CUF kufungua kampeni Mwanza, mgombea ataja vipaumbele 12
Muktasari:
Miongoni wa vipaumbele 12 vya Chama cha Wananchi (CUF) ni huduma za matibabu na elimu zitakuwa bure, tatizo la ajira kwa vijana litapewa suluhisho la kudumu, wafanyakazi wataboreshewa maslahi kwa kufutwa kikokotoo na kupewa viwanja na masharti nafuu ya kupata magari, huku Watanzania wakipunguziwa mzigo wa kodi kwa kodi moja ya taifa.
Mwanza. Mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo ametaja vipaumbele 12 vya chama chake iwapo kitapewa ridhaa ya kuunda Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku akiahidi mageuzi makubwa katika sekta za afya, elimu, ajira na maslahi ya wafanyakazi.
Ametaja vipaumbele hivyo leo Jumamosi Agosti 30, 2025 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza, ambapo chama hicho kitazindua kampeni zake katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani hapa.
Gombo amesema CUF imeamua kuanzia Mwanza kwa sababu ni mkoa wa kimkakati kisiasa na kwamba yeye mwenyewe ni mzawa wa eneo hilo.
“Mwanza ni nyumbani kwetu mimi siyo mgeni, tumeamua kufungua kampeni zetu hapa kwa sababu huu ni mkoa wa kimkakati wa chama chetu katika safari ya kuingia Ikulu,” amesema Gombo.
Amesema kipaumbele cha kwanza kitakuwa kutoa huduma za afya bure kwa Watanzania wote, akibainisha kuwa mfumo wa bima ya afya uliopo umejaa mianya ya rushwa na ubadhilifu wa fedha.
Ameongeza kuwa elimu pia itatolewa bure kuanzia awali hadi chuo kikuu, akisema hakuna haja ya kuendelea na mfumo wa mikopo kwa sababu rasilimali zilizopo zinatosha kugharamia elimu hiyo.
Akieleza kuhusu ajira, mgombea huyo alisema changamoto hiyo siyo tatizo la kiasili bali imetengenezwa na mfumo wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba CUF ikishika dola, kila mwenye vyeti vya ajira atapata nafasi ya kazi.
“Wale wanaotaka kujiajiri watawezeshwa kupitia sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji. Hatutaki kusikia mtu anasema hana ajira kwa sababu Serikali itatengeneza mazingira ya kila mmoja kufanya kazi, ikiwemo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),” amesema Gombo.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya wafanyakazi, Gombo ameahidi kufuta kikokotoo cha mafao ya wastaafu na kila mmoja atalipwa fedha zake zote ili aamue mwenyewe namna ya kuzitumia.
“Kila mwajiriwa mpya atapatiwa hati ya kiwanja sambamba na masharti nafuu ya kupata magari ili kupunguza changamoto za makazi na maslahi. Lengo la CUF ni kuhakikisha wafanyakazi hawaingii kwenye rushwa na ubadhilifu kutokana na mazingira magumu ya maisha,” amesema Gombo.
Mbali na hayo, amesema Serikali ya CUF itatoa huduma za maji na umeme bure bila vikwazo vya kuunganishwa, itafuta mikopo inayowakandamiza watumishi wa umma hasa walimu na askari, na kuruhusu uraia pacha kwa watoto wenye mzazi mmoja Mtanzania, ingawa masharti yatawekwa kwa wanaotaka kushika nyadhifa za juu serikalini.
Ameongeza kuwa utitiri wa kodi unaowaumiza wafanyabiashara utapunguzwa kwa kuanzisha kodi moja ya taifa itakayokusanywa kwa mfumo wa kidijitali, na kwamba kutakuwepo na mpango maalum wa ujenzi wa nyumba kwenye miji mikubwa mitano ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
“Tutabadilisha utaratibu wa utoaji leseni za madini mbapo kila mwombaji atatakiwa kuthibitisha umiliki wa ardhi kabla ya kupewa leseni, lakini pia tutaifuta Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwa sababu imeshindwa kusimamia majukumu yake na kuingiza taifa kwenye migogoro ya mara kwa mara na wananchi,” amesema mgombea huyo.
Gombo ameahidi kuimarisha usalama wa wananchi ili kuondoa hofu ya kutekwa au kupotea kwa watu, akisisitiza kuwa vyombo vya dola vitarejea kwenye majukumu yake ya msingi ya kulinda haki na usalama wa raia.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa CUF, Husna Mohamed Abdallah amewaomba wakazi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kesho Agosti 31, 2025 kwenye mkutano rasmi wa kampeni utakaohudhuriwa pia na mmoja wa waasisi wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
“Nawaomba watu wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla mjitokeze kutuunga mkono. CUF haitaji msaada wa chama kingine, tunajitosheleza na tunaamini tunakwenda kushindana na kushinda,” amesema Husna.