Zambia, Nigeria zaanza kwa vipigo Olimpiki

Muktasari:
- Timu za soka za wanawake za Afrika, Zambia na Nigeria, zilianza vibaya katika mashindano ya Olimpiki 2024 nchini Ufaransa. Zambia ilifungwa 3-0 na Marekani katika Kundi B, huku Nigeria ikifungwa 1-0 na Brazil katika Kundi C.
Dar es Salaam. Timu za soka za wanawake zinazoiwakilisha Afrika katika mashindano ya Olimpiki 2024 yanayofanyika nchini Ufaransa, Zambia na Nigeria zimeanza vibaya baada ya kupoteza mechi zao za kwanza hatua ya makundi.
Zambia iliyo Kundi B, ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Marekani wakati Nigeria ikifungwa 1-0 na Brazil katika mchezo wa Kundi C. Mechi zote hizo zilichezwa Alhamisi Julai 25, 2024.
Marekani chini ya Kocha Emma Hayes, ilijihakikishia ushindi mapema tu kipindi cha kwanza kwani hadi kufikia dakika ya 25, walikuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Trinity Rodman (dk 17) na Mallory Swanson (dk 24 na 25), huku Zambia ikimaliza pungufu ya mchezaji mmoja kutokana na Pauline Zulu kuonyesha kadi nyekundu dakika ya 34.
Zambia na Nigeria zina nafasi ya kujiuliza katika michezo inayofuatia itakayochezwa Julai 28, 2024 ambapo Zambia itakabiliana na Australia wakati Nigeria ikicheza dhidi ya Hispania.
Matokeo ya mechi zingine zilizochezwa Julai 25, 2024 ni Canada 2–1 New Zealand, Ufaransa 3–2 Colombia, Ujerumani 3-0 Australia na Hispania 2-1 Japan.
Katika michuano hiyo upande wa soka la wanawake, yamepangwa makundi matatu, Kundi A lina timu za Ufaransa ambao ni wenyeji, Canada, Colombia na New Zealand. Kundi B ni Ujerumani, Marekani, Australia na Zambia wakati Kundi C kuna Hispania, Brazil, Japan na Nigeria.
Baada ya kumalizika hatua ya makundi, timu mbili za juu kila kundi zitafuzu moja kwa moja kwenda robo fainali huku mbili zingine zitapatikana kwa njia ya best loser kufanya idadi ya timu kuwa nane.