Vifukuza mbu hivi ni salama?

Leo ni siku ya kimataifa ya Malaria Duniani, chini ya mwavuli wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Siku hii huadhimishwa Aprili 25 ya kila mwaka.
Kaulimbiu ya mwaka huu 2025 inasema “Tuimalize Malaria; Wazia tena, Wekeza tena, Anzisha tena”.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa kila baada ya dakika moja, kifo kimoja hutokea duniani kwasababu ya malaria. Na vifo vingi vinatokea katika ukanda wa Afrika, Tanzania ikiwamo.
Katika kuunga mkono siku hii, leo nitawapa ufahamu wa vifukuza mbu. Aina ya kwanza ni zile za kupaka mwilini zinazoingilia uwezo wa mbu kumvamia mtu na kumuuma.
Kundi la pili ni dawa za kupulizia ambazo si za kupaka mwilini, bali zipo kama gesi au kimiminika ambazo zikipuliziwa au kunyunyiziwa huweza kumfukuza mbu.
Lakini pia zinaweza kuainishwa kama vifukuza mbu vya asili na vifukuza mbu vya kutengenezwa viwandani.
Kwa kifupi, vifukuza mbu ambavyo baadhi huwa na kemikali na nyingine huwa vinapachikwa katika umeme ni salama kwa matumizi ya binadamu na vimeidhinishwa kutumika.
Kitu cha msingi cha kuzingatia ni kusoma na kuelewa mwongozo wa kutumia kifaa hicho uliopo katika chapa. Hakikisha unanunua bidhaa katika maduka ya dawa yanayotambulika na Serikali.
Au kama ni vya kuuzwa madukani hakikisha ina chapa za mamlaka za udhibiti bidhaa, ikiwamo TBS.
Vilevile ukinunua bidhaa hizo hakikisha vipo ndani ya muda wa kutengenezwa na kutumika. Zingatia maelekezo yote ya tahadhari na usalama kabla ya kutumia.
Kwa upande wa dawa za kupaka zilizo katika mfumo wa kimiminika, yaani mafuta au losheni hubeba aina fulani za kemikali ambayo hutoa harufu inayomfanya mbu kuikimbia.
Kemikali zinazotumika humu ni salama kwa afya ya ngozi. Na hakuna ushahidi mpaka sasa kuwa zinasababisha saratani ya ngozi.
Madhara machache ya kuvumilika hutokea kwa baadhi ya watumiaji, ikiwamo kupata mzio, harufu, kikohozi na chafya kwa muda mfupi.
Kitabibu inashauriwa dawa za kupaka kutumika katika maeneo ya ngozi iliyowazi isipokuwa mdomoni, machoni na eneo lenye jeraha la wazi, michubuko na ngozi inayowasha
Dawa za kupaka zinapatikana katika michanganyiko na viwango tofauti. Uchunguzi umeonyesha kuwa dawa iliyo na kiambata cha DEET (N,N-diethyl-m-toluamide), picaridin au IR3535 ni bora zaidi.
Vilevile zina athari za muda mrefu kufukuza mbu kuliko dawa za asili zinazotumia vitu vilivyopo katika mimea, kama vile minti, mikaratusi na pareto.
Daima angalia chapa na utumie dawa ya kufukuza kulingana na maagizo ya mtengenezaji. Kwanza pima kwa kupaka kidogo kuona kama itakuletea mzio katika ngozi. Usitumie kupita kiasi, tumia tu ya kutosha kufunika ngozi na nguo zilizoachwa wazi.
Dawa hizi za kupaka ili ziwe na ufanisi, zinahitaji kupakwa juu ya kitu kingine. Mfano usianze kupaka kifukuza mbu kisha uanze kupaka mafuta ya kawaida au vipodozi.
Hakikisha unapopaka kusiwepo na majimaji au jasho, hii inapunguza ufanisi wake.
Kwa upande wake, dawa za kupulizia au kunyunyizia hewani au katika mazingira hutoa kemikali ambazo hufukuza mbu.Kemikali zinazotawanywa angani kumfukuza mbu ni salama kiafya.
Zina kemikali, kama vile metofluthrin, transfluthrin, prallethrin na D- au D-trans allerthrin ambazo zimeonyeshwa kuwa na ufanisi katika kuwadhibiti mbu.
Kwa matumizi ya ndani, hakikisha chumba kina hewa ya kutosha. Weka mbali na watoto, vyakula na malisho ya wanyama.
Vifukuza mbu vipo pia katika taa, feni za majumbani, mishumaa, mataulo, mablanketi na rangi za kuta.
Vifaa hivi vingelikuwa na madhara kiafya basi vingeishapigwa maarufu. Muhimu kuepuka ununuzi wa bidhaa za mtandaoni na mtaani zinazouzwa kiholela.