Mvuruguko wa homoni, moja ya sababu zinazochangia ugumba

Muktasari:
- Tatizo la kuharibika kwa uwiano wa homoni mwilini ikijulikana na watu wengi kama tatizo la ‘Hormone Imbalance’, linaweza kumtokea mtu yeyote awe mwanaume au mwanamke.
Tatizo la kuharibika kwa uwiano wa homoni mwilini ikijulikana na watu wengi kama tatizo la ‘Hormone Imbalance’, linaweza kumtokea mtu yeyote awe mwanaume au mwanamke.
Kuharibika kwa uwiano wa homoni mwilini hutokana na kupungua au kuongezeka kwa homoni kwenye damu. Mabadiliko yanaweza kuwa kidogo, lakini bado yakawa na dalili za kuonekana.
Waathirika wakubwa wa tatizo hili ni wanawake ambao wanahangaika kusaka tiba hospitalini na sasa hasa hata kwenye mitandao ya kijamii.
Tatizo hili ni moja ya sababu inayochangia ugumba kutokana na vichocheo kutokuwa katika uwiano sawa.
“Kilikuwa ni kipindi kigumu kwangu hususani nilipokuwa nikitafuta ujauzito bila ya mafanikio na nisijue nini tatizo.
“Baada ya kujaribu njia tofauti, ndipo hospitalini waliniambia kuwa nina tatizo la hormone imbalance ambayo inanifanya upataji wa mimba kuwa mgumu kwa sababu kuna homoni zinatakiwa mimi nazikosa,” anasema Martha Jailos, ambaye ni mkazi wa Tabata.
Hali hiyo hushuhudiwa si kwa wanawake tu, bali hata baadhi ya wanaume hukumbwa na tatizo hili, jambo linalowasababishia baadhi ya vitu kutoonekana kuwa vya kawaida kwao.
Miongoni mwake ni vitu hivyo ni kuwa na matiti, kutoota ndevu au kuwa na muonekano ambao huwafanya watu kushindwa kumuelewa.
“Sijui kwanini sina ndevu na sioni kama ni tatizo,” anasema Jonathan Julius.
Wawili hawa wanawakilisha watu ambao wamekuwa wakikikabiliana na tatizo la ongezeko au upungufu wa vichocheo (homoni) katika mzunguko wa damu ambao wengi wamekuwa hawajui hasa vyanzo vya shida zao.
Baadhi wamejikuta wakihangaika huku na kule kutafuta msaada, huku wengine wasijue cha kufanya ili kuondokana na tatizo hilo.
“Nilikuwa sijui chochote hata nilipoambiwa hospitali ni hormane imbalance ndio tatizo nililonalo nilikubali tu, lakini sikuwa nimeelewa ina maana gani na inasababishwa na nini,” anasema Martha.
Kwa mujibu wa Dk Goodlove Godwin, Mkurugenzi wa Lifelight foundation Tanzania anasema tatizo hilo hutokea baada ya moja kati ya tezi ya mfumo wa homoni (endocrine gland) kushindwa kuzalisha kemikali za kutosha au kuzalisha kwa kiwango cha juu.
Unapozungumzia vichocheo au homoni inamaanisha kemikali zinazozalishwa na tezi.
Anasema licha ya kuwa tatizo hili huwapata watu wa jinsia zote, lakini wanawake wanaonekana kuwa waathirika wakubwa kuliko wanaume.
Kwa mujibu wa DK Godwin, wanawake wamekuwa wakipata zaidi tatizo hili tofauti na wanaume kwa sababu mifumo yao ya homoni na mizunguko yake ni tofauti na ya wanaume, pia ni mingi zaidi hasa katika ukuaji wao na maumbile.
Anabainisha kuwa mwanamke anaweza kupata tatizo hilo iwapo ovari zake zitakua bila mpangilio ikiwa na maana ya tatizo la (polycystic ovarian syndrome).
“Utumiaji wa dawa za kuzuia mimba au njia yoyote ya kuzuia mimba pia huweza kumfanya mtu kupata tatizo la hormone imbalance.
“Namna ya kuzuia mimba ikiwemo vijiti, vitanzi vyote huathiri mfumo wa mzunguko wa homoni labda badala ya kutoka zinarundikana sehemu fulani,” anasema Dk Godwin.
Anasema pia mwanamke kufikia ukomo wa hedhi (menopause) mapema kabla ya miaka 45 nayo hutajwa kama moja ya sababu ya tatizo.
“Mtu pia akiwa na saratani ya ovari huwa kunakuwa na uzalishaji mkubwa wa homoni, jambo ambalo husababisha tatizo hili,” anasema.
Wakati hivyo vikitajwa kuwa visababishi kwa upande wa mwanamke, kwa mwanaume imetajwa kuwa tatizo hilo hutokea kwa nyakati mbili kuu ambazo ni ule wa kubalehe na umri unapoongezeka.
“Pia na mwanaume anaweza kuwa kwenye hatari ya kupata hormone imbalance iwapo atapatwa na saratani ya tezi dume au atapatwa na hali ya kutoa mbegu chache za kiume (low testosterone).
“Hivyo ukilinganisha sababu za upande wa mwanamke na mwanaume utaona tatizo hili limeegemea sana upande wa wanawake kwa sababu ya kuwa na mizunguko mingi tofauti na wanaume,” anasema Dk Godwin
Watu wanaosumbuliwa na tatizo hilo pia huweza kukumbana na changamoto nyingine ambayo pia hutofautiana kati ya mwanamke na mwanaume.
Kwa wanawake huweza kusumbuliwa na tatizo la ugumba kutokana na homoni huenda kuwa nyingi au chache katika mzunguko wa damu ambazo zitafanya utungaji mimba kuwa mgumu.
Pia kuongezeka uzito, uke kuwa mkavu, kupata maumivu ya matiti, kuota nywele kwenye uso, kifua, shingo ni miongoni mwa vitu anavyoweza kukutana navyo mwanamke aliye na tatizo hilo.
“Wakati mwingine mtu hutokwa jasho sana wakati wa usiku au kupata hedhi isiyokuwa ya kawaida hata muda ambao si wa hedhi na maumivu makali wakati wa hedhi na asijue nini tatizo, kumbe homoni zake haziko sawa,”
Pia maumivu ya mifupa na ngozi kudhohofika ni miongoni mwa vitu ambavyo mwanamke aliye na tatizo la homoni, lakini kwa mwanaume huwa ni kukosa hamu ya kufanya mapenzi, uume kutosimama, kutoa manii chache na baadhi kuota matiti.
“Hii ya kuota matiti ni sawa na ile ya wanawake kuwa na ndevu au nywele katika kifua na shingo sababu kubwa huwa ni homoni zao kutokuwa sawa,” anasema Dk Godwin
Pia kutokuota nywele au kuota chache na inaweza kuwa ndevu na kupata maumivu ya matiti ni miongoni mwa matatizo yanayoweza kusababishwa na homoni kutokuwa sawa.
Lakini kila tatizo huwa na namna ambavyo mtu huweza kuliepuka kwa kuufanya uzito wa mwili wake kuendana na urefu wake.
Hiyo ni kwa sababu kila mtu kuna uzito anaopaswa kuwa nao kulingana na urefu wake, hivyo unapozidi anatakiwa kuupunguza kwani bila kufanya hivyo huweza kumletea matatizo.
Kula mlo kamili ni moja ya njia inayotajwa kusaidia mtu kuepukana na tatizo la hormone imbalance na ili mlo kuwa kamili ni lazima uambatane na mbogamboga pamoja na matunda.
Kufanya mazoezi, kupunguza msongo wa mawazo, kupunguza vyakula vyenye sukari na vyakula vilivyofungashwa ni miongoni mwa njia zinazoweza kumfanya mtu kuepukana na tatizo hili.
“Kuacha kutumia vipodozi hasa vya kujichubua, kula matunda ambayo hayajapuliziwa kemikali, kutokula vyakula vilivyopashwa kwa kutumia plastiki au microwave pia huweza kusaidia kuepukana na tatizo hili,”
Sambamba na hilo pia matumizi sahihi ya dawa iwapo mgonjwa ataelekezwa na daktari ni miongoni mwa vitu vinavyoweza kumuepusha mtu na tatizo hili.
Mbali na hayo yote, pia daktari anabainisha kuwa vipo vidonge ambavyo baadhi ya watu hutumia ili kuweka homoni zao katika usawa kulingana na ushauri wa daktari
“Lakini kubwa ni kubadilisha mfumo wa maisha, tabia na kufanya mazoezi.”