Prime
Wanawake hawa hupata mimba wakati wa hedhi pekee

Muktasari:
- Wanawake wengi hupata hedhi kila baada ya siku 28 mpaka 33 za mzunguko wa mwezi, siku ya yai kupevuka inaweza pia kuwa ya 12, 13 14 au 15, siku hizi ndizo tunaziita siku za hatari.
Dar es Salaam. Kama ulidhani siku za kubeba ujauzito kwa mwanamke ni kuanzia siku ya 12 hadi ya 15, huku ukiilenga siku ya 14 kwamba ni lazima atapata ujauzito, basi umekosea.
Endapo unatafuta mimba kwa muda mrefu bila mafanikio au unataka kushika mimba haraka, ni muhimu kufuatilia kwa makini mzunguko wako wa hedhi kujua zipi siku za hatari.
Moja ya imani potofu sana kwa wengi ni kuamini mwanamke hawezi kushika mimba kwenye hedhi, ingawaje wanaume na hata wanawake asilimia kubwa hawawezi kushiriki tendo wakati huu.
Wataalamu wa afya ya uzazi wanakwambia lipo kundi la wanawake hawawezi kushika ujauzito isipokuwa kama watashiriki tendo wakati wa hedhi. Ni kwa namna gani? Mwananchi linakuchambulia;
Mkufunzi wa elimu ya afya ya uzazi, Mgeni Kisesa amesema wanawake wanaopata mimba wakati wa hedhi zao ni wale wenye mzunguko wa siku 21.
Amesema wanawake wengi hupata hedhi kila baada ya siku 28 mpaka 33 za mzunguko. Na wengi wao mayai hukomaa siku ya 14 baada ya hedhi, siku ya yai kutolewa inaweza pia kuwa ya 12, 13 14 au 15, siku hizi ndizo huitwa za hatari.
“Wanawake wenye mzunguko mfupi wa siku 21, siku yao ya kubeba ujauzito huwa inakuwa ya saba, lakini kupevuka kwa yai huanza siku tatu nyuma.
“Kupevuka kwa yai kutaanza siku ya tano na inapofika siku ya saba inakuwa ya kilele. Mwanamke huyu itokee kwamba yeye ile damu yake ya hedhi anaenda kwa siku saba kwa hivyo, akisubiri mpaka amalize hedhi ndipo ashiriki kama anatafuta mtoto hawezi kupata.
“Kwa sababu anapomaliza hedhi ile siku ya saba ndiyo inakuwa ilikuwa siku ya kupevuka kwa yai, kuanzia siku ya nane hawezi kupata mimba,” amesema Mgeni.
Amesema siku ya yai kupevuka na kutolewa inatofautiana kulingana na mzunguko wa mwanamke mmoja na mwingine. Baadhi ya wanawake wenye mzunguko mrefu wa siku mpaka 35, yai lao linaweza kupevuka siku ya 21. Na wanawake wenye mzunguko mfupi zaidi wanaweza kushika mimba hata siku ya saba ya hedhi.
“Sasa kwa mantiki hii, chukulia hedhi yako inachukua siku sita kuisha, umefanya mapenzi na mtu katika siku ya tano ya hedhi, na yai likapevuka siku ya saba na tunajua mbegu zinaweza kukaa siku mpaka sita ndani ya kizazi. Maana yake unaweza ukashika mimba ukikutana na mwanaume kwenye siku za hedhi yako,” amesisitiza.
Kujamiiana wakati wa hedhi
Maswali ya wengi ni kama kuna madhara yatakayotokea baada ya kujamiiana wakati wa hedhi, ambapo wataalamu wa afya wanasema kisayansi inakubalika, kwani kufika kileleni kunapunguza maumivu wakati wa hedhi na kupunguza idadi ya siku za hedhi
Lakini kidini, kitamaduni na kijamii kushiriki tendo katika hali hii inaelezwa kama ni uchafu na huharibu murua wa tendo hilo na hata msisimko unapungua kutokana na hali hiyo kuonekana inawaathiri wenza kisaikolojia.
Daktari wa binadamu, Samwel Shita amesema hakuna madhara, ingawaje lina athari za kiakili (hisia) kwani hofu, wasiwasi na woga kwa vijana wa kiume huwa juu kipindi hicho hutokana na kuona damu.
“Uwepo wa athari za kihisia kama vile woga hufifisha hamu ya kushiriki tendo hilo na kufikishana kileleni,” amesema.
Dk Shita ameeleza kuwa wataalamu waliotafiti maelfu ya wanawake wanaeleza kuwa kujamiiana wakati wa hedhi hakuna madhara kiafya, bali zipo faida kadhaa ikiwamo kuongeza kasi ya ushukaji wa hedhi kwa haraka hivyo kuisha mapema zaidi.
“Hii ni kwa sababu wakati mwanamke anapofika kileleni misuli ya nyumba ya uzazi hujikunja na hivyo tando laini (hedhi) hujinyofoa na kutiririka.
“Wakati wa kujamiiana mwanamke hupata hisia nzuri kutokana na kuzalisha kwa kichochezi (hormone) kinachojulikana kama Endophins ambacho hufanya mtu kuwa na hisia chanya ikiwamo furaha,” amesema Dk Shita.