Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu dawa kukosekana hospitalini hii hapa

Muktasari:

  • Kumekuwa na malalamiko ya wananchi kwa baadhi ya nyakati kwamba wanakosa dawa hospitalini huku lawama ikiwa kwa Serikali au bohari ya dawa.

Tabora. Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tabora, Peter Sungusia ametaja sababu za kukosekana kwa baadhi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma.

Akizungumza na watumishi wa vituo vya kutolea huduma za afya leo Alhamis mjini Tabora leo Mei Mosi, 2025, Sungusia amesema sababu kubwa ni kushindwa kufanya maoteo sahihi ya dawa.

Amesema kama watumishi wa afya watafanya maoteo sahihi, changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo, hasa wakati huu ambao Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, itaisha.

Amesema ingawa Bohari Kuu ya Dawa ina akiba ya kutosha, bado changamoto ya ukosefu wa dawa katika vituo inaendelea kujitokeza kutokana na maoteo yasiyo sahihi kutoka kwa wahusika vituoni.

“Kwa sasa bohari imejaa dawa, hadi tunafikiria kujenga maghala mapya kwa ajili ya kuhifadhi. Hali hii inatufanya tujiulize, kama dawa zipo nyingi, kwa nini vituo vinakosa dawa? Jibu lipo kwenye maoteo yasiyo sahihi. Hili ni jambo linalojirudia mara kwa mara na tunashauri kuwe na majukwaa ya mara kwa mara ya kujadili na kuboresha namna ya kuotea dawa,” amesema Sungusia.

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Honoratha Rutatinisibwa amekiri kuwapo kwa changamoto ya madeni katika vituo vya kutolea huduma, lakini akaeleza kuwa huduma za bohari ya dawa zimeimarika kwa kiasi kikubwa.

“Ni kweli tuna changamoto ya vituo kuwa na madeni makubwa kwa MSD. Hata hivyo, tunapaswa kuangalia namna bora ya kuyapunguza au kuyamaliza kabisa, huku tukiendelea kutoa huduma kwa wananchi bila kuyumbishwa,” amesema Dk Rutatinisibwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedith Katwale amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh13 bilioni katika sekta ya afya mkoani Tabora ndani ya kipindi cha miaka minne, ikilinganishwa na Sh4 bilioni zilizowekezwa kabla ya hapo.

“Kwa uwekezaji huu mkubwa, hatupaswi kuwa na malalamiko ya ukosefu wa dawa wala huduma hafifu. Huduma zinazotolewa ni lazima ziwe bora na stahiki kwa wananchi,” amesisitiza Katwale.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Bukene, Sela Mwinuka amekiri kuwa moja ya changamoto waliyoipitia ni makosa katika kufanya maoteo ya dawa.

Hata hivyo amesema juhudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuboresha utendaji kwa weledi unaotakiwa.

“Tumejipanga kuhakikisha tunafanya maoteo kwa usahihi kulingana na mahitaji halisi ya kituo ili kuondoa kabisa tatizo la uhaba wa dawa,” amesema Mwinuka.

Kwa upande wake, mtaalamu wa maabara, Leokadia Humbi amesema pamoja na changamoto ya maoteo, mfumo wa kuagiza dawa pia unachangia matatizo hayo kwa kufuta oda za dawa bila taarifa kwa watumiaji.

“Unaweza kuwa umeingiza oda na ukaamini kila kitu kiko sawa, lakini unakuja kugundua baadaye kuwa mfumo umefuta oda hiyo bila taarifa. Wakati huo muda umeshapita na unaishia kuagiza dawa chache sana,” amesema Humbi.