Hatifungani ya CRDB Al Barakah Sukuk ni uwekezaji wa uhakika wenye faida hadi asilimia 12
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua hatifungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Sharia Benki ya CRDB, Abdul Mohamed na viongozi wa dini.
Kama ubunifu ungekuwa thawabu, hivi tunavyozungumza Benki ya CRDB ingekuwa na kiti chake peponi, kwa namna jamii zinazoishi kwa miongozo ya imani zao wanavyofurahia mifumo ya kifedha hivi sasa.
Itakumbukwa kuwa Agosti 9, 2025, Benki ya CRDB ilizindua hatifungani ya CRDB Al Barakah Sukuk, ambayo inalenga kuongeza huduma jumuishi za kifedha na kurahisisha uwekezaji kwenye miradi ya kijamii yenye kuzingatia maadili hapa nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza katika uzinduzi wa hatifungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Hatifungani hiyo inalenga kukusanya kiasi cha Sh 30 bilioni na Dola za Marekani milioni 5, huku ikitarajiwa kuwa na ongezeko la mauzo ya ziada ya hatifungani hiyo hadi kufikia Sh 40 bilioni na Dola za Marekani milioni 7 kwa pamoja.
Hii inaifanya CRDB Al Barakah Sukuk kuwa hatifungani kubwa zaidi inayozingatia Sharia iliyowahi kutolewa na taasisi ya kifedha nchini na kuwa hatifungani ya kwanza ya unayoweza kuwekeza kwa Shilingi ya Kitanzania au Dola ya Marekani katika soko la hisa nchini.
CRDB Al Barakah Sukuk ni hatifungani ya tatu chini ya Mpango wa Hatifungani wa miaka mitano wa Benki ya CRDB wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300, uliopitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), baada ya uzinduzi wa kihistoria wa Kijani Bond na Samia Infrastructure Bond.
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati wa uzinduzi wa hati fungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Sherehe rasmi ya uzinduzi ilifanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, ilihudhuriwa na Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye aliipongeza Benki ya CRDB kwa kujitolea kwake katika kukuza ujumuishi wa huduma za fedha na uwekezaji unaozingatia imani ya dini.
“CRDB Al Barakah Sukuk ni hatua ya mapinduzi katika kufungua masoko ya mitaji kwa wananchi wote nchini. ikiwezesha kushiriki kwa wale ambao awali walikuwa wameachwa nyuma kwa sababu ya imani zao za kidini, kupitia kuundwa kwa njia ya uwekezaji inayozingatia misingi ya Sharia, Watanzania wote hivi sasa watanufaika na uwekezaji unaozinhatia imani zao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika uzinduzi wa hatifungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Hii siyo tu ushindi kwa ujumuishi wa kifedha, bali pia ushindi kwa maendeleo ya kimaadili. Nina imani kwamba hatifungani hii itazidi matarajio, kama ilivyokuwa kwa uwekezaji wa kihistoria wa hatifungani za CRDB zilizopita,” alisema Dk Jakaya Mrisho Kikwete.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, alisema: “Hatifungani hii inaakisi imani yetu kwamba fedha lazima ziwe jumuishi na zikidhi mahitaji ya kila Mtanzania.
Kupitia CRDB Al Barakah Sukuk, tunafungua milango kwa watu wengi zaidi kushiriki kwenye masoko ya mitaji bila kuathiri imani au maadili yao. Pia ni kichocheo cha kufungua mitaji kwa ajili ya miradi ya kimaadili, endelevu na yenye manufaa kwa jamii.”
Nsekela alibainisha kuwa mapato yatakayopatikana kupitia hatifungani hiyo yatatumika kuwezesha miradi yenye kuzingatia maadili na isiyo na madhara kwa ustawi wa binadamu, kwa kuzingatia misingi ya Sharia, ikiwemo sekta kama afya, kilimo halali, elimu na uzalishaji rafiki kwa mazingira.
“Hatifungani hii inatoa faida shindani ya asilimia 12 kwa mwaka kwa wawekezaji wanaotumia Shilingi ya Kitanzania na asilimia 6 kwa mwaka kwa wawekezaji wanaotumia Dola ya Marekani, huku mgao wa faida ukitolewa kila robo mwaka.
Kiwango cha chini cha uwekezaji kinaanzia Sh 500,000 au Dola za Kimarekani 1,000, jambo linaloifanya ipatikane kwa urahisi kwa wawekezaji wadogo, Watanzania waishio ughaibuni na taasisi mbalimbali. Dirisha la uwekezaji limefunguliwa kwa mwezi mmoja na linatarajiwa kufungwa Septemba 12, 2025,” alifafanua.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete akiwasili katika hoteli ya Johari Rotana akiongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto), Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir (wa pili kulia), Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila (kulia) kuelekea katika hafla ya uzinduzi wa hatifungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk.
Wakati mwekezaji mkuu wa hatifungani hii akiwa ni kampuni ya British International Investment (BII), Balozi Mkazi wa Uingereza nchini, Mheshimiwa Marianne Young, alieleza kuwa ufadhili huu unaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya Uingereza na Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Sharia ya Benki hiyo, Abdul Van Mohammed, wote walisisitiza umuhimu wa dhamana hii kutoka katika mtazamo wa fedha zinazozingatia imani za dini.
“Hatifungani hii inajenga daraja kati ya imani na fedha. Inaonyesha kwa kina dhamira ya Benki ya CRDB katika kuthamini miongozo ya Sharia na uwekezaji wenye kuzingatia maadili,” walisema.
Muziki wenye mahadhi ya pwani ulikuwa sehemu ya burudani katika hafla ya uzinduzi wa hatifungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk.
Katika taarifa ya pamoja, CPA Nicodemus Mkama, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), na Peter Nalitolela, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), walisema:
“Uzinduzi na uorodheshwaji wa CRDB Al Barakah Sukuk ni hatua kubwa inayochangia utanuaji fursa za masoko ya mitaji nchini Tanzania.”
Faida za hatifungani ya CRDB Al Barakah Sukuk
Sukuk, inayojulikana pia kama hatifungani za Kiislamu, imekuwa mbadala maarufu wa uwekezaji katika masoko ya hisa na mitaji duniani. Tofauti na hatifungani za kawaida ambapo mwekezaji huwa mdai (creditor) wa kampuni au Serikali, na hupokea riba ya kudumu hadi hatifungani hiyo inapoiva, Sukuk inatoa hadhi ya umiliki katika mali au miradi ya uwekezaji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori akizungumza katika uzinduzi wa hatifungani ya kwanza inayofuata misingi ya Sharia ya CRDB Al Barakah Sukuk katika hafla iliyofanyika Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.
Kwa kuwekeza katika CRDB Al Barakah Sukuk, mwekezaji/mteja atapata usalama wa fedha katika kipindi chote cha uwekezaji, uhakika wa faida inayovutia katika kipindi kizima cha hatifungani, utulivu wa moyo kwa kuwekeza katika njia inayofuata misingi ya Sharia, mteja /mwekezaji hatakatwa kodi kwenye kuponi atakazowekewa, anaweza kuombea mkopo halikadhalika anaweza kuuza hatifungani yake katika soko la hisa la Dar es Salaam kwa kutegemea na uhitaji wa soko.
Jambo lingine ambalo watu wengi hawafahamu au wana mawazo tofauti na ilivyo ni kwamba Al Barakah Sukuk ni kwa ajili ya kila mwekezaji, si kwa waislamu pekee. Inaweza kuwa ni mtu binafsi au shirika (isipokuwa, biashara zisizozingatia misingi ya Sharia), bila ubaguzi wa dini wala rangi.