Doweicare yaipatia Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma taulo za watoto za Sh65 milioni

Waziri wa Afya, Dk Jenista Mhagama (katikati) Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa SUNDA Group Tanzania, Andy Liu (kulia) wakiwa wamebeba sampuli ya taulo za watoto zilizokabidhishwa kwenye Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma na Kampuni ya Doweicare.
Katika kuonyesha namna gani wanaigusa mioyo ya wakazi wa Dodoma, Doweicare Technology Company Limited, mzalishaji wa bidhaa za afya na usafi wa mwili, imeendelea kuthibitisha kuwa mafanikio ya kibiashara yanaweza kwenda sambamba na urudishaji kwa jamii.
Juni 9, 2025, kampuni hiyo ilitoa msaada wa taulo za watoto wachanga zenye thamani ya Sh 65 milioni kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake endelevu ya kuimarisha afya na utu wa familia za Kitanzania.
Msaada huo pia umeelekezwa kwenda katika halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa akiwemo Waziri wa Afya, Dk Jenista Mhagama na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, pamoja na viongozi wengine wa hospitali, wadau wa jamii, waandishi wa habari na wafanyakazi wa Doweicare.
Tukio hilo lilikuwa zaidi ya hafla ya kawaida likiakisi maadhimisho ya kampuni inayotanguliza maadili na maono ya kusaidia jamii mbele.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Afya, Dk Jenista Mhagama amesema msaada huo ni sehemu ya wadau hao kuzingatia taratibu za Serikali zilizowekwa.
“Kampuni ya Doweicare Technology Limited mmeonyesha moyo wa huruma, uzalendo, na uwajibikaji wa kijamii,” amesema Dk Jenista.
Amesema Kampuni hiyo imetoa jumla ya paketi 110,000 zenye nepi mbili kuwasaidia kinamama wote wanaojifungua kwenye hospitali za mkoa wa Dodoma. Nepi hizi ni kwa watoto wachanga na makadirio ya msaada huu ni kuwanufaisha wamama wote watakaokuwa wanajifungua.

Waziri wa Afya, Dk Jenista Mhagama akihutubia wananchi waliohudhuria tukio la makabidhiano ya taulo za watoto kwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma na Kampuni ya Doweicare.
“Natoa wito kwa kampuni nyingine kuiga mfano huu wa kutoa kwa jamii kwa moyo wa upendo, hasa kwa makundi yenye uhitaji mkubwa kama watoto, wazee na mama wajawazito.
Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau wote wa ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha huduma bora za afya zinaimarishwa na zinamfikia kila Mtanzania,” amesema Dk Jenista.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma unaendelea kutoa ushirikiano kwa kadri itakavyohitajika ili kuhakikisha Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto zinaimarika.
“Ninatoa shukurani za dhati kwa Mkurugenzi wa Doweicare Technology pamoja na timu yake kwa kuwakumbuka wananchi wa Mkoa wa Dodoma; nami niahidi taulo hizi za watoto wachanga zitafikishwa kwa walengwa wote kama ilivyokusudiwa,” amesema Rosemary.
Kwa maelfu ya taulo za watoto zilizotolewa, msaada huu unalenga kupunguza mzigo kwa familia na wahudumu wa afya, hususan katika siku za awali ambazo zinakuwa na changamoto nyingi kwa maisha ya mtoto mchanga.
Ikiwa imeanzishwa kwa lengo la mahsusi la kuhakikisha bidhaa za usafi wa mwili zinapatikana kwa urahisi na unafuu, Doweicare ndiyo kampuni ya kwanza nchini Tanzania kuzalisha taulo za watoto na taulo za kike kwa kutumia teknolojia ya ndani kupitia kiwanda chake kilichopo Lulanzi, Kibaha.
Mbali na kuzalisha bidhaa muhimu kwa bei nafuu, kampuni imejenga urithi wa kweli kwa jamii.
Hadi sasa, Doweicare imezalisha zaidi ya ajira 3,000 ikiwa ni ajira 1,000 za moja kwa moja na zaidi ya 2,000 zisizo za moja kwa moja huku ikichangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa kutambua uwazi wake kwenye rekodi za kifedha na maadili ya kibiashara, kampuni hiyo ilitajwa kuwa mlipakodi bora wa Mkoa wa Pwani kwa mwaka wa fedha 2024.
Mkurugenzi wa SUNDA GROUP Tanzania, Andy Liu ameishukuru Serikali ya Tanzania, akisisitiza mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji yaliyowezesha kampuni kukua.
“Tunatoa pongezi zetu za dhati kwa Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wenye maono wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji,” anasema Liu.
Anasema SUNDA GROUP, wanaamini katika nguvu ya mabadiliko ya ubia na uwekezaji wa ndani. Doweicare Technology Company Limited inaiishi ahadi hii. Sisi sio waagizaji tu; sisi ni wazalishaji halisi wa kitanzania. Dhamira yetu kuu ni kuzalisha bidhaa bora na muhimu za matumizi ya kila siku hapa nchini hususan bidhaa muhimu za usafi wa mwili kama vile nepi za watoto, taulo za kike, na taulo za watoto, zote zikiwa chini ya chapa maarufu ya “SOFTCARE”.
Kupitia uzalishaji wa ndani, tunalenga kuzalisha ajira endelevu, kukuza maendeleo ya kiuchumi, na zaidi ya yote, kuhakikisha kuwa bidhaa hizi muhimu za usafi wa mwili zinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu kwa familia za Kitanzania na barani Afrika kwa ujumla.
Uwekezaji huu mkubwa umeongeza uzalishaji wa ndani na kutoa ajira za moja kwa moja 1,000 pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 2,000, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii.
“Tukio la leo linaendana moja kwa moja na dhamira yetu. Tumekusanyika hapa kwa ajili ya kuchangia afya, utu, na faraja ya jamii zetu. Kwa fahari kubwa, tunatangaza mchango wa katoni 1,600 za nepi za watoto wachanga za Softcare zenye thamani ya Sh 65 milioni kwa Mkoa wa Dodoma.”
Anasema wataendelea kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuzalisha fursa, na kuunga mkono miradi inayoinua jamii wanazozihudumia. Kushirikiana na Serikali, sekta binafsi, na jamii katika kujenga mustakabali wenye afya bora, nguvu zaidi, na ustawi kwa wote.
Akizungumza kwa hisia, Zarina Hassan Tlale maarufu kama Zari, balozi wa chapa ya Softcare, alisisitiza kuwa chapa bora hujengwa kwa kusikiliza jamii.
“Tunapotoa diaper hizi, hatutoi bidhaa tu tunasambaza upendo, utu na matumaini kwa Watanzania,” alisema.