Hatuwezi kumaliza Malaria bila kuwa na msukumo thabiti

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Msukumo unahitajika kwani tuna kila sababu ya kuhakikisha tunatokomeza malaria
Uimara wa uongozi haupimwi katika nyakati njema, bali katika nyakati ambazo unatakiwa kukabiliana na changamoto zinazoweza kufifisha mafanikio yaliyopatikana kutokana na kazi kubwa iliyofanyika. Mojawapo ya changamoto kubwa inayoikabili bara la Afrika ni afya na ustawi wa watu wake. Na ni dhahiri kuwa, malaria ni moja ya kiini cha changamoto hizo.
Inaelezwa kuwa, malaria bado inasababisha vifo vya zaidi ya watu laki tano barani Afrika kila mwaka, huku wengi kati ya hao wakiwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Rais wa Jamhuri ya Botswana, Wakili Duma Gideon Boko akizungumza wakati akikabidhiwa uenyekiti wa ALMA katika mkutano wa AU uliofanyika Februari, 2025.
Zaidi ya asilimia 95 ya vifo hivyo hutokea kutokana na jamii kukosa mbinu za kujikinga na ugonjwa huo, kupima afya mara kwa mara na kukosekana kwa matibabu sahihi. Hii inasababisha ugumu katika kufikia lengo la Umoja wa Afrika la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030, huku visa vya malaria vikiongezeka.
Changamoto hii inasababishwa pia na kupunguzwa kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili wakubwa, ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa hivi karibuni kwa misaada ya kigeni ya Marekani ambayo kihistoria imekuwa msaidizi mkuu wa kutokomeza malaria kupitia Mpango wa Rais wa Malaria (PMI) na Mfuko wa Dunia (Global Fund). Kusitishwa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kumerudisha nyuma juhudi za kupambana na malaria zilizosababishwa na kupungua kwa bidhaa muhimu za malaria katika nchi nyingi hasa za Afrika.
Wataalamu wanakadiria kuwa, kama fedha za misaada zitaendelea kukosekana, Afrika itashuhudia visa milioni 112 na vifo 280,000 zaidi vya malaria kuanzia mwaka 2027 hadi 2029. Aidha, ufadhili mdogo wa Global Fund utasababisha visa kufikia milioni 137 na vifo 337,000 vya malaria na hivyo kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika miongo iliyopita. Kwa mwenendo huu, hatutapoteza tu nguvu ya mapambano dhidi ya malaria bali pia tutarudisha nyuma maendeleo yaliyofikiwa katika karne iliyopita.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kuzindua ofisi za ALMA jijini Dar es Salaam mwaka 2009.
Na huo ndiyo ukweli kuhusu malaria, bila marekebisho ya haraka, changamoto hii itaongezeka na hivyo kuhatarisha vifo vya watoto zaidi na vikwazo kwa afya, uchumi na utulivu wa kikanda. Hatutakiwi kulichukulia hili kama jambo la kawaida bali ikiwa tuna nia ya dhati ya kulinda kizazi kijacho, mapambano dhidi ya malaria lazima yaendelee bila kuathiriwa na kitu chochote. Tanzania na Botswana zimeonyesha jinsi uongozi unavyopaswa kuwa katika juhudi za kudhibiti malaria.
Tanzania imejikita katika kupanua juhudi hizi katika ngazi ya jamii, kuunganisha huduma za malaria katika huduma za afya ya msingi na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa wakati. Botswana, ambayo sasa inakaribia kutokomeza ugonjwa huo, ina mifumo dhabiti ya ufuatiliaji, mwitikio wa haraka wa mlipuko na udhibiti wa vimelea vya malaria unaolenga katika maeneo yenye hatari kubwa. Nchi zote mbili zinaendelea kuonyesha kwamba kutokana na uwepo wa uongozi thabiti na mikakati imara, maendeleo yanawezekana.
Changamoto zilizopo katika kukabiliana na malaria Afrika
Katika bara zima la Afrika, mapambano dhidi ya malaria yanakumbana na changamoto kadhaa zinazotishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi.
Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya malaria. Mabadiliko ya hali ya hewa na matukio mengine kama hayo yanasababisha kueneza maambukizi katika maeneo mengine na kurefusha misimu ya malaria. Wakati huohuo, upungufu wa fedha unatishia maendeleo ya mapambano haya. Afrika inahitaji nyongeza ya Dola bilioni 5.2 kila mwaka kutekeleza kikamilifu mikakati ya kitaifa ya kupambana na malaria.

Watoa huduma za afya wa kijamii wakionyesha matumizi ya vyandarua vilivyowekwa dawa nchini Nigeria. Picha na US PMI
Licha ya kutengwa kwa bajeti na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo, upungufu wa fedha bado unaongezeka. Kupunguzwa kwa misaada ya kimaendeleo kunakwamisha programu za malaria, kuchelewesha miradi na kusababisha uhaba wa dawa na vifaa kinga na tiba.
Pia tunakabiliwa na changamoto ya ukinzani wa kibaolojia. Viuatilifu vinashindwa tena kuwaathiri mbu na vimelea vya malaria vinaonyesha dalili za kustahimili dawa. Ukinzani huu wa kibaologia unadhoofisha ufanisi wa dawa na kinga hivyo kuwepo kwa uhitaji wa haraka wa jitihajada mpya.
Migogoro ya kibinadamu inayoendelea ni changamoto nyingine katika utoaji wa huduma za malaria. Katika mazingira haya magumu, mwendelezo wa huduma unakuwa mgumu na hatari ya milipuko ya malaria inaongezeka zaidi.
Kuendelea kupambana na changamoto bila kuchoka
Licha ya kupitia changamoto hizi, maendeleo katika kupambana na malaria yanawezekana. Nchi zinaendelea kuongeza zana za udhibiti wa malaria ikiwa ni pamoja na vyandarua vyenye dawa na kunyunyizia dawa ukoko ndani ya nyumba. Vyandarua hivi pia vinasaidia kupambana na ukinzani wa viuatilifu katika maeneo yenye maambukizi makubwa na hivyo kusababisha kupungua kwa malaria.
Tumeshuhudia kwamba dawa za kuzuia malaria na chanjo vinaleta matumaini mapya. Matumizi ya dawa za kemikali za kuzuia malaria yanaendelea kuongezeka jambo linalosaidia kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi.

Mtoa huduma za afya wa kijamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara akimfanyia vipimo vya malaria mwananchi. Picha na Abbie Trayler-Smith - Malaria No More UK
Uchunguzi wa mapema na matibabu yanaendelea kuokoa maisha. Watoa huduma za afya wa kijamii mara nyingi ndiyo wamekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma. Hivyo kuongeza nguvu kazi hii na kuboresha minyororo ya usambazaji wa bidhaa tiba bado ni muhimu. Juhudi za kuwalinda wale ambao wanakabiliwa na hatari zaidi kama vile wakinamama wajawazito zinaimarika huku utumiaji wa dawa kinga wakati wa ujauzito (IPTp) husaidia kuwalinda mama na mtoto.
Juhudi hizi zinafanya kazi, lakini ni lazima ziboreshwe na kuungwa mkono na viongozi, ushirikishwaji wa jamii na uwekezaji thabiti.
Msukumo mkubwa unahitajika ili kutokomeza malaria
Kutokomeza malaria hakutafanikiwa pasi na kuwepo juhudi za ziada. Inahitaji msukumo thabiti katika nyanja zote ili kuhakikisha matokeo yanapatikana kwa haraka na kwa viwango.
Lazima tuhakikishe upatikanaji endelevu wa kinga, utambuzi na matibabu. Vyandarua vilivyowekwa dawa, vipimo vya haraka na dawa bora huokoa maisha. Ni lazima kuwepo kwa mifumo bora ya utendaji kazi, kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake na kuhakikisha uwajibikaji katika ngazi zote.
Maendeleo yanategemea uratibu sahihi pamoja na maamuzi yanayotokana na data. Nchi zinatakiwa kutumia data sahihi katika utekelezaji wa afua za malaria. Hii inahitaji uwekezaji katika mifumo ya taarifa na uongozi wenye maono.
Mbinu moja haitafanya kazi. Ndiyo maana ushirikiano wa kimataifa katika utekelezaji wa afua za malaria ni muhimu sana. Wilaya zenye maambukizi tofauti ya malaria zinahitaji masuluhisho tofauti, na ni lazima tubadilike ipasavyo.

Mtoa huduma za afya wa kijamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara akimfanyia vipimo vya malaria mwananchi. Picha na Abbie Trayler-Smith - Malaria No More UK
Uhamasishaji wa rasilimali za ndani ni msingi wa maendeleo endelevu. Mafanikio ya muda mrefu yanategemea nchi kuweka kipaumbele kwa ugonjwa wa malaria ndani ya bajeti zake na mikakati ya ufadhili pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi.
Tunahitaji juhudi za jamii nzima. Serikali haiwezi kufanya hivyo peke yake. Mafanikio yanategemea kushirikisha kila sekta, iwe ya afya, fedha, elimu, kilimo, mazingira, na kila sehemu ya jamii, wakiwemo wabunge, jumuiya za kiraia, vijana, sekta binafsi na viongozi wa imani. Kila mtu ana jukumu lake. Kutokomeza malaria kunaanza na sisi sote!
Hakuna mkakati utakaofanikiwa bila kuwa na watu wanaofanya kazi kwa bidii. Watoa huduma za afya wa kijamii, ambao mara nyingi ndiyo sehemu ya kwanza ya utoaji wa huduma, ni lazima wapatiwe mafunzo, wawezeshwe ili wawe na vifaa bora na waungwe mkono ili kuendeleza kazi yao ya kuokoa maisha.
Ni lazima tujumuishe malaria katika utoaji wa huduma za afya kwa mapana zaidi, kuingiza malaria katika huduma za wajawazito, programu za afya shuleni na huduma za afya za jamii ili kufanya afua ziweze kupatikana kwa ufanisi zaidi. Zana pekee haziwezi kumaliza malaria isipokuwa zikiungwa mkono na dhamira ya kisiasa na uwajibikaji.
Jukwaa la Afrika la uongozi na uwajibikaji
Muungano wa Viongozi wa Afrika Dhidi ya Malaria (The African Leaders Malaria Alliance, ALMA) uliundwa ili kukidhi mahitaji haya. ALMA ilianzishwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ikiwa na maono ya kuwaleta pamoja wakuu wa nchi na Serikali ili kugeuza dhamira za kisiasa kuwa hatua endelevu, kupambana na malaria kuwa kipaumbele chao na kuunganisha bara zima katika malengo ya pamoja.

Mtoa huduma za afya wa kijamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara akifanyia vipimo vya malaria maabara. Picha na Abbie Trayler-Smith - Malaria No More UK
Tanzania ni mwenyeji wa makao makuu ya ALMA, kama sehemu ya uongozi na dhamira ya kudumu ya kuendeleza ushirikiano wa afya na kikanda katika bara la Afrika.
Kwa miaka mingi, uongozi wa ALMA umekuwa ukizunguka katika nchi zote, ikionyesha wajibu wa Afrika nzima. Leo, kanda ya SADC inaongoza, huku Rais Wakili Duma Gideon Boko wa Botswana akiwa mwenyekiti wake.
Jukumu la ALMA katika kuongeza kasi ya kupambana na malaria
Kama jukwaa linaloongozwa na wakuu wa nchi za Afrika, ALMA huzipa nchi zana zinazohitaji ili kupata matokeo. Zana hizi husaidia nchi kufuatilia maendeleo, kutambua vikwazo na kuchukua hatua haraka ili kuleta matokeo. Wizara za Afya hutumia zana hizi katika kufanya maamuzi na kuelekeza matumizi ya rasilimali kwa ufanisi zaidi. Zana hizi pia huwapa wananchi sautikwa kutoa maoni kuhusu huduma za afya ili kuimarisha uwajibikaji kuanzia ngazi za chini.
ALMA inakuza mtazamo wa jamii nzima, kuwashirikisha wabunge, mashirika ya kiraia na vijana katika juhudi za kitaifa. Kampeni ya ‘Zero Malaria Starts with Me’ imesaidia kuongeza ufahamu wa malaria katika jamii. ALMA pia imefadhili mifuko 9 ya kupambana na malaria, ambayo imekusanya zaidi ya dola za Marekani milioni 125 na kuzindua Kundi la Vijana katika nchi 16 ili kuwawezesha viongozi vijana.
ALMA inaunga mkono wazalishaji wa ndani, mageuzi ya udhibiti na upatanishi wa kikanda ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Maamuzi haya yatasaidiakuimarisha uwezo wa Afrika wa kukabiliana na matishio ya afya katika siku zijazo.
Upatikanaji wa ubunifu na uzalishaji wa ndani
Afrika haijapungukiwa na ubunifu. Lakini mara nyingi, kuna pengo kati ya kile kilichopo sehemu zingine za dunia na kile kinachopatikana ndani ya bara la Afrika. Kuziba pengo hilo kunamaanisha kuharakisha ufikiaji wa zana mpya na kuwekeza katika uzalishaji wa ndani katika bara zima.
Mkakati wa ubunifu katika kupambana na malaria una nguvu zaidi kuliko hapo awali. Zana mpya ni pamoja na vyandarua vyenye dawa, huduma bora za vipimo, chanjo na dawa zinazofaa zaidi. Pia kuna masuala ya teknolojia kama vile dawa za kufukiza (spatial repellents), kingamwili za monokloni n.k.
Lakini ubunifu ni muhimu tu ikiwa utawafikia watu wanaouhitaji. Hata hivyo, nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto za muda mrefu kama sheria ngumu za usajili kwa ajili ya ununuzi na michakato ya upatikanaji wa vyeti vya ithibati vya bidhaa tiba. Vyote hivi huchelewesha ufikiaji wa huduma hizo.

Mtaalamu wa afya akipulizia dawa ukoko kwenye nyumba kwa ajili ya kuua mbu waenezao malaria. Picha na Brant Stewart RTI
Chini ya asilimia 2 ya bidhaa za malaria zinatengenezwa barani Afrika. Kuongeza uzalishaji wa ndani si hiari tena bali ni muhimu. Tanzania tayari inaonyesha kwamba hili linawezekana. Kupitia uwekezaji wa ndani kama ule wa kiwanda cha A-to-Z, unazalisha vyandarua vyenye dawa, hivyo basi kupunguza gharama na kujenga uwezo wa nchi na bara la Afrika.
Kinachohitajika kwa sasa ni kasi na ushirikiano mkubwa ili kuoanisha michakato ya udhibiti. Mwitikio endelevu wa malaria lazima uwe wa kujitegemea. Afrika lazima iondoke kutoka kuwa mlaji mkubwa zaidi duniani hadi kuwa mzalishaji mkubwa.
Je, tutashinda au tutashindwa?
Bado tunaweza kushinda pambano hili. Nchini Tanzania, maambukizi ya malaria yamepungua kutoka asilimia 18.1 hadi 8.1 katika kipindi cha muongo mmoja tu. Botswana inakaribia hali ya kutokuwa na malaria kabisa. Haya si mafanikio pekee, bali yanaonyesha kile kinachowezekana kwa uongozi thabiti, na hatua endelevu.
Kuondoa malaria kutawezeakana tu kupitia kujitoa, uratibu thabiti na upatikanaji wa haraka wa zana mpya. Tunajua kinachofanya kazi, sasa ni lazima tukifanye haraka, kwa ubora na kwa pamoja.
Hitimisho: Dhamira ya Afrika kuelekea msukumo thabiti
Kama Marais wa Tanzania na Botswana, tunasisitiza dhamira yetu ya pamoja ya kukomesha ugonjwa wa malaria, sio tu katika nchi zetu, bali Afrika nzima.
Hii sio safari ambayo Serikali zinaweza kutembea peke yake. Inahitaji ushirikiano wa pamoja kutoka kila sekta, ikijumuisha viongozi wa imani, vijana, wanasayansi, wahudumu wa afya na sekta binafsi. Ukweli ni kwamba Afrika haijawahi kujitosheleza katika juhudi za kupambana na malaria, lakini sasa uwezo tunao, mifumo tunayo na nia tunayo. Tunachohitaji ni msukumo thabiti ili kumaliza kazi hii.
Msukumo huu huanza kwa kuziba pengo la ufadhili. Ufadhili wa kimataifa ni muhimu na ni lazima tuwe na msaada wa kifedha kutoka Mfuko wa Dunia. Upatikanaji wa rasilimali za ndani ni muhimu ikijumuisha mifuko ya kitaifa ya kutokomeza malaria. Majukwaa haya yanawezesha rasilimali za ndani na kuweka malaria kama kipaumbele katika ajenda za kisiasa. Malaria lazima pia iunganishwe katika ufadhili wa afya, kuanzia huduma za msingi hadi juhudi za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Lazima pia tuhakikishe kunakuwa na ubunifu. Ni lazima nchi ziondoe urasimu, zipunguze gharama na kuimarisha mifumo ya udhibiti ili zana mpya ziwafikie wale wanaozihitaji zaidi.
Tanzania na Botswana ziko tayari kuongoza msukumo huo. Tumejitolea kuharakisha michakato, kuhamasisha washirika wetu na kuwa na uongozi unaoleta matokeo. Tunawaalika wengine Afrika na ulimwenguni, kuungana nasi. Hatua inayofuata katika mapambano dhidi ya malaria ni nzuri. Wacha hatua hii iwe ya vitendo, umoja na ushindi.
Imeandikwa na:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Botswana, Wakili Duma Gideon Boko