Prime
Wanasayansi wataja mbinu kutokomeza malaria Tanzania

Wakati leo dunia ikiadhimisha Siku ya Malaria, imeelezwa kuwa takribani asilimia 86.2 ya watu nchini (sawa na watu milioni 58) wako kwenye hatari ya kupata malaria, huku watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito wakiwa kwenye hatari kubwa zaidi.
Kwa wastani, kiwango cha maambukizi ya malaria nchini Tanzania ni asilimia 8.1, lakini kiwango hicho hutofautiana sana kati ya eneo moja na jingine, kikianzia chini ya asilimia moja hadi zaidi ya asilimia 24.
Katikati ya hali hii, wanasayansi na watafiti wa masuala ya afya wanataja njia mbalimbali zinazoweza kukabili ugonjwa huu na hata kuutokomeza.
Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk Nico Govella anasema kama jitihada zikichukuliwa malaria inaweza kutokomezwa kabisa.
Anasema kwa sasa hapa nchini moja ya mbinu zinazotumika kukabiliana na malaria, ni kutumia chandarua na watu kwenda kutibiwa hospitalini.
Lakini anasema kuna baadhi ya mbu ambao huwang'ata watu wanapokuwa nje nyakati za jioni na upo ushahidi kuna maambukizi mengi hutokea kabla watu hawajaingia ndani ya nyumba zao.
"Hivyo pamoja na matumizi ya vyandarua, kunahitajika njia nyingine mbadala ili kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwemo kukabiliana na mbu wakiwa bado katika mazalia yao," anasema Dk Govela.
Anasema kwa Tanzania kuna kiwanda kinachotengeneza dawa ya kuua mazalia hayo ya mbu, lakini matumizi ya dawa pekee haitoshi, kuna mazalia ya mbu ambayo huhitajika kuondolewa kwa kuondoa maji yaliyotuama, kuweka mitaro safi na kufukia mashimo.
"Suala la kukabiliana na malaria halitakiwi kuachwa kwa wizara pekee, kila mmoja katika eneo lake anapaswa awajibike. Watu wa mipango miji pia wanatakiwa wahusike kuona wanafanya nini katika kuboresha miundombinu," anasema.
Dk Govela anasema jamii pia inatakiwa kushiriki kuondoa mazingira yote ambayo yanaweza kutengeneza mazalia ya mbu.
Pia anasema wanawajibika katika kuboresha makazi yao na mazingira yanayowazunguka, ikiwemo kufyeka nyasi, kuondoa makopo, matairi na kuweka mazingira safi
"Kwa Dar es Salaam utafiti tuliofanya miaka ya nyuma kidogo, ulionyesha kuwa watu walioboresha mazingira yao kwa kuweka hata dari na kuziba juu majumbani waliweza kupambana na malaria kwa asilimia 60," anasema.
Uwekezaji katika mbinu mpya
Wanasayansi na watafiti wanatoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika mbinu ya kutokomeza mazalia ya mbu kama mkakati muhimu katika udhibiti wa malaria nchini.
Licha ya historia yake ndefu na mafanikio yaliyothibitishwa, mbinu hiyo ya kudhibiti mbu inayolenga mazalia kabla hayajawa mbu waliokomaa, mara nyingi haifanyiki kutokana na ukosefu wa fedha na changamoto za kubaini na kutibu maeneo ya kuzaliana kwa mbu.
Dk Fredros Okumu, mchunguzi mkuu wa utafiti kuhusu utokomezaji wa mazalia ya mbu, anasema juhudi zao zilizaa mapendekezo saba muhimu kama mkakati wa kudhibiti malaria na magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu barani Afrika.
“Kuongezwa kwa uwekezaji wa kifedha na msaada wa kimuundo ndani ya mifumo ya afya ya umma, utambuzi wa WHO (Shirika la Afya Duniani) kama hatua muhimu ya utekelezaji, kujua vyanzo na matumizi ya viuadudu dhidi ya mabuu pamoja na usimamizi wa mazingira kama vile kukausha maeneo ya maji yaliyotuama ambayo ni mazalia ya mbu,” anasema Okumu.
Anasema mbinu hiyo ni tofauti na matumizi ya vyandarua vyenye dawa au upuliziaji wa dawa ndani ya nyumba, vinavyolenga mbu waliokomaa, kwani utokomezaji mazalia hutoa suluhisho la muda mrefu kwa kuvuruga mzunguko wa maisha ya mbu mapema zaidi.
Pamoja na hayo, walipendekeza kutoa kipaumbele kwa utokomezaji katika sera za kudhibiti malaria, akisema viongozi wa afya duniani wanaweza kupiga hatua kubwa katika kupunguza wagonjwa wa malaria na hatimaye kutokomeza ugonjwa huo.
Mtafiti mwingine, Issa Mshani anasema kuna umuhimu wa kuboresha zana za uchunguzi ili kuimarisha vita dhidi ya malaria.
“Zana za sasa za kugundua malaria, huenda zisitoshe kwa kutambua hali halisi. Wakati wagonjwa wengine hawagunduliwi, jamii hubaki kwenye hatari na rasilimali zinaweza zisifikishwe maeneo yanayoyahitaji zaidi.
“Lakini kwa kutumia zana za uchunguzi zenye uwezo mkubwa wa kugundua malaria, wataalamu wa afya wanaweza kuunda ramani sahihi zaidi za malaria, kuhakikisha hatua za kudhibiti zinaelekezwa ipasavyo,” anasema.
Mshani anasema aliwahi kufanya utafiti katika vijiji 35 vya wilaya za Ulanga na Kilombero kusini-mashariki mwa Tanzania kati ya mwaka 2022 na 2023, akilinganisha mbinu tatu za uchunguzi, vipimo vya haraka (RDTs), hadubini na upimaji wa mnyororo wa vinasaba (qPCR).
Matokeo yalionyesha tofauti kubwa katika ufanisi wa zana hizi. Ingawa RDTs na hadubini ni nafuu na hutumika sana, mara nyingi zilishindwa kugundua wagonjwa, hasa katika maeneo yenye maambukizi ya chini ya malaria.
Katika baadhi ya vijiji, thamani ya utabiri chanya wa vipimo hivi ilishuka hadi chini ya asilimia 20.
“Matokeo yale yanatuonyesha haja ya kuwa na zana za uchunguzi rahisi kutumia, za bei nafuu na zenye uwezo mkubwa kwa ajili ya maeneo yaliyoathirika na malaria,’’ anapendekeza.
Malaria Tanzania
Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyoitwa kitaalamu kwa jina la “plasmodium” ambavyo husambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kung’atwa na mbu jike aina ya “anopheles” mwenye vimelea.
Mikoa kadhaa, ikiwemo Songwe, Njombe, Arusha, Manyara na Kilimanjaro ina kiwango cha maambukizi ya malaria kilicho chini ya asilimia moja, wakati mikoa ya kusini na kaskazini-magharibi mwa nchi ikiwa na kiwango cha maambukizi ya malaria kilicho juu ya asilimia 20.
Akizungumzia hali ya ugonjwa wa malaria nchini, Mkuu wa Program Kutoka Wizara ya Afya, Dk Samwel Lazaro anasema takwimu za utafiti wa viashiria vya malaria katika jamii wa mwaka 2022, kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kimepungua kwa asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Anaitaja mikoa mitano inayoongoza kwa maambukizi ni Tabora kwa asilimia 23.4, Mtwara asilimia 19.7, Kagera (17.5) Shinyanga (15.6) na Mara (15.1).
Hata hivyo, anasema idadi ya mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria, imepungua kutoka mikoa 14 mwaka 2015 hadi kufikia mikoa nane mwaka 2023.
Dk Lazaro anasema mikoa yenye kiwango cha chini kabisa cha maambukizi ya malaria (chini ya asilimia moja) imeongezeka kutoka mikoa sita mwaka 2017 hadi kufikia mikoa 9 mwaka 2022.
Anaitaja mikoa hiyo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, na Singida.
"Wagonjwa waliothibitika kuwa na malaria wamepungua kwa asilimia 45 kutoka wagonjwa milioni 6.0 mwaka 2020 hadi kufikia wagonjwa milioni 3.3 kwa mwaka 2024," anasema Dk Lazaro.
Pamoja na hayo, Dk Lazaro ameyataja makundi yanayoathirika zaidi na malaria wakiwemo wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, na watu wanaoishi na VVU.