MSD MPYA: Safari ya ufanisi, mageuzi na uhakika wa upatikanaji dawa kwa Watanzania

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai.
Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ambayo ni sehemu ya kipindi cha mageuzi katika taasisi nyingi za umma, Bohari ya Dawa (MSD) imepiga hatua kubwa kutoka kuwa taasisi ya ugavi wa bidhaa za afya pekee, hadi kuwa kielelezo cha mafanikio ya mageuzi ya kimuundo, kiutendaji, na kiuwekezaji ndani ya sekta ya umma.
Ni safari ya kujijenga upya kwa msingi wa uwajibikaji, ubunifu, na ufanisi iliyoibua taasisi ambayo sasa ni miongoni mwa taasisi bora zaidi za ugavi barani Afrika. Jukumu la MSD ni kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya ni endelevu zikiwa na ubora unaohitajika na kwa gharama nafuu.

Ghala la MSD, Mbeya.
Muhimu ni kuhakikisha uwepo wa bidhaa ili kuistawisha jamii ambayo ndiyo nguvu kazi ya Taifa. Katika mahojiano maalumu na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, picha halisi ya taasisi inayokua na kusonga mbele, taasisi inayojifunza, inayofanya mageuzi, na kukidhi mahitaji halisi ya Watanzania iliwekwa wazi. Na hii ni sehemu ya mahojiano hayo:-
Swali: Miaka mitatu iliyopita Rais Samia alielekeza MSD kufanya mageuzi ya kiundeshaji ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji ili ijiendeshe kibiashara zaidi. Agizo hilo limefanyiwa kazi kwa kiasi gani?
Tukai: Ni kweli. Tarehe 30 Machi 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, alielekeza kufanyika kwa mageuzi makubwa ndani ya MSD. Lengo lilikuwa moja: kuifanya MSD iendane na mahitaji ya sasa, na iwe taasisi ya kibiashara yenye ufanisi mkubwa katika wa utoaji huduma.
Hatua ya kufanya mageuzi, hatukufanya wenyewe bali tulishirikiana na Wizara ya Afya, wataalamu elekezi na sehemu kubwa ya wafanyakazi wetu. Hatujaenda tu kubadili mfumo, tumeamua kujijenga upya. Tumebadili fikra, mifumo, na utendaji.
Katika maazimio ya kujijenga upya, tulikaa na kukubaliana kuhusu mambo makuu sita; awali ya yote ni kuwa na msuli wa kifedha ili kuimeza falsafa ya kibiashara. Pili, kuwa na muundo unaoendana na wakati wa kibiashara. Tatu, kuongeza ufanisi. Nne, kuboresha hali za wafanyakazi.

Muonekano wa ndani wa ghala la MSD.
Tano, kujenga uwezo wao na wa taasisi ili kuwekeza kwenye utawala bora, weledi na mazingira sahihi kwa taasisi kutimiza majukumu yake. Sita, kutumia ubunifu wa kidijiti kuboresha upatikanaji wa bidhaa, MSD imeamua kifanya Tehama kuwa mhimili wake mkuu wa mnyororo wa ugavi.
Tuelezee mageuzi katika tarakimu hususan kwenye majukumu yenu ya kisheria
Tukai: Katika miaka hii minne, kwenye upatikanaji wa bidhaa, tumesogea kutoka asilimia 42 hadi 74 kwa wastani. Lakini mapato kwa mwaka yameongezeka kutoka Sh 278 bilioni kwa mwaka 2021/22 hadi Sh 551 bilioni kwa mwaka 2023/24, ikiwa na ongezeko mara mbili ya lile la awali, huku matarajio yetu ni kuvuka Sh 600 bilioni kwa mwaka huu wa fedha (2025/26). MSD ni moja ya taasisi zinazojiendesha kwa mapato yake, bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
Maana yake biashara inafanyika na Serikali inaendelea kutoa fedha kwa hospitali kuweza kumudu kununua dawa kutoka kwetu. Thamani ya MSD kiujumla pia imeongezeka.
Maeneo gani ya kiutendaji ambayo MSD imeyafanya kuwa ya kibiashara kwa asilimia mia moja?
Tukai: Swali zuri sana. MSD imeamua kuchagua kuyaendesha kibiashara majukumu mawili kati ya manne huku mawili mengine yakibaki katika utaratibu wa kawaida.
Tumeamua kuhakikisha uzalishaji na usambazaji unaingia katika mfumo wa biashara kwa asilimia mia moja ambapo mpaka sasa tumeanzisha kampuni tanzu ya MSD Medipharm Manufacturing Company Ltd ili kusimamia eneo la uzalishaji pamoja na kuingia ubia na wawekezaji wengine.
Kampuni hiyo ina bodi yake, uongozi wake na imeshaanza kuwa na miradi yake. Kampuni hiyo ndiyo inayosimamia miradi ya uzalishaji mipira ya mikononi (glovu) kupitia kiwanda cha Idofi kilichopo Makambako, mkoani Njombe na uzalishaji wa barakoa kupitia kiwanda cha barakoa kilichopo Dar es Salaam.
Vile vile, Medipharm imeingia ubia wa uzalishaji wa bidhaa za afya wenye thamani ya Sh 183.3 bilioni na kampuni ya Rotabiogen ya nchini Misri ambapo Medipharm itahodhi asilimia 26.
Moja ya mafanikio makubwa ya kampuni hiyo tanzu ni kusaidia uzalishaji katika kiwanda cha dawa cha Keko na mpango uliopo ni kuendelea kuingia ubia na viwanda vingine ili iweze kukua kama kampuni inayojitegemea.
Kwenye usambazaji (ugavi), MSD inahudumia zaidi ya vituo 8,700 vya afya nchini. Kwa uwezo mkubwa wa magari, maghala, na rasilimali watu, MSD ni miongoni mwa kampuni kubwa zaidi za ugavi kwa sekta ya umma Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Watumishi wa Kiwanda cha Mipira ya Mikono cha MSD, Idofi, Makambako wakishughulikia bidhaa hiyo.
Tunayo magari. Tunayo miundombinu. Kwa nini tusipanue huduma hata kwenye usambazaji wa chanjo za mifugo au bidhaa zisizo na madhara? Tunawaza kwenda nje ya dawa tu. Na huko ndiko tunakokuangalia zaidi.
Kiashiria gani kingine mnachokiona kuwa ni sehemu ya ukuaji wenu tangu muanze kufanya mageuzi?
Tukai: Idadi ya wataalam imeongezeka kwa kasi kutoka maafisa ununuzi na famasia hadi wahandisi wa vifaa tiba, madaktari, wauguzi na wataalamu wa maabara. Hili limeboresha ufanisi wa utoaji hudu¬ma, ikiwemo usahihi wa vipimo na ubora wa bidhaa zinazopatikana.
Lakini kwenye uhifadhi tumepanua uwezo wetu. Mwaka 2022, MSD ilikuwa na uwezo wa kutunza dawa katika eneo la sqm 36,000 pekee. Leo hii, imeongeza zaidi ya sqm 12,000, ikiwa na mkakati wa kufikia sqm 100,000 ili kuhifadhi dawa za kutosha kwa miezi mitano kwa maandalizi ya dharura.
Ujenzi wa maghala ya kisasa mawili mkani Dodoma na Mtwara umekamilika, na kwa sasa wanaweka miundombinu (racks) ya kuhifadhia bidhaa hizo kama inavyohitajika ghalani.
Aidha, ghala la Dodoma lenye ukubwa wa mita za mraba 7,800 linategemewa kuwa kitovu cha ugavi kwa kanda nzima ya Kati na kuhudumia pia Kanda za Iringa, Dodoma, Tabora, Kagera, Mwanza na Kanda mpya itakayojengwa Chato.
Nini mpango wa siku za usoni kwa MSD ambayo tayari imeshavaa joho la kibiashara?
Tukai: MSD inapendekeza kuanzishwa kwa mfuko wa uwekezaji (investment fund) kwa taasisi za kibiashara zilizo chini ya msajili wa hazina kama vile MSD, ambazo zinaweza kuzalisha mapato lakini bado zinahitaji mtaji (capital injection) au fedha za muda mfupi za kutimiza majukumu yake kama vile ununuzi wa kimkakati ili kuchangia vilivyo katika uchumi na maendeleo ya jamii kuliko kukimbilia kwenye mabenki ambayo yana viwango vikubwa vya riba.
Kama mnavyofahamu, kila mwaka tuna siku ya gawio ambapo taasisi za umma huwasilisha gawio la mapato kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia tafrija maalumu inayoandaliwa na msajili wa hazina… mapendekezo yetu ni kwamba katika lile gawio, basi asilimia 30 ibaki kama ‘catalytic fund’ ya kuchochea ukuaji wa taasisi za umma za kibiashara.
Kwa mfano tukikusanya trilioni moja na kuamua kubakiza asilimia 30 ya fedha kama investment fund tutaweza kuharakisha ukuaji wa taasisi kama zetu badala ya kwenda kwenye mlolongo mrefu wa mikopo.
Kwa ujumla na kwa muhtasari, unaizungumziaje safari ya mageuzi ya MSD ndani ya miaka minne?
Tukai: Mageuzi yoyote yale huanza na uongozi thabiti na dira. Maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ya kuifumua MSD, na utekelezaji wa maagizo hayo uliosimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ndizo nyenzo kuu zilizotutoa hapa tulipo.
Utekelezaji wa maagizo ya viongozi wetu yalisimamiwa na kuratibiwa vizuri sana chini ya uongozi wa Wizara ya Afya, na wizara nyingine Pamoja na taasisi na vyombo vingine vya serikali Pamoja na wadau wa maendeleo.
Kila tunachoona, ni matunda ya ushirikishwaji wa waau ndani nan je ya Serikali, kwa sasa naewza kusema kwamba MSD leo ni zaidi ya bohari ni injini ya uhai, ni moyo wa huduma za afya, na ni kiashiria cha namna taasisi za umma zinavyoweza kufanyika kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.
Kwa uongozi madhubuti, mageuzi makini, na maono yaliyo wazi MSD imejijenga upya na sasa iko tayari kuipeleka Tanzania katika hatua mpya ya uhakika wa dawa, kwa wakati, na kwa kila Mtanzania. Tunapojenga MSD mpya, tunajenga Taifa lenye afya, lenye matumaini, na lenye hadhi.