Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwongozo wa hedhi kuleta ahueni kwa wasichana Tanzania

Muktasari:

  • Mwongozo wa Taifa wa Afya na Usafi wa Hedhi wa mwaka 2025, unazielekeza shule zote za msingi na sekondari, kuwa na vyumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike kujistiri wakati wa hedhi, huku ukiielekeza Serikali kugharamia pedi shuleni.

Dodoma. Serikali imezindua Mwongozo Taifa wa Afya na Usafi wa Hedhi wa mwaka 2025, utakaowezesha shule na maeneo ya kijamii kutenga vyumba maalumu kwa ajili ya wanawake kujistiri wakati wa hedhi, huku Serikali ikigharamia pedi mashuleni.

Hatua hiyo imekuja ikiwa imepita miaka minane tangu kuwe na hekaheka za kampeni mbalimbali za kutaka taulo za kike ziondolewe kodi Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na kuishinikiza Serikali kupitia halmashauri kutenga fedha kushughulikia hilo.

Kuwepo kwa mwongozo huo, sasa kutazilazimu halmashauri nchini kuanza kutekeleza ugharamiaji wa bidhaa za hedhi shuleni kama zilivyoelekezwa hapo awali.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Mei 29, 2025 Katibu Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania Severine Allute amesema awali halmashauri zilielekezwa kutenga fedha kugharamia bidhaa hizo.

Amesema fedha hizo ni za uwezeshwaji wa shule, walimu wakuu walielekezwa kutenga asilimia 10 kugharamia bidhaa za hedhi pia.

“Serikali pia kupitia halmashauri, inatakiwa kutenga bajeti kuhakikisha watoto wanapata bidhaa hizo shuleni, ilikuwa maelekezo tu hakukuwa na mwongozo rasmi, lakini uwepo wa mwongozo huu utasaidia utekelezaji wa hili,” amesema Severine.

Pia, amesema wadau wa hedhi walifanya kazi bila miongozo kwa matakwa ya taasisi zao, lakini sasa mwongozo huo utasaidia utekelezaji wa kazi kwenye ubora na taratibu zilizowekwa.

Mwaka 2018 Serikali ilipiga hatua yenye mwelekeo sahihi wa kupunguza gharama anazoingia mwanamke kwenye kununua bidhaa za kujihifadhi wakati wa hedhi kwa kutoa kodi kwenye bidhaa ya pedi.

Lakini mwaka 2019 ukiwa umepita mwaka mmoja tangu kutolewa kwa kodi, Serikali iliirudisha tena kutokana na kudai kuwa wafanyabiashara hawajapunguza bei kama ilivyokusudiwa.

Mwongozo ni kitu kilichokuwa kikipiganiwa na wadau wa masuala ya hedhi, wakishinikiza kuwa ili kuwe na utekelezaji, lazima upatikane mwongozo.

Mwongozo huo wa kitaifa uliozinduliwa jana Jumatano, Mei 28, 2025 utawezesha shule pamoja na maeneo ya kijamii kama vile stendi, sokoni na ofisi za umma kuwa na chumba salama kwa ajili ya wanawake kujihifadhi.

Akitoa kauli hiyo mwakilishi wa Waziri wa Afya, Dk Otilia Gowele amesema kumekuwa na changamoto nyingi kuhusu hedhi salama, baadhi ya watu huhisi ni laana, bila kujua kuwa hedhi ni uhai wa msichana na mwanamke.

“Mwongozo huu sasa utakwenda kutatua baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili wasichana wakati wa hedhi, kama vile kuwa na vyumba salama kwenye vyoo vya mashuleni, kuelezea imani potofu zinazokinzana na hedhi salama pamoja na mambo ya kufanya na kutofanya msichana anapokuwa kwenye hedhi,” amesema Dk Gowele.

Amesema mwongozo huo pia unatoa dira ya ujenzi wa vyumba salama kwa shule na maeneo ya kijamii, ambayo bado hayajajengwa na kwa wale ambao wana vyoo vya zamani watapewa utaratibu wa kujenga vipya.

Katika mwongozo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe kabla ya kuusaini ameandika kuwa Tanzania kuna wanawake wapatao milioni 15 ambao wako katika kipindi cha hedhi kati ya jumla ya watu milioni 61.7.

“Ili waweze kudhibiti hedhi zao kwa usalama na kwa heshima, ni muhimu kuwa na upatikanaji wa taarifa sahihi za kuaminika na za kina, huduma bora za maji, usafi na mazingira safi, vifaa vya kujikinga wanavyovipendelea, pamoja na huduma na mazingira yenye msaada shuleni, katika jamii, sehemu za kazi, maeneo ya umma na katika mazingira ya kibinadamu,” ameandika Dk Shekalaghe.

Ongezeko la gharama kwa bidhaa ya pedi imekuwa ikipaa kwa kasi kutoka Sh1,500 mwaka 2017 mpaka kufikia Sh2,000 - 3,500 mwaka 2025.

Mwananchi iliangazia takwimu za Best za mwaka 2022, zinazoonesha wasichana wa zaidi ya umri wa miaka 13 ambao wanakadiriwa kuwa wamebalehe au kuelekea hatua hiyo ya ukuaji waliopo katika shule za msingi ni 413,955 na waliopo shule ya sekondari ni zaidi ya milioni 1.47.

Ikiwa Serikali itagawa pakiti ya pedi yenye thamani ya Sh2,000 kwa kila msichana aliyepo shuleni itatumia Sh827.91 milioni kwa mwezi; kwa mwaka itatumia Sh8.28 bilioni.

 Kwa upande wa shule za sekondari itatumia Sh29.53 milioni ambayo ni sawa na Sh29.53 bilioni kwa mwaka.

Takwimu hizo zinaashiria kuwa iwapo Serikali itafanya uamuzi wa kugawa pakiti moja ya pedi kwa kila msichana kwa kipindi cha miezi 10 ya mwaka anayokuwepo shuleni itatumia Sh3.781 bilioni kwa mwezi, ambayo ni sawa na Sh37.806 bilioni kwa mwaka, kiwango ambacho Wizara ya Elimu na Sayansi inaweza kutenga kwenye bajeti ya mwaka wa fedha.


Maoni ya wadau

Wanamtandao wa hedhi salama nchini, wamesema hiyo ni hatua kubwa waliyofanikiwa baada ya kuipigania kwa miaka mingi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca  Gyumi amesema kufikia nchi kuwa na mwongozo eneo hilo, inamaanisha sasa masuala ya hedhi salama yanaanza kupewa uzito unaostahili.

“Ni eneo mojawapo unaozingatia utu. Ili kufikia utekelezaji wake ni muhimu kuona wizara inaweka bidhaa ya pedi kwenye orodha ya bidhaa muhimu, kodi zote zitatoka na itakuwa rahisi kuangalia suala la upatikanaji wake.

“Kodi isitozwe, Serikali inaweza pia kuangalia mkakati mahususi kwa wasichana waliopo shuleni, ikawa na mpango wa kuzigawa bure kwani hedhi ina muunganiko na matokeo ya kwenye elimu, kuhakikisha namna gani wanabaki shuleni, msisitizo wangu Serikali ione umuhimu wa kuweka kipaumbele kuhakikisha bidhaa za pedi zinapatikana,” amesema Gyumi.

Kwa upande wake mdau wa hedhi salama kutoka Shirika la Afya Plus, Susan Yumbe amesema mwongozo huo ni faraja kwao kwa kuwa, wameupigania kwa muda mrefu, hivyo unaleta mwanga kwa wanafunzi wa kike kusoma hata wakiwa kwenye hedhi.

Ameishauri Serikali kuweka pedi za kike kama dawa muhimu ili zipatikane hata kwa kutumia bima ya afya, tofauti na sasa ambapo wananchi wengi wanashindwa kumudu kutokana na bei kuwa kubwa.

“Kuondoa kodi siyo tatizo. Tatizo linaweza kuwa lingine kabisa ambalo linalisababisha pedi kuuzwa bei kubwa, hivyo tunashauri pamoja na mwongozo huu lakini zipatikane kama dawa muhimu ambayo hata mtu akiwa na bima anaipata kwa gharama nafuu,” amesema Yumbe.

Naye Ofisa Masoko kutoka shirika lisilo la kiserikali la Days of Girls, Rose Kapama amesema kuzinduliwa kwa mwongozo huo ni hatua nzuri kwa wadau wanaopambania hedhi salama kwa kuwa sasa watakuwa na pakuanzia.

Amesema shirika hilo limekuwa likitengeneza taulo za kike na kuzigawa shuleni hasa kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia maskini.