Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afya turufu ya watia nia Ada-Tadea, UMD na TLP

Muktasari:

  • Rwamugira ataja mambo hayo kuwa ni afya na elimu bure, ulinzi, utawala bora na uchumi imara, na kusisitiza kila Mtanzania lazima afanye kazi itakayomuingizia kipato.

Dodoma. Mchakato wa uchukuaji fomu za kugombea kiti cha urais umeingia siku ya tatu leo, huku vyama tisa vikiwa tayari vimeshawasilisha majina ya wagombea wao katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Hata hivyo, wakati uchukuaji fomu ukiendelea, kila mgombea amekuwa akitumia fursa hiyo kueleza kipaumbele chake kuelekea kwenye kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Miongoni mwa hoja zinazojitokeza mara kwa mara ni sekta ya afya, ambayo imeendelea kutamalaki katika hotuba za wagombea hao.

Karibu kila chama kinachowania nafasi hiyo kimeweka afya kuwa sehemu ya ajenda kuu za kampeni zao, ikiwasilishwa kama ahadi muhimu kuelekea katika uchaguzi huo.

Hata vyama vilivyochukua fomu katika siku mbili zilizopita vimesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za afya, vikibainisha kuwa ni moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbele endapo vitapata ridhaa ya kuongoza nchi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na INEC, leo Jumatatu Agosti 11, 2025, uchukuaji fomu za kuwania nafasi ya urais ulikuwa zamu ya vyama vya Ada-Tadea, UMD na TLP.

Wagombea wa vyama hivyo na wapambe wao waliwasili katika viunga vya ofisi za INEC jijini Dodoma na kukabidhiwa fomu. Kwa hatua ya awali, vinatakiwa kuanza mchakamchaka wa kusaka wadhamini mikoani kabla ya kuzirejesha fomu hizo.

Mwananchi imewashuhudia wagombea wote wanaofika, hupokelewa katika viwanja vya jengo la Tume na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, ambaye huwakaribisha na kuwaelekeza kabla ya barua zao kukaguliwa.

Kwa mujibu wa Kailima, hatua hiyo ikikamilika bila kasoro na barua ikikidhi vigezo, mgombea hukabidhiwa fomu ya kuomba kugombea nafasi hiyo.

Baada ya hatua hiyo, mgombea anatakiwa aende kusaka wadhamini katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Akikamilisha, anatakiwa kuirejesha fomu hiyo ambayo itahakikiwa na kulipiwa dhamana ya Sh1 milioni kwa mujibu wa sheria.

Kanuni ya 35(1) inaeleza kuwa kila mgombea wa urais ataweka dhamana ya kiasi kinachoainishwa na kanuni, kwa sasa kikiwa ni Sh1 milioni.

Kwa mujibu wa kifungu cha 20(4) (c), dhamana hiyo itataifishwa ikiwa mgombea atajitoa baada ya siku ya uteuzi au kupata chini ya asilimia 10 ya kura halali.


Mgombea urais wa TLP

Mgombea urais wa chama cha TLP, Yustas Rwamugira, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu, ametaja ajenda nne kuu wakati wa kampeni zake, ikiwamo afya.

Rwamugira amesema ni aibu familia kushindwa kujitokeza kuchukua maiti zao hospitalini, kisa hazina fedha za kulipia gharama za matibabu.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele akimkabidhi fomu ya uteuzi kwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira leo Jumatatu Agosti 11, 2025 kwenye ofisi za tume zilizopo Njedengwa Jijini Dodoma.

“Hali hii ndiyo inachangia maiti kukuta zikizikwa na manispaa. Kwetu sisi hatutakubali hali kama hiyo ijitokeze,” amesema Rwamugira.

Akizungumzia elimu bure, ulinzi, utawala bora na uchumi imara, mgombea huyo amesisitiza kila Mtanzania kufanya kazi kwa lengo la kujipatia kipato, huku akiahidi kuimarisha ulinzi na kuheshimu sheria za nchi.

Kuhusu elimu, ameahidi kufundisha ufundi kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu. Pia ametangaza mpango wa bima ya afya kuanzia kwa waendesha pikipiki na watumishi wa umma, huku wengine wakipata matibabu bure endapo hawana ajira rasmi.


UMD yaja na kodi, sera ya majimbo

Mgombea urais wa UMD, Mwajuma Mirambo, akiwa na mgombea mwenza, Mashabi Alawi Haji, amesema Serikali atakayoiunda itajikita katika uchumi wa mtu mmoja mmoja, huku kodi ikiwa kipaumbele cha kwanza.

Amesema kuwa, iwapo wananchi hawatalipa kodi, basi hawataweza kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.

Mirambo ametaja vipaumbele vyao kuwa ni afya, maji, elimu na miundombinu, huku akisisitiza sera ya majimbo.

Amesema hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji na manufaa ya rasilimali kwa wananchi. Ameongeza kuwa huduma za kujifungua zinapaswa kuwa bure, akisema uhuru bila haki haukamiliki.


Turufu ya Ada-Tadea

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, mgombea wa urais wa chama cha Ada-Tadea, Georges Bussungu, aliyefuatana na mgombea mwenza wake, Ali Makame Issa, amesema chama chake kitajikita katika matumizi ya Akili Unde (AI), uchumi na “mapinduzi ya njano” ili kuifikisha Tanzania kwenye maendeleo yanayokusudiwa.

Amesema rasilimali za nchi lazima zigawiwe kwa usawa na kila Mtanzania anastahili kunufaika.

Bussungu amesisitiza mapinduzi ya teknolojia na fikra katika kilimo na uchumi, akibainisha kuwa hawaendi kuongoza nchi maskini.

Vyama ambavyo vimeshachukua fomu hizo ni CCM, Makini, AAFP, NRA, NLD na UPDP. Kwa mujibu wa ratiba ya INEC, kesho ni zamu ya vyama vya chama cha Umma (Chaumma), chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Kijamii (CCK).