Chaumma yaahidi mikopo ya nyumba vijijini
Muktasari:
Chaumma kimeahidi Serikali yake kwa kushirikiana na sekta binafsi itajenga nyumba bora vijijini na kuwapokesha wananchi watakaorejesha mkopo kwa miaka 50.
Dodoma. Mgombea mwenza urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amesema kutokana na wananchi wengi kuishi vijijini, wakishika dola watawajengea nyumba za kisasa na watazilipia kwa miaka 50.
Amesema haiwezekani wananchi kuendelea kuishi nyumba za tembe wakati Serikali ina uwezo wa kujenga nyumba na kuwakopesha wananchi, waishi maisha bora.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) takribani asilimia 60 hadi 70 ya Watanzania wanaishi vijijini.
Devotha ametoa ahadi hiyo leo Septemba 5, 2025 katika Kata ya Pahi, Jimbo la Kondoa Vijijini kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Nyumba za tembe zipo au hazipo? Kwani kuna Watanzania wanapenda kuishi maisha duni? Tupeni Chaumma, ilani yetu inaelekeza kwa kuwa wananchi wengi wanaishi vijijini, makazi yao ni duni na kipato chao ni kidogo, tukiingia madarakani tunataka maisha bora kwa kila Mtanzania," amesema.
Amesema Chaumma itaweka mkakati bora wa makazi ambao mwananchi atajengewa nyumba na kulipa kidogokidogo serikalini kwa miaka 50.
Utekelezaji wa mkakati huo amesema ni kupitia sekta binafsi.
Kuhusu uvamizi wa tembo, amesema kero hiyo wataipatia ufumbuzi na kifuta machozi kinachotolewa watakiongeza.
Amesema haiwezekani mwananchi aliyevamiwa na tembo kulipwa Sh500,000 wakati raia akiua tembo hutakiwa kulipa hadi Sh35 milioni ikiwa ni faini.
"Hapa tatizo lingine ni barabara, hakuna miundombinu. Barabara ni vumbi kila mahali, tupeni Chaumma tutashughulika na matatizo ya wananchi," amesema.
Asia Mohamed, mkazi wa Upiha jimboni humo aliyesikiliza sera za chama hicho ameeleza changamoto zilizopo ni kutumia gharama kubwa katika kilimo lakini vipato vya wananchi ni duni kutokana na kukosekana masoko.
Amesema mfumo wa stakabadhi ghalani unawanyonya na hawaukubali na hawakupata elimu kuhusu mfumo huo.
"Unaambiwa ufuta na mbaazi peleka ghalani ukishapeleka unaambiwa rudisha kwa sababu hakuna sehemu pa kuweka, mfumo huu wa stakabadhi ghalani siyo rafiki," amesema.
Abbas Kondo, mkazi wa Kondoa Vijijini amesema changamoto inayowakabili ni upungufu wa ardhi kutokana na Serikali kuitwaa.
"Vijana wengi wa Kondoa ajira yao ni kilimo, eneo la Pori la Mkungunero ambalo Serikali imelichukua kwetu limesababisha vijana kurandaranda bila ajira,” amesema na kuongeza: “Tatizo lingine ni uvamizi wa tembo, wananchi wanakanyagwa na wanyama na huruhusiwi kumuua. Ukimdhuru tembo unalipa hadi Sh35 milioni lakini yeye akikudhuru fidia ni Sh500,000," amesema.
Vilevile, amesema mikopo ya asilimia 10 kwa vijana wanawake na wenye ulemavu utoaji wake ni wa kusuasua.
"Tunaomba Chaumma kama itashida, Serikali iyafanyie kazi mambo hayo, hatuna majibu na changamoto zinazotukumba. Wakati huu wa kampeni ndiyo tunawaona viongozi wakitutembelea," amesema.