Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaotumia dawa za kulevya kukata hedhi waonywa

Muktasari:

  • Baadhi ya madhara yanayoweza kupata ni kuvurugika kwa homoni na mzunguko wa hedhi, kansa na hata tatizo la ugumba.

Dar es Salaam. Wanawake wanaotumia mbinu mbalimbali, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya kukata hedhi, amesisitizwa kuacha tabia hiyo kwani inawaweka katika hatari ya kupata matatizo katika mfumo wa uzazi.

Baadhi ya madhara yanayoweza kutokea ni kuvurugika kwa homoni na mzunguko wa hedhi, kansa na hata tatizo la ugumba.

Hayo yamebainishwa Ijumaa ya Machi 28, 2025 na Mfamasia Mkuu kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Upendo Chenya, wakati akitoa mada katika mdahalo wa kitaifa ulioandaliwa na taasisi ya Msichana Initiative kuhusu masuala ya hedhi salama uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Chenya amesema matumizi ya dawa za kulevya, akitolea mfano wa bangi, cocaine na heroin, huwa na athari ya moja kwa moja katika mfumo wa uzazi.

Amesema kwa mwanamke, moja ya changamoto inayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya dawa hizo ni kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi na kusababisha mwanamke kuzipata kwa siku chache au kukosa kabisa.

"Hivyo, baadhi ya wanawake hasa wanaofanya biashara ya kuuza miili yao hutumia dawa hizo ili kukata hedhi, jambo hilo ni hatari kwani linakwenda kusababisha changamoto katika mfumo wao wa uzazi," amesema Upendo.

Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa Masuala ya Uzazi, Familia na Malezi, Dk Katanta Simwanza, amesema matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuathiri tezi za hypothalamus na pituitary zinazopatikana katika ubongo, ambazo ni muhimu katika udhibiti wa homoni, ikiwemo inazohusiana na mzunguko wa hedhi.

"Homoni zinazohusika na mzunguko wa hedhi ni pamoja na estrogeni na progesteroni, ambazo huhitajika ili kudumisha mzunguko wa hedhi wa kawaida Dawa za kulevya zinaweza kuvuruga uzalishaji wa homoni hizi, na kusababisha mzunguko wa hedhi kutokuwa wa kawaida au kutokuwepo kabisa," amesema.


Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk Isaya Mhando, amesema mchakato wa mzunguko wa hedhi huanzia katika ubongo, hivyo ukiathirika husababisha hata mzunguko wa hedhi kuvurugika.

Amesema, kutokana na mfumo wa hedhi kuvurugika, inaweza kuleta ugumu kwa mwanamke kupata ujauzito.

Pia, amesema matumizi ya dawa hizo kwa mwanamke yanamuweka katika hatari ya kupata ugumba kutokana na ubora wa mayai na mfumo wa uzazi kwa ujumla.

Hivyo, amewaonya wanawake wanaofanya hivyo kwani ni hatari kwa mfumo wa uzazi na afya ya mwili na akili kwa ujumla.


Elimu kuendelea kutolewa

Katika hatua nyingine, wadau wamesema kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kuhusiana na dhana potofu zilizopo kwenye jamii kuhusu hedhi.

Ofisa miradi kutoka taasisi inayojishughulisha na haki za wanawake wa kifugaji (PWC), Nang'ambo Mollel, amesema pamoja na jitihada zinazofanyika, bado kuna kazi kubwa ya kuielimisha jamii kuondokana na imani potofu.

"Sisi wasichana vinara tunaamini hedhi ni tunu, na ni mwanzo wa maisha ya mwanadamu na hivyo ni suala linalopaswa kupewa kipaumbele kwa ustawi wa wasichana na Taifa letu kwa ujumla," ameeleza.

Akizungumza kwa niaba ya wasichana wengine, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Emanyata iliyopo Arusha, Elizabeth Mollel, amesema, kutokana na baadhi ya wasichana kushindwa kumudu gharama za kupata taulo za kike kila mwezi, huishia kutumia vifaa kama vipande vya nguo, majani ya miti, na vifaa vingine ambavyo si salama kwa afya.

Elizabeth amesema pakiti moja ya taulo za kike inauzwa kwa Sh2000 na inaweza kuwa juu zaidi kulingana na kampuni na mahali, na msichana atahitaji kuanzia pakti mbili na zaidi ili kukamilisha mzunguko wake wa hedhi wa mwezi mmoja.

"Ukiangalia gharama hii ni kubwa, hasa kwa wasichana wanaotoka katika kaya maskini ambazo taulo za kike si kipaumbele katika bajeti ya familia.

“Ukosefu wa taulo za kike unachangia wasichana kujiingiza katika tabia hatarishi na kuingia katika mahusiano katika umri mdogo ili apate fedha zitakazomuwezesha kununua taulo hizo," amesema.

Ameongeza sambamba na kutoa pedi bure na kuondoa kodi kwenye taulo za kike, bado kuna umuhimu wa kuwa na vyumba salama vya kujihifadhi wanapokuwa shuleni.

"Ukosefu wa mazingira salama ya kujihifadhi shuleni ni moja ya sababu inayochangia utoro wa wasichana kwa siku tatu hadi saba kila mwezi," ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, amesema kuwa wao kama moja kati ya taasisi zinazotetea haki za wasichana, itahakikisha sauti za mabinti hao zinasikika ili mamlaka husika zione ni namna gani inazifanyia kazi.