Yanga yamaliza nuksi ikiichapa AS FAR Rabat
Muktasari:
- Katika Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Yanga imepangwa kundi B na timu za Al Ahly, AS FAR Rabat na JS Kabylie.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Yanga imeibuka na ushindi katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika baada ya leo, Jumamosi, Novemba 22, 2025 kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.
Kabla ya hapo, Yanga haikuwahi kupata ushindi katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi katika mara sita tofauti ambazo iliwahi kushiriki ama katika Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika.
Aliyeitoa Yanga kimasomaso katika mechi ya leo ni Prince Dube ambaye amepachika bao hilo pekee katika dakika ya 58.
Dube amefunga bao la kuongoza akimalizia kwa shuti la mguu wa kulia, pasi ya Mudathir Yahya.
Hilo limekuwa bao la kwanza kwa Dube baada ya kucheza mechi saba mfululizo za mashindano tofauti bila kufumania nyavu.
Ikumbukwe kabla ya hapo, mara ya mwisho kwa Dube kufunga ilikuwa ni katika mchezo wa ugenini wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete ya Angola, Septemba 19, mwaka huu ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Katika mchezo wa leo, Yanga ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Celestin Ecua, Mudathir Yahya, Prince Dube na Maxi Nzengeli na kuwaingiza, Edmund John, Lassine Kouma, Mousa Balla Conte na Andy Boyeli.
AS FAR Rabat iliwatoa Ouarkhane Khalid, Reda Slim, Ahmed Hammoudan na Zineddine Derrag na kuwaingiza Abdelfettah Hadraf, Hamza Khabba, Soulaimane El Bouchqali na Achref Habbassi.
Kikosi cha Yanga kilichoanza katika mchezo wa leo kilikuwa na Djigui Diarra, Israel Patrick, Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Abdullah, Duke Abuya, Celestin Ecua, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Prince Dube na Pacome Zouzoua.