Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yapuliza kipenga Tanganyika packers

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza uzinduzi wa kishindo wa kampeni zake za urais kitaifa kesho katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amewataka viongozi, makada, wachungaji, wasanii na wananchi kufurika kusikiliza sera za Samia Suluhu Hassan na Emmanuel Nchimbi.

Dar es Salaam. Joto la kisiasa nchini limeanza kupamba moto baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza rasmi kesho Alhamisi, Agosti 28, 2025 kitazindua kampeni zake za urais katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja huku vyama vya upinzani vikiwa kwenye hatua za ndani za kupanga mikakati yake kukikabili chama hicho tawala, jambo linalofanya CCM kuwa chama cha kwanza kupiga kipenga cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Katika mkutano na wanahabari uliofanyika leo Jumatano Agosti 27, 2025 viwanjani hapo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi ameweka wazi chama hicho kimejiandaa kikamilifu kwa hafla hiyo, akiwataka viongozi wote wa kitaifa na mikoa, wabunge, madiwani, makada, wanachama wa kawaida, na wafuasi wake kuungana na chama chao kushuhudia kile alichokiita ‘kampeni ya kishindo haijawahi kutokea.’

“Kesho Tanganyika Packers patashuhudiwa historia itakayoandikwa kwa wino wa kijani. Tunawaalika viongozi wote wa CCM kutoka kila kona ya nchi, kuanzia wajumbe wa Halmashauri Kuu, sekretarieti, wabunge, madiwani, viongozi wa mashina, matawi, wanachama wa kawaida na wadau wote," amesema na kuongeza:

"Huu ni uzinduzi wa kitaifa wa kampeni za urais, tunataka kila mmoja awepo kushuhudia sera na maono mapya ya chama chetu, usipange kukosa kuwa sehemu ya historia hii," amesema Kihongosi.


Amwaga sifa kwa Samia na Nchimbi

Akizungumzia wagombea walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, Kihongosi amewamwagia sifa kemkem akiwaita viongozi bora wenye maono thabiti ya kuliongoza Taifa.

“Ukisoma wasifu wa Samia Suluhu Hassan na Emmanuel Nchimbi utaona jinsi CCM ilivyo na wagombea wenye sifa na uzoefu mkubwa serikalini na ndani ya chama. Wawili hawa wakipewa ridhaa ya wananchi wataendelea kulipeleka Taifa letu mbele kwa kasi mpya,” amesema.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa chama ambaye ameteuliwa hivi karibuni katika wadhifa huo, wagombea hao watawasilisha sera zao kesho viwanjani hapo, ambapo wananchi watapata nafasi ya kusikiliza moja kwa moja maono ya viongozi wao watarajiwa ili wafanye maamuzi sahihi siku ya uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.


Makundi yote ya kijamii yaitwa kushiriki

Katika mkutano huo, Kihongosi hakusita kutoa mwaliko kwa makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki katika hafla hiyo kubwa.

“Tunataka Tanganyika Packers kesho ifurike, kiasi ambacho hakijawahi kutokea. Tunawaalika watu wa makundi yote, wasanii, wanahabari, viongozi wa dini, wenye ulemavu na makundi yote kwa ujumla, wasanii wa muziki na maigizo, viongozi wa michezo, wafanyabiashara, wakulima, wavuvi, vijana, kina mama, na hata wazee," amesema na kuongeza:

"Hii ni siku ya historia ambapo chama chetu kinazindua kampeni zake rasmi tufurike wote kesho Kawe si ya kuikosa," amesema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM, uzinduzi huo utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii nyota wa muziki wa kizazi kipya na vikundi vya sanaa asilia, sambamba na hotuba kuu ya mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan atakayeambatana  na mgombea mwenza wake, Emmanuel Nchimbi.


Atafsiri kauli mbiu ya utu na haki

Aidha, Kihongosi amesema uzinduzi wa kampeni za mwaka huu unakuja na kauli mbiu mpya yenye kuhamasisha mshikamano wa kitaifa unaojali utu na maendeleo jumuishi.

Amesema chama chake, CCM kimejiandaa kufanya kampeni za kujali utu, amani na mshikamano wa Taifa akisisitiza kuwa kauli za matusi, dhihaka na uvunjifu wa amani hazitakuwepo.

“Tumejipanga kwa maandalizi ya kipekee. Kauli mbiu yetu ya utu na haki tunasonga mbele itakuwa dira ya safari mpya ya Tanzania. Kampeni hizi hazitakuwa za kawaida. Zitakuwa za kishindo zenye ujumbe thabiti wa maendeleo, mshikamano na uadilifu,” amesema.


Viwanja vya Tanganyika Packers vyajaa shamrashamra

Wakati huohuo, maandalizi katika viwanja vya Tanganyika Packers yamepamba moto. Leo yameshuhudiwa maandalizi ya mahema makubwa yakisimikwa, mapambo yenye rangi za kijani na njano kila kona, na shamrashamra za makada wa chama hicho.

Aidha, mabango yenye picha za Rais Samia na Nchimbi yamewekwa kila upande wa viwanja hivyo, yakibeba ujumbe wa mshikamano na maendeleo.


Hali ya ulinzi na usalama yaimarishwa

Mapema asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amefika viwanjani na kutoa wito wa amani akiweka wazi kuwa serikali ya mkoa imejipanga kulinda amani ndani ya jiji hilo kipindi cha uchaguzi.

"Jeshi letu la Polisi litakuwepo kila mahali kuimarisha ulinzi katika eneo hili ili kuhakikisha mkutano huu mkubwa wa kisiasa unafanyika bila dosari wala uvunjifu wa amani," amesema.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Dar es Salaam amewataka Viongozi wa chama hicho kudumisha amani kwa kuepuka kauli za ubaguzi, uchochezi na kusisitiza uchaguzi ufanyike kwa amani ndani ya vyama vyote, akiweka wazi kuwa serikali ya mkoa imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani jijini humo.

"Nitoe wito kwa wana CCM mliopo hapa na vyama vingine vitakavyofanya mikutano yao jijini hapa, zingatieni sheria na kanuni kama zilivyopangwa, serikali ya mkoa haitamfumbia macho mtu yeyote atakayejaribu kuharibu amani na kuvuruga shughuli za maendeleo za wananchi wakati wote wa uchaguzi," amesema mkuu huyo wa mkoa.