Geay hatihati kushiriki Olimpiki, daktari aeleza tatizo

Muktasari:
- Mwanariadha Gabriel Geay, anayesumbuliwa na majeraha ya mguu, huenda akakosa kushiriki Olimpiki jijini Paris.
Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kufunguliwa kwa michezo ya Olimpili itakayofanyika jijini Paris, Ufaransa kambi ya Tanzania imeanza kupatwa na hofu.
Hofu hiyo inatokana na hali ya kiafya ya mwanariadha wake tegemeo, Gabriel Geay kusumbuliwa na majeraha na huenda akashindwa kuchuana kwenye michezo hiyo.
Mbali na Geay, wanariadha wengine waliofuzu kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki ya msimu huu, ni Alphonce Simbu, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu ambao watakimbia Agosti 10 na 11, 2024.
Hata hivyo, Daktari wa timu ya Tanzania kwenye michezo hiyo, Eliasa Mkongo amesema nyota huyo atasafiri na timu kwenda Ufaransa kwenye michezo hiyo itakayofunguliwa Julai 26.
Amesema, Geay ambaye ana maumivu ya mguu wa kulia kwenye kifundo ataendelea kufuatiliwa afya yake kama atamudu kukimbia ama la.
"Kwa jinsi hali yake ilivyo na siku zilizosalia kabla ya mbio ya marathoni, kuna uwezekano afya yake ikaimarika na kukimbia," amesema daktari huyo.
Wanariadha hao wanatarajiwa kuondoka nchini Agosti 7, 2024 kwenda Paris wakati timu nyingine ya Tanzania ya judo na kuogelea pamoja na watu wengine wakiondoka leo Julai 23, 2024.
Akizungumza kabla ya kuondoka, Dk Mkongo amesema kwa majeraha ya Geay anaweza kuendelea na matibabu na kuimarika kwa siku zilizosalia na akakimbia kwenye Olimpiki .
"Amekuwa mwenye majeraha hayo kwa wiki mbili, ambayo kwa wanariadha wa mbio ndefu hayo ni maumivu ya kawaida.
"Gaey ana maumivu lakini si kwa kiwango cha juu, amekuwa anapata maumivu akishamaliza kufanya mazoezi, lile eneo la kifundo linavimba.
"Siku timu inaagwa (Ijumaa iliyopita) Geay hakuwepo alikuwa anafanya baadhi ya vipimo, ikiwamo cha MRI, tulishauriana na mchezaji mwenyewe alikuwa tayari kuwakilisha nchi yake kwenye Olimpiki.
Anasema amemshauri apumzike kidogo na wameona ni vema asafiri na timu kwa kuwa nchini Ufaransa kuna madaktari wote, hivyo itampa nafasi ya kufanyiwa vipimo zaidi kwa muda uliobaki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema Geay atasafiri na timu wakati afya yake ikiendelea kuimarika na huenda muda wa kukimbia ukifika atakuwa ameshapona.
"Taarifa yake ya kuumwa tumeipata siku timu inaagwa, tulijua anaendelea na mazoezi.
"Tulipoambiwa Geay ana majeraha hayo, tulimtuma daktari kwenda Arusha kuchukua vipimo ili tuone tunamsaidiaje na daktari ameshauri asafiri na timu, kuna uwezekano hadi kufika siku ya mbio yake atakuwa ameimarika," amesema.
Rais wa TOC, Gulam Rashid amesema kwenda kwa Geay Paris ni kuangalia kama ataimarika na kupata madaktari zaidi wa kumtibu akiwa kule.
"Kukimbia au kutokimbia itategemea na afya yake itakavyokuwa, taratibu zake za safari zilishafanyika na hata asipokwenda hakuna ambacho kitapunguza gharama au kuongeza kama atakwenda.
"Hata kama hatashiriki mbio yake, hiyo itakuwa ni nafasi nzuri kuonana na madaktari ili kuangalia zaidi afya yake, tunachojua Geay yupo kwenye safari na hakuna tunachoweza kupoteza hata asipokwenda Paris," amesema Gulam.