Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mpango aagiza usalama mitandaoni uimarishwe kuelekea uchaguzi mkuu

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akiwasili katika viwanja vya shule ya Polisi Tanzania-Moshi,mkoani Kilimanjaro

Muktasari:

  • Dk Mpango ametoa maelekezo ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mkuu na hatimaye kufanyika uchaguzi Oktoba 29,2025.

Moshi. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza Jeshi la Polisi kufanya doria mtandaoni (cyber surveillance) kubaini na kuchambua machapisho, picha na video zenye viashiria vya uvunjifu wa sheria kuelekea uchaguzi mkuu, na kuchukua hatua za kisheria haraka.

Akifungua mkutano wa maofisa wakuu waandamizi wa polisi leo Jumatatu, Agosti 11, 2025 katika Shule ya Polisi Moshi, Dk Mpango amesema polisi washirikiane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine kwa kutumia Tehama kufuatilia taarifa za uchochezi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari. Pia amesisitiza ushirikiano na wadau wa uchaguzi kulinda amani na usalama wakati wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

"Zaidi ya hayo, kwa kutumia teknolojia za akili bandia (Artificial Intelligence - AI), baadhi ya watu wanaweza kusambaza picha au video za uongo za wagombea wa vyama vya siasa, jambo linaloweza kuleta madhara makubwa kwa amani na utulivu wa jamii.”

Pia, Dk Mpango amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano na wadau wote wa shughuli za uchaguzi kwa kuwa  wana wajibu wa kuhakikisha amani, utulivu na usalama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Amewataka polisi kuhakikisha mikutano ya kampeni inafanyika kwenye maeneo yaliyoruhusiwa na ndani ya muda uliopangwa; Kuzuia maandamano yasiyo na kibali ambayo yanaweza kusababisha vurugu, uharibifu wa mali, majeruhi au vifo ikiwamo kuimarisha ulinzi wa wagombea na viongozi wa vyama vya kisiasa, bila kujali vyama vyao au itikadi zao.

"Napenda kutoa wito pia kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kujichukulia sheria mkononi pale wanapoona ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, na badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki," amesema.

Dk Mpango pia amelitaka Jeshi la Polisi lishirikiane kwa karibu na wadau wengine wa uchaguzi, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama, ili kudhibiti vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura amesema hali ya usalama wa nchi ni shwari na kwamba jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

"Jeshi la Polisi liko imara na linaendelea kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa shwari wakati wote na haitamvumilia mtu yeyote au kikundi cha watu watakaojaribu kuvuruga amani ya nchi yetu kwa namna yeyote ile," amesema Wambura.

Pia, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mkoa huo upo salama na wananchi wanaendelea kufanya shughuli za kimaendeleo huku akiwaonya wanaotaka kuleta vurugu katika kipindi cha uchaguzi.

"Mkoa wa Kilimanjaro ni tulivu na tunataka uendelee kuwa tulivu wakati wa kampeni na wakati wa Uchaguzi Mkuu, wale wote waliojipanga kufanya vurugu katika mkoa huu wakati wa uchaguzi watafute mahali pa kwenda. Hatutaki vurugu, tunahitaji utulivu uendelee kudumu."

Mkutano huu umeandaliwa kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha na kudumisha usalama wa nchi, ili kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa hali ya juu.

Mkutano huo, ambao unatarajiwa kukamilika Agosti 15, 2025, unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo; “amani, utulivu na usalama: Kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025.”

Katika kipindi chote cha mkutano huu, mada mbalimbali zitawasilishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.

Mada hizo zitahusisha maeneo muhimu ya usalama wa raia na mali zao, kama yalivyoainishwa na sheria mbalimbali za nchi, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.