ACT-Wazalendo: Hatutateua mwingine, Mpina anatosha
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Omar Issa Shaaban amesema chama hicho hakiwezi kuteua mgombea mwingine zaidi ya Luhaga Mpina kuwanaia urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Shaaban amesema hayo leo Jumatano, Agosti 27, 2025 makao mkuu ya chama hicho, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu sakata la Mpina kuenguliwa katika na Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Mzizi wa yote hayo ni hatua ya Monalisa kukiandikia chama chake, kisha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akipinga uteuzi wa Mpina, kwa kurejea kifungu cha 16(4)i, iii na iv, cha Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama toleo la mwaka 2015.
Kwa mujibu wa kifungu cha 16(4)(i) “Wagombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa. Awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama."
Aidha kifungu cha 16(4)(ii), kinasema wagombea urais/viongozi wa chama ngazi ya Taifa, “Awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya mgombea wa chama.”
16(4)(iii) inasema, “Awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea kwa kufuata utaratatibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.
16(4)(iv) “awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.”
Katika barua yake, Monalisa alidai Mpina anakosa sifa zote hizo, kwani alijiunga na chama hicho, Agosti 5 na Agosti 6, mkutano mkuu ukampitisha kuwa mgombea wa urais.