Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simbu, Geay wawekewa Sh134 milioni wabebe medali Olimpiki

Timu ya Taifa ya Riadha ya Tanzania ikiendelea kujifua katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Ilboru jijini Arusha kwa ajili ya maandalizi ya Olimpiki 2024. 

Wakati kesho Ijumaa Julai 25, 2024 ufunguzi rasmi wa Olimpiki 2024 ukitarajiwa kufanyika katika Jiji la Paris nchini Ufaransa, wanariadha wa Tanzania watakaoshiriki wamewekewa donge nono endapo watashinda medali.

Wanariadha hao ni Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri ambao wote wanakimbia mbio ndefu kilomita 42.

Fedha hizo zitatolewa kama bonasi na mdhamini mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Kampuni ya Xtep ambapo mwanariadha ambaye atapata medali ya dhahabu kwa maana ya kushika nafasi ya kwanza atazawadiwa dola 50,000 ambazo ni zaidi ya Sh134 milioni za Tanzania.

Mshindi wa medali ya fedha atazawadiwa dola 30,000 (zaidi ya Sh80 milioni za Tanzania) na mshindi wa medali ya shaba atapewa Dola 20,000 (zaidi ya Sh53 milioni za Tanzania).

Akizungumza na Mwanachi, Katibu wa RT, Jackson Ndaweka amesema bonasi hiyo imeongeza ari ya upambanaji kwa wanariadha hao ambao wamebeba jukumu la kuiwakilisha Taifa kwenye michezo ya Olimpiki.

“Hivi ni moja ya vitu ambavyo vinawapa motisha wachezaji wetu kwa sababu wanajua mashindano ya Olimpiki kwa kawaida Kamati ya Olimpiki haitoi zawadi ya fedha na mshiriki huwa anaenda kukimbia kwa ajili ya nchi yake na kujitengenezea fursa ya masoko.

“Kwa sasa mwanariadha wetu akienda kushiriki anafahamu kwamba atakapopata medali basi kuna donge kubwa la fedha atapata pia,” alisema Ndaweka huku akibainisha kwamba wanariadha hao wanaweza kukosa fursa ya kupata bonasi hiyo hata kama wakishinda endapo watashiriki Olimpiki kwa kuvaa sare tofauti na za mdhamini huyo ambaye ametoa vifaa vya michezo kwa timu hiyo ya riadha iliyoweka kambi Sakina jijini Arusha. Wanariadha hao wanatarajiwa kukimbia Agosti 10 mwaka huu kwa upande wa wanaume na Agosti 11 wanawake.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa 206 yanayoshiriki Olimpiki mwaka huu ambapo itawakilishwa na wanamichezo saba ambao ni wanariadha wanne Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri, waogeleaji wawili Collins Saliboko na Sophia Lattif na mcheza judo Mlugu Thomas.

Bendera ya Tanzania itaanza kupeperushwa Julai 29 pale ambapo Mlugu atakaposhiriki mchezo wa judo katika uzito wa kilogramu 73 super middle, kisha Julai 30 ni zamu ya Saliboko katika mchezo wa kuogelea mita 100 mtindo wa butterfly, huku Agosti 3 Sofia akiogelea mita 50 mtindo wa butterfly. Baada ya hapo, riadha wanaume Simbu na Geay watakimbia Agosti 10 na Agosti 11 zamu ya Sakilu na Magdalena.