta maarufu Chopa.
Katika mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi na wanachama wa CCM, Dk Nchimbi amesema Serikali imekusudia kujenga maduka ya kisasa maeneo ya stendi, Soko la Ndizi Kagondo, kujenga stendi ya mabasi Chakalabwa pamoja ujenzi wa masoko ya Rwamishenyi na Kashai.
Pia, amesema wataanzisha ujenzi wa kiwanda cha kusindika vyakula vya mifugo ili kukuza ufugaji wa mifugo katika mkoa kagera.
Amesema Rais Samia atakapopata ridhaa ya kuongoza katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025, atahakikisha wananchi wote wanapata huduma ya bima za afya kwa kuanza na makundi maalumu kama wajawazito, wazee, watoto na vijana kwa cha siku 100 za mwanzo.
"Serikali imekusudia kupambana na kuwasaidia wananchi wenye magonjwa sugu ambao hawana msaada kwa kuongeza watumishi wa afya kwenye vituo vya afya 5,000 na upande wa sekta ya elimu tumekusudia kuongeza walimu wa shule za msingi 7,000," amesema.
"Watanzania tuna haja ya kumchagua Rais Samia, wabunge na madiwani wa CCM kutokana na miradi mikubwa aliyoanzisha na atakayoanzisha. Jambo la msingi wananchi ni kuhakikisha wanatengeneza myororo Bukoba kwa kuchagua viongozi wa chama hiki," amesema.
Dk Nchimbi amehitimisha mikutano yake kanda ya ziwa, alianzia Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera. Kesho Jumatatu, Septemba 8, 202 ataanza mikoa ya Rukwa kisha Katavi.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amefurahishwa na kitendo cha kuona mbunge aliyemaliza muda wake Bukoba Mjini, Staphen Byabato akimuunga mkono katika hatua za kitafuta kura za CCM, hivyo ameomba wananchi kutambua unaweza usitumike leo ila ukatumika kesho.
Byabato ambaye amehudumu kwa miaka mitano jimbo hilo, alipojitosa tena kuwania kugombea, jina lake halikupenya kwenye vikao vya kamati.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Byabato amesema atahakikisha anakipambania chama ili kukiwezesha kushika dola ya kuongoza nchi.
"Naomba Dk Nchimbi, mimi bado mtoto na kijana, naomba chama changu kinipatie majukukumu mengine, kichama niko tayari kutumika," amesema.
Mgombea ubunge wa Bukoba Mjini, Jonhstoni Mtasingwa amesema sasa ni wakati wa kupiga kura na kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuivusha Bukoba kwa kuleta maendeleo.
Mtasingwa amesema wakimpatia ridhaa ya kuwa mbunge kwa kumchangua, atahakikisha anasimamia miradi yote iliyoanzishwa na itakayoletwa ili Manispaa ya Bukoba ibadilike kuwa kama Ulaya.
"Najua benki kuna fedha ya miradi mbalimbali zaidi ya Sh43 bilioni iliyoletwa, nitaisimamia mpaka ifaye kazi kama ilivyopangwa," amesema.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amesema kama wanahitaji Samia aweze kuwa Rais lazima wananchi washiriki kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
"Rais Samia ameleta miradi mikubwa, mtu akitaja kukuuliza kwanini uende kupiga kura, mwambie ameleta shule, bei ya Kahawa imepanda na kuna amani na mshikamano," amesema.
Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kagera, Nasir Kalamagi amesema katika uchaguzi popote duniani watu wanachagua maendeleo, kwa upande wa Tanzania kwenye uchaguzi huu yapo kwenye ilani ya chama ya 2025/2026.